
HISTORIA FUPI YA MAISHA YAKE
“Mimi ni mtoto wa tatu kati ya wanne, katika familia yetu. Tulizaliwa Kijiji cha Masimba wilayani Kisarawe, Pwani, nimebaki na mama baada ya baba kufariki dunia mwaka 2010.
“Sina elimu yoyote, kwani sijawahi kwenda shule hata chekechea, naamini wazazi wangu walichangia.
“Mwaka 1997, kutokana na ugumu wa maisha niliamua kuja jijini Dar kutafuta, nikawa nafanya kibarua katika Machinjio ya Vingunguti
“Mwaka 1999 nilimuoa Aisha Salum. Mwaka 2002 akajifungua mtoto wetu wa kwanza, tukampa jina la Sikujua. Kwa bahati mbaya alifariki dunia. Hapa naomba ieleweke kwamba mpaka wakati huo sikuwa na tatizo hili la mguu.
“Mwaka 2005 Mungu akatupa mtoto mwingine, tukampa jina la Mwajuma. Wakati huo nilikuwa naendelea na shuguli zangu za machinjioni na nilikuwa nikiishi kwa mapenzi makubwa na familia yangu kule Vingunguti.
TATIZO LAANZA
“Mwaka 2008 katika hali ambayo sikuitarajia, mguu wangu wa kulia ulianza kuuma na kuvimba. Nilishangaa ingawa si kwa kiwango cha kufikiria hali hii, baadaye kwenye uvimbe kulipasuka na kutoa usaha mwingi na harufu kali.
“Niliamua kwenda Hospitali ya Amana kisha Muhimbili bila mafanikio, madaktari waliniambia huenda nilikuwa na tatizo la tende. Mguu uliendelea kutoa harufu kali sana, hata mimi nilitamani usiwe wangu.
WAPANGAJI WAMTENGA, WAOMBA AFUKUZWE
“Niliumia zaidi baada ya kubaini kwamba wapangaji wenzangu walianza kumlalamikia mwenye nyumba na kutishia kuhama kama hatanifukuza mimi,” Seleman alianza kulia hapo akidai kuwa akikumbuka anaumia sana.
“Mwenye nyumba ingawa alikuwa ananipenda lakini ilimbidi aniambie ukweli kwamba nitafute pa kuelekea.
“Siku ananiambia zilibaki siku tatu kodi ya nyumba iishe, kwa hakika hakuna aliyenipenda kutokana na harufu ya huu mguu. Kuna wakati hata mke wangu alikuwa akinichukia.
“Ni binti yangu pekee ndiye aliyekuwa akinipenda, mke wangu alifika mahali akawa hataki tulale kitanda kimoja, alinishusha chini akidai nanuka. Ilibidi nifanye hivyo.
MKE AINGIA MITINI
“Siku moja mke wangu akaniambia kuwa amepata chumba kule Yombo, akashauri tukaishi huko. Mimi nilikuwa nina watu nawadai kama shilingi laki tatu (300,000/-), nilitafuta pikipiki ili kwenda kudai fedha hizo ili nimpe mke wangu akalipie hicho chumba.
“Niliporudi jioni sikumkuta, alichukua kila kitu kisha akatoweka na mwanangu. Niliumia sana na nilichanganyikiwa. Nilimpigia simu na kumuuliza nini kilimpata, akaniambia mkataba wa kuishi na mimi uliishia pale, akakata simu na kuanzia hapo ikawa hapatikani tena.
Tags
Matatizo haya