Mkutano wa kujadili Usalama Nigeria



Rais Goodluck Jonathan Rais Goodluck Jonathan
Mkutano wa kitaifa nchini Nigeria ulianza Jumatatu ya jana chini ya hatua kati za kiusalama. Mkutano huo unaofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja, ulifunguliwa kwa hotuba ya Rais Goodluck Jonathan wa nchi hiyo na unahudhuriwa na karibu shakhsia 500 wa kidini, kisiasa na kikabila. Malengo ya mkutano huo ni kujadili masuala muhimu ya nchi hiyo na kuleta umoja na mshikamano baina ya wananchi wa nchi hiyo yenye wakazi wengi zaidi barani Afrika. Mustakbali wa Nigeria, namna ya kupambana na vitendo vya utumiaji mabavu vya wanamgambo wa Boko Haram, ufisadi mkubwa serikalini na kugawanywa pato la nchi linalotokana na utajiri wa taifa bila kusahau kuchunguza manufaa ya muundo wa kisiasa wa nchi ni miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele katika mkutano huo. Akihutubia katika kikao cha ufunguzi, Rais Gooluck Jonathan wa nchi hiyo alisisitiza kwamba, mkutano huo wa kitaifa ni fursa muhimu ya kujenga miundo mbinu imara ya ustawi wa haraka, mshikamano zaidi na maendeleo ya Nigeria. Akiwahutubia hadhirina wa mkutano huo, Rais wa Nigeria aliwataka wananchi na serikali kufanya hima ya kuleta uhuru, amani na umoja katika nchi hiyo. Chama cha upinzani cha "All Progressives Congress" (APC) kimekosoa vikali matumizi makubwa ya Naira bilioni saba kwa ajili ya kuandaa mkutano huo. Pamoja na hayo, viongozi wa chama hicho walitarajiwa kukutana leo katika kikao cha dharura  ili kuchukua uamuzi wa kushiriki au kutoshiriki kongamano hilo. Kwa mtazamo wa chama hicho cha upinzani ni kuwa, malengo ya mkutano huo ni sawa na mkengeuko katika siasa za sasa za serikali na sio kwa maslahi ya wananchi wa Nigeria hata kidogo. Baadhi ya magazeti ya Abuja nayo yamezungumzia wazi jambo hili kwamba, kusambaratika mazungumzo katika mkutano wa kitaifa kutakuwa ni kikwazo kikubwa katika mwenendo wa mazungumzo hayo ambayo filihali yanaandamwa na wimbi la ukosoaji kutokana na ufujaji mkubwa wa fedha zilizotumika kuandaa mkutano huo.  Baadhi ya vyombo vya habari vinaamini kwamba, hakuna wakati ambao wananchi wa Nigeria walikumbwa na hitilafu za kikaumu, kisiasa na kimadhehebu kama ilivyo hivi sasa, hali ambayo imelifanya taifa hilo kugawanyika vipande vipande. Wakosoaji wa serikali ya Nigeria wanaamini kwamba, mikutano kama hiyo huandaliwa  kabla ya kufanyika uchaguzi kwa lengo la kutoa ahadi za uongo kwa wananchi. Uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Nigeria umepangwa kufanyika Aprili mwaka ujao wa 2015.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post