UNAPOANZA safari ya mapenzi, shika muongozo huu na uuamini. Amini katika mapenzi siku zote. Siyo tu yenyewe kama maneno, bali mapenzi katika maana na mzani wake sahihi. Amini kuwa zipo nyakati ngumu kwenye safari yako lakini simamia ushindi wako.
Endelea kuushika huu muongozo; Je, unaingia kwenye ndoa? Tambua kwamba ndoa si rahisi, ina changamoto nyingi. Unapoamua kuoa/kuolewa, hakikisha umejipanga kuzikabili changamoto zote na kuzishinda. Hakikisha changamoto za ndoa hazikushindi! Wenye imani, changamoto za ndoa tunaziita majaribu.
Amini kuwa watu hufanya makosa.
Kwa maana hiyo hata mwenzi wako anaweza kukukosea. Zingatia kwa heshima ya hali ya juu kuwepo kwa msamaha wenye uangalifu. Kwamba atakukosea lakini binadamu wote wanakosea, msamehe ila asirudierudie. Ikiwa anarudiarudia, basi usalama wako ni kumpa ‘baibai’.
Katika muongozo wangu, nakutaka pia ushike haya yafuatayo; Binadamu wana tamaa, kuna nyakati wanaweza kutaka mawili kwa wakati mmoja. Watu ni wabinafsi, vilevile ni wakarimu. Hivyo, upo uwezekano mwenzi wako akawa kwenye moja ya makundi hayo mawili.
Kama ni mbinafsi jitahidi kupambana kumbadilisha, anapokuwa mkarimu shukuru Mungu. Hata hivyo, kuna wengine wanakuwa wakarimu kupitiliza kiasi kwamba hata kuweka mipaka wanashindwa. Kama wako yupo hivyo, ni vema ukawa naye macho!
Tambua kwamba ni watu wachache sana huwa na dhamira ya kuwaumiza wapenzi wao. Muangalie mwenzi wako pindi anapokuumiza, je, kuna makusudi ndani yake? Uamuzi wako uzingatie dhamira yake. Unapogundua ni bahati mbaya, piga moyo konde, mfungulie ukurasa wa pili.
Pata muongozo pia kwamba wakati wowote lolote linaweza kutokea. Weka akilini kuwa ‘sapraizi’ ipo lakini hujui lini wakati wake. Mpo vizuri kabisa lakini usishangae kumfumania mwenzi wako. Lolote linaweza kutokea na ukapatwa na mshangao wa SMS kwenye simu ya mwandani wako.
Jina kwenye simu limeandikwa “muuza machungwa”, unaamua kupokea umwambie mwenye simu anaoga, unashangaa kukutana na sauti tofauti, mapenzi tu! Usije kuanguka kwa presha, ishi kwa kuamini ‘sapraiz’ ipo. Muamini lakini wengi hawaheshimu imani wanayopewa.
Yote sawa ila amini zaidi kwenye mwisho wenye furaha. Kinachobeba maana hapa ni jinsi ambavyo unaweza kubaki imara na kushughulikia tatizo katika namna bora kabisa. Hapa pia niseme kuwa uzuri wa kuvuka nyakati ngumu ni matokeo ya jumla ambayo åkuachana au kuvuka pamoja, angalia kinachokupa amani.
Weka akilini pia kuwa uhusiano haudumu kwa sababu ya uwepo wa nyakati nzuri. Kinachofanya udumu ni pale nyakati ngumu zinapopatiwa ufumbuzi kwa upendo na uangalifu. Usije ukadhani kuwa wote waliodumu hawakupita kwenye majaribu.
Unapoingia katika nyakati ngumu siyo kila mtu unaweza kumweleza matatizo yako. Bora usimwambie yeyote. Jitahidi kulala na kuamka ukitafakari, pengine ukapata ufumbuzi unaoridhisha. Jadili na uamue bila jazba, ni njia sahihi ya kukupeleka kwenye hatma yenye furaha.
Kuhusu watu wanaokuzunguka, wenye thamani kwako ni wale watakaocheka na wewe baada ya kuvuka kipindi kigumu. Chunga sana, wengi ni wambeya watakaokuwa wanaombea mabaya yasikuishe. Wengine wanaweza hata kununa pale wanapoona umeshinda changamoto.
0 Comments