Adam Kuambiana kuzikwa alipozikwa Kanumba


Marehemu Adam Kuambiana aliyeaga dunia juzi Jumamosi
SHABIKI wa Yanga na msanii wa filamu za maigizo nchini kutoka kambi ya Bongo Muvi, aliyejizolea umaarufu miaka ya hivi karibuni, Adam Kuambiana aliyeaga dunia juzi Jumamosi, anatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam alipozikwa msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Akizungumza na Championi Jumatatu, jana, Rais wa Bongo Muvi, Steve Mengere ‘Steve Nyerere’, alisema ratiba iliyopo ni kesho asubuhi waombolezaji kudamkia Muhimbili kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Viwanja vya Leaders Club kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika katika makaburi ya Kinondoni jijini.
Kiongozi huyo wa Bongo Muvi alisema bado hawajampata kiongozi wa kuongoza mazishi hayo lakini mpaka tunaelekea mitamboni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alithibitisha kuhudhuria mazishi hayo.
Akizungumza na gazeti hili rafiki wa marehemu ambaye ni msanii mwenzake na shabiki mwenzake wa Wanajangwani, Yanga, Rashid Makupa ‘Kupa’, alisema anakumbuka mechi ya mwisho kwenda naye uwanjani kuiangalia ni ile ya Simba na Yanga iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Kupa alisema katika vitu ambavyo anakumbuka kwa marehemu, ni kwamba alikuwa hapendi kitendo cha Yanga kukosa ushindi.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post