The Holy Sin - 28

ILIPOISHIA:ILE anajiandaa kutoka tu, alisikia mlango wa mbele wa nyumba yao ukigongwa kwa nguvu, harakaharaka akaficha begi lake chini ya meza na kuchungulia aliyekuwa akigonga. Hakuyaamini macho yake kwa alichokiona.

“Mungu wangu, nimekwisha,” alisema kwa sauti ya chini huku akitetemeka kuliko kawaida, kijasho chembamba kikawa kinamtoka.
 SASA ENDELEA…
“FUNGUA,” sauti kali ya baba Caro ilisikika kutokea nje huku akionyesha kuwa na jazba kali. Aidan alipochungulia vizuri, aligundua kuwa mzee huyo ‘mtata’ hakuwa peke yake bali aliongozana na wanaume wengine wawili ambao Aidan hakuwa akiwafahamu.
“Nitafanya nini mimi… eeh Mungu nisaidie,” alisema moyoni Aidan huku akipiga moyo konde na kwenda kufungua, akajiapiza kuwa kamwe hatakubali kuhusishwa na ujauzito ule wa Caro kwani haukuwa wake.
“Hata ikibidi kwenda kupima DNA nipo tayari,” alijisemea huku akifungua mlango, mwili mzima akitetemeka kwa hofu kubwa iliyouzingira moyo wake.
“Baba yako yuko wapi?”
“Sijui, ila nahisi ameenda kazini,” alijibu Aidan kwa sauti ya kutetemeka.
“Hayupo humo ndani?”
“Hayupo,” Aidan alijibu huku kijasho chembamba kikimtoka, akashangaa kumuona baba yake Caro akigeuza na kuanza kuondoka na wale watu. Alibaki akijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Alishindwa kuelewa kwamba kama yeye ndiye mshukiwa namba moja, kwa nini baba yake Caro aondoke bila kumuuliza wala kumfaya kitu chochote? Kengele ya hatari ikalia kwenye kichwa chake.
Alianza kuunganisha matukio, kuanzia siku aliyoenda na baba yake pamoja na Caro ufukweni kisha akatumwa katika mazingira ya ajabu akiwaacha baba yake na Caro wakiendelea kupunga upepo wa bahari.
Alikumbuka jinsi alivyopigiwa simu na mama yake na kuambiwa arudi kuendelea kufurahi ufukweni lakini alipofika akawakosa baba yake na Caro huku kukiwa hakuna anayejua wameenda wapi.
Aliendelea kukumbuka zogo kubwa lililoibuka siku hiyo baada ya baba yake kuchelewa sana kurudi nyumbani, tena akiwa na Caro na kusababisha hali ya sintofahamu nyumbani kwa wazazi wa msichana huyo.
Alikumbuka pia jinsi uhusiano kati ya familia hizo mbili ulivyovurugika baada ya siku hiyo, jinsi baba yake alivyokuja kukamatwa na polisi na yote yaliyoendelea baada ya hapo.
“Ina maana baba ndiye aliyetembea na Caro na kumpa ujauzito? Hapana, baba yangu hawezi kufanya kitu kama hicho, hapana, hawezi kabisa,” povu lilimtoka Aidan, akawa hataki kabisa kuamini kitu alichokuwa anakihisi.
Mpango wake wa kutoroka haukuwa na maana tena kwa sababu aligundua kuwa kumbe yeye siyo mhusika wa matatizo yaliyokuwa yakimuandama Caro. Akarudisha nguo zake chumbani kwake na kufunga mlango, akatoka mbiombio kurudi hospitali kwa lengo la kwenda kuwahoji vizuri mama yake pamoja na Caro juu ya mhusika wa ujauzito wa msichana huyo.
“Lazima watasema ukweli leo, nimechoka kuishi kama mfu,” alisema Aidan huku akikaza mwendo kuelekea kwenye stendi ya Bajaj. Hata hivyo, kabla ya kwenda hospitali, akili nyingine zilimtuma kwenda kwanza kazini kwa baba yake kumweleza juu ya ujio wa shari wa baba Caro nyumbani kwao.
Akamuelekeza dereva wa Bajaj kumpeleka moja kwa moja mpaka ofisini kwa baba yake. Dakika kadhaa baadaye, tayari Aidan alikuwa kwenye geti la kuingilia kazini kwa baba yake lakini kabla hajaingia, aliona kitu kilichomshtua mno.
Aliliona gari la baba Caro likiwa limeegeshwa pembeni kidogo ya geti la kuingilia kazini kwa baba yake, moyo ukamlipuka na mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda kwa kasi kubwa. Alijua kama baba Caro amekuja ofisini kwa baba yake, basi hakukuwa na usalama tena.
Akiwa bado anashangaashangaa kiasi cha kumshtua hata dereva wa Bajaj aliyokuja nayo, Aidan alipigwa na butwaa baada ya kumuona baba yake akitolewa mzobemzobe ofisini na wale wanaume wawili waliokuja na baba Caro, huku mwenyewe akimfuata kwa nyuma.
“Mungu wangu, kwani kuna nini,” Aidan alisema na kupita getini bila hata kusubiri idhini ya mlinzi, akakimbia mpaka pale baba yake alipokuwa. Akashtuka zaidi baada ya kugundua kuwa alikuwa amefungwa pingu mikononi.
“Baba! Baba, kwani kuna nini kinachoendelea? Mbona sielewi?” Aidan alimuuliza baba yake huku akilengwalengwa na machozi lakini baba yake hakumjibu kitu zaidi ya kujiinamia.
Wale wanaume wawili ambao kwa mwonekano walionyesha kuwa ni polisi, waliendelea kumkokota mzee Kenan mpaka getini. Wafanyakazi wengi waliokuwa wanafanya kazi na mzee huyo, wakaacha kila walichokuwa wanakifanya na kutoka kushangaa tukio hilo la ajabu.
“Kwa nini unamdhalilisha baba yangu? Kwani amekukosea nini,” Aidan alimfuata baba Caro na kuanza kumhoji huku akilia. Mzee huyo naye hakumjibu kitu zaidi ya kumsukumia pembeni na kupita. Aidan hakukubali kirahisi, akawa anawafuata nyuma huku akimporomoshea baba Caro lawama nyingi kwa kile alichokiita kuwa anamdhalilisha baba yake bila kosa.
“Baba yako ni zaidi ya shetani, amembaka mwanangu Caro na kumpa ujauzito halafu na wewe unamtetea, au mlishirikiana?” alifoka baba Caro huku akimsogelea Aidan kwa kasi, akawa anarudi nyuma huku akiwa haamini alichokisikia.
“Baba amembaka Caro na kumpa ujauzito?”
“Ndiyo, kama namsingizia si mwenyewe huyo hapo, muulize kama atabisha.”
“Eti baba, anachosema baba Caro ni kweli?”
“Nisamehe mwanangu,” alisema mzee Kenan, kauli ambayo ilizidi kumduwaza Aidan. Mwili ulimuisha nguvu, hakuweza hata kupiga hatua moja, akabaki amesimama palepale kama sanamu, akiwa amekodoa macho lakini haoni chochote.
Kilichomshtua baada ya muda mfupi, ilikuwa ni muungurumo wa gari la baba Caro ambalo ndani yake alikuwa amepakizwa baba yake, akiwa amefungwa pingu mikononi.
 Aidan alitamani iwe ndoto lakini haikuwa hivyo, alitamani dunia ipasuke na kummeza lakini bado haikuwezekana, alitamani baba Caro aje kumwambia kwamba alikuwa anamtania lakini hilo pia halikuwezekana.
Palepale akakaa chini na sekunde chache baadaye, uso wake ulikuwa umelowa chapachapa kwa machozi, huku akijihisi maumivu makali kwenye kifua chake, upande wa kushoto.

Je, nini kitafuatia? Usikose wiki ijayo.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post