humph the GREAT
KOCHA wa Yanga, Hans van Der
Pluijm, amesema ana matumaini na ameomba timu yake isifanye makosa
katika mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya MO Bejaia kwenye Uwanja wa
l’Unite Maghrebine jijini hapa.
Yanga inacheza na MO Bejaia mechi yake
ya kwanza ya Kundi A kuwania Kombe la Shirikisho Afrika na Pluijm raia
wa Uholanzi ana matumaini ya ushindi kwa kikosi chake.
Jambo linalosubiriwa kwa hamu na
mashabiki wa Yanga ni kuona beki wao mpya Hassan Kessy akiichezea timu
hiyo kwa mara ya kwanza akitokea Simba.
Katika mechi dhidi ya Yanga, Machi 20,
mwaka huu, Kessy akiichezea Simba alipiga pasi fupi iliyowahiwa na
straika Donald Ngoma (Yanga) kisha akafunga na kuzua mjadala wa Kampa
Kampa Ngoma.
Pluijm ana nafasi kubwa ya kumtumia
Kessy katika beki ya kulia ili kuziba nafasi ya Juma Abdul
anayesumbuliwa na maumivu ya enka, pia beki wa kati na nahodha Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ hayupo kikosini akitumikia adhabu ya kadi nyekundu.
“Baada ya kambi yetu ya Uturuki, tutaona
tulichopata, sitaki kumpa presha mchezaji yeyote yule. Soka ni mchezo
wa makosa, yeyote anaweza kufanya kosa na akajutia.
“Tunawajua wapinzani wetu na kuna sehemu
muhimu wapo makini na tayari tumezifanyia kazi, tuingie uwanjani na
matumaini ila hatutaki kufanya makosa,” alisema Pluijm, raia wa
Uholanzi.
Katika mchezo wa kesho utakaochezeshwa
na mwamuzi Bouchaib El Ahrach raia wa Morocco, Pluijm anaweza kumtumia
beki wa kati Andrew Vincent ‘Dante’ katika nafasi ya Cannavaro akicheza
sambamba na Kelvin Yondani kwani Vincent Bossou anayetumika mara kadhaa,
amefanya mazoezi siku chache baada ya kuchelewa kujiunga na kambi ya
Uturuki.
Yanga iliyoingia kambini Uturuki
Jumapili iliyopita, iliondoka nchini humo kuelekea Algeria ambako
ilifika jana saa 7:00 mchana tayari kwa mechi ya kesho. Yanga
inatarajiwa kupangwa hivi: Deo Munishi ‘Dida’, Kessy, Oscar Joshua,
Dante, Yondani, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Ngoma,
Amissi Tambwe na Deus Kaseke.
Katika mchezo mwingine wa Kundi A kesho,
TP Mazembe ya DR Congo itacheza na Medeama ya Ghana kwenye Uwanja wa TP
Mazembe, Lubumbashi, DR Congo.
Tags
Michezo na burudani