humph the GREAT
Jackson Mayanja
Nicodemus Jonas na Wilbert Molandi
KWA kiasi kikubwa Simba
imeshamalizana na Kocha Mghana, Sellas Tetteh Teivi ili aje kukinoa
kikosi hicho msimu ujao katika safari ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu
Bara.
Sasa kali zaidi ni kwamba, kocha huyo
ndiye atakayetoa ruhusa ya kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Jackson
Mayanja kwamba aendelee na kazi au apigwe chini.
Teivi amewahi kukinoa kikosi cha timu ya
vijana ya Ghana na sasa akiwa na Sierra Leone amekabidhiwa hatma ya
Mayanja ambaye mkataba wake wa awali unamtambulisha kama kocha msaidizi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema,
uongozi unasubiri ujio wa kocha mpya ili atoe pendekezo lake kama
ataendelea na Mayanja au atakuja na msaidizi wake kwani kila mwalimu ana
falsafa zake.
Habari zinasema, sekretarieti ya Simba
imeliacha suala la Mayanja kwa Teivi ila wao sasa wanaendelea na
mchakato wa kumpata kocha mpya wa makipa.
“Suala la kocha msaidizi tumeliacha
kwanza, unajua makocha wengi wanapenda kuja na wasaidizi wao, iwapo huyu
atakuja mwenyewe, basi atafanya kazi na Mayanja lakini kama atakuja na
mwenzake, haina jinsi pia tunamsikiliza.
“Lakini sisi kama kamati (ya utendaji)
kila mmoja anataka Mayanja tuendelee naye kutokana na kazi kubwa
aliyoifanya msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho.
Akiwa kaimu kocha mkuu akichukua mikoba
ya Muingereza Dylan Kerr, Mayanja aliiongoza Simba katika mechi 16 za
ligi kuu na kushinda 11, sare moja huku akifungwa michezo minne dhidi ya
Yanga, Toto African, Mwadui FC na JKT Ruvu.
Hakuna kiongozi wa Simba ambaye alikuwa
tayari kulitolea ufafanuzi suala hilo na hata ofisa habari wa timu hiyo,
Hajji Manara alipotafutwa alisema: “Nipo likizo hivyo sijui
kinachoendelea klabuni.”