humph the GREAT
KUNA uwezekano mkubwa beki mpya
wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ akachezeshwa kesho Jumapili dhidi ya MO
Bejaia ya Algeria, mwenyewe amesema akipata nafasi hiyo hatatoka kikosi
cha kwanza.
Yanga kesho Jumapili inatarajiwa kucheza
na MO Bejaia mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye
Uwanja wa l’Unite Maghrebine uliopo Bejaia, Algeria.
Dante aliyesajiliwa na Yanga siku chache
zilizopita kutoka Mtibwa Sugar, ana nafasi kubwa ya kucheza katika beki
ya kati na Kelvin Yondani kwani Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hayupo kikosini.
Cannavaro anatumikia adhabu ya kadi
nyekundu aliyoipata dhidi ya Sagrada Esperanca na Vincent Bossou ambaye
hucheza nafasi hiyo, naye hakufanya mazoezi kikamilifu na wenzake
kutokana na kuchelewa kujiunga nao.
Akizungumza na Championi Jumamosi
kutoka Algeria, Dante alisema: “Kwa jinsi nilivyo fiti kutokana na
mazoezi niliyofanya kambini Uturuki, naamini nikipata nafasi kikosi cha
kwanza sitatoka.”
“Nitacheza kwa juhudi kubwa kumvutia
kocha ili awe ananipa nafasi kila mara kikosini, labda nisipangwe lakini
nikicheza tu nitahakikisha sikai benchi .”
Dante anayemudu kucheza nafasi zote za
ulinzi na kiungo mkabaji, alisema kambi ya muda iliyoweka Yanga nchini
Uturuki tangu Jumapili iliyopita hadi jana Ijumaa, imewasaidia kwa kiasi
kikubwa.
Mbali ya Dante, hadi sasa Yanga
imewasajili Hassan Kessy kutoka Simba, Juma Mahadhi (Coastal Union) na
Beno Kakolanya kutoka Prisons.
Tags
Michezo na burudani