humph the GREAT
Serikali kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) itaisaidia serikali ya
jimbo la Puntland la Somalia kuboresha sekta yake ya utumishi wa umma
kwa kuendesha mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa umma wa jimbo hilo.
Puntland ni Jimbo la Kusini mwa Somalia ambalo limejitangazia mamlaka
yake ya ndani, ingawa halitaki kujitenga moja kwa moja na Somalia yenye
machafuko.
Mkataba wa makubaliano hayo ulisainiwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora),
Angela Kairuki na Waziri wa Kazi, Vijana na Michezo wa Puntland,
Abdurahman Ahmed Abdulle.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo TPSC itashirikiana na Chuo Kikuu Cha
Puntland kuendesha kozi mbalimbali kwa watumishi wa umma wa Puntland
hususani za muda mfupi na watumishi wengi wa umma wa jimbo hilo
watanufaika na programu kadhaa za mafunzo.
Mpango huo wa Puntland umefadhiliwa na Benki ya Dunia ambao pia
umeuwezesha ujumbe wa Puntland kuzuru Tanzania mara kadhaa kwa lengo la
kufanikisha makubaliano hayo.
Waziri Kairuki alisema makubaliano hayo yanalenga kuboresha uhusiano wa
watu wa Tanzania na Puntland na yatasaidia kuimarisha utendaji kazi wa
watumishi wa Umma wa Jimbo la Puntland.
Kwa mujibu wa Kairuki, Tanzania kupitia chuo cha Utumishi wa Umma
kimekuwa kikishirikiana na taasisi za ndani na nje kuboresha sekta ya
umma.
Kwa upande wake Waziri Abdulle alisema jimbo lake limechagua kuja
kujifunza Tanzania kutokana na umadhubuti wake katika sekta ya utumishi
wa Umma.
Alisema anaamini mkataba huo utanufaika jimbo lake.