humph the GREAT
MUDA mfupi tangu Jackson Mayanja, raia wa Uganda aliyekuwa Kocha
Msaidizi wa Simba kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na kile
kilichoelezwa matatizo ya kifamilia, hatimaye mrithi wa nafasi hiyo
ametangazwa.
Mrithi huyo ni aliyekuwa Kocha wa Rayon Sport, Irambona Masoud
Djuma, kocha ambaye anaweza kufananishwa na Kocha wa Manchester United,
Jose Mourinho kutokana na kuwa na mbwembwe nyingi na maneno mengi.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya klabu
hiyo ya Simba, Djuma aliweka hadharani kuwa amekuja ndani ya kikosi
hicho kwa ajili ya kufanya kazi na kukisaidia kufanya vizuri kwenye kila
kombe wanaloshiriki.
“Nimekuja hapa Simba kwa ajili ya kufanya kazi tu, na nataka
tushirikiane ili timu iweze kusonga mbele itoke hapa ilipo, na pia nipo
hapa ili kukuza jina langu maana kiukweli unapozungumzia Simba
unazungumzia juu ya klabu kubwa hapa nchini.
“Lakini pia nafahamu juu ya upinzani uliopo kati ya Simba na Yanga na
siwezi kutabiri kwamba eti kwenye mechi yao Oktoba 28, nini kitatokea
kwa sababu mimi siyo Mungu ila nataka watu wafahamu kwamba kwenye mechi
kuna kufunga, kufungwa na sare, hivyo matokeo yoyote wakubaliane nayo.
“Unajua kwamba hizi mechi za watani duniani kote presha yake inakuwa
ileile siyo Simba na Yanga pekee, hata nilipotoka mimi huko Rwanda
kulikuwa na ushindani wa namna hiyo na hata Ulaya kwenyewe inapofika
mechi hii basi presha huwa kubwa sana.
“Na watu wanajiuliza kwamba kwa nini nimekubali kuwa msaidizi hapa,
niwaambie kwamba Simba ni sehemu kubwa na naamini uwepo wangu hapa
utasaidia kwenye suala zima la kukuza jina langu.
“Niwaambie mashabiki kwamba nipo hapa na ninahitaji tu sapoti yao
kwa ajili ya kuifanya Simba isogee zaidi ya ilipo hapa kwa sasa, na mimi
nitashirikiana nao kulifanikisha suala hilo,” alisema Djuma ambaye
amewahi kufundisha soka kwenye Klabu ya Inter Club na Inter FC.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Makao
Makuu ya Simba, Msimbazi jijini Dar, kocha huyo alionekana kuchangamka
huku akitoa maneno mengi ya utani na hata majibu yake yalikuwa
yamechangamka kitendo kilichofanya waandishi wawe wanacheka mara kadhaa.
Kocha huyo hadi anaondoka ndani ya klabu yake ya Rayon Sport, tayari
alikuwa ameshaisaidia kutwaa ubingwa wa ligi sambamba na Kombe la FA la
kwao, ambapo kocha huyo pia ni mtu wa misimamo na asiyependa
kuyumbishwa.
Kocha huyo anatarajiwa kusaini mkataba leo Ijumaa.
Lakini pia uongozi wa Simba chini ya kaimu rais wake, Salim Abdallah
‘Try Again’, umemteua Richard Robert kuwa meneja wa kikosi hicho
akichukua mikoba ya Cosmas Kapinga ambaye aliamua kubwaga manyanga hivi
karibuni.
Jana jioni kocha huyo aliungana na wenzake mazoezini ambapo pia
alitambulishwa kwa wachezaji na benchi la ufundi, akapata muda kidogo wa
kuzungumza na Omog na kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima.
Moja ya sifa za kocha huyo ni kuwa alikuwa mshambuliaji, hivyo
anaweza kuwa na nafasi nzuri ya kuwapa mbinu washambuliaji Emmanuel
Okwi, John Bocco, Shiza Kichuya, Laudit Mavugo na wengineo.
Mbali na hapo kuna taarifa kuwa kocha huyo atasaini mkataba wa kuwa
msaidizi wakati ambapo anasubiri mkataba wa Omog umalizike baadaye mwaka
huu ili apewe nafasi ya kuwa kocha mkuu.
Waandishi: Ibrahim Mussa, Musa Mateja na Said Ally.
0 Comments