A Saint and a Ghost (Mtakatifu na Mzimu) - 4

MWANAMKE mrembo kupindukia, anaishi katika dunia mbili tofauti na kumfanya awe anabadilikabadilika kila mara. Kwa saa kumi na mbili anaishi kitakatifu jina lake likiwa ni Sista Karen na kwa saa nyingine kumi na mbili, jina lake ni Milembe na anaishi maisha ya ukatili, akiwa muuaji asiye na huruma.

Amekamatwa na polisi akituhumiwa kwa mauaji aliyoyafanya kwenye makaburi ya Wajerumani na kuondoka na fuvu. Chumba chake kinapokaguliwa anakutwa na fuvu hilo, anapelekwa kituo cha polisi.
Upelelezi wa kina unaendelea na anapelekwa kwenye Gereza la Segerea wakati taratibu za kumburuza mahakamani zikianza kufanywa.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Ndani ya Gereza la Segerea, saa tatu na nusu za usiku, zikiwa zimepita saa kumi na mbili tangu Sista Karen aliporejewa na kumbukumbu na kujikuta ufukweni, mikononi mwake akiwa na fuvu la binadamu huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu, akiwa haelewi fuvu hilo lilikuwa la nani na damu zilitoka wapi, kumbukumbu zake zikapotea tena, akili ikabadilika, akaondoka katika  ulimwengu wa ubinadamu na kuingia katika ulimwengu mwingine ambako hakika alikuwa ni mnyama.
“Hapa nipo wapi? Sio nyumbani kwangu hapa? Fuvu langu liko wapi? Nimelipoteza? Hapana! Liko nyumbani, hapa nimekujaje? Hawa waliolala kando yangu ni akina nani? Au ndiyo walionileta humu?” alijiuliza maswali mengi bila majibu huku akiwaangalia wanawake wengine waliolala kando yake wakikoroma.
“Milembe, wamekunyang’anya fuvu lako, hawataki uwe na akili nyingi, wanataka uendelee kuwa mjinga! Waue, watoe damu, wala usisisite, nitakulinda!” aliisikia sauti hiyo masikioni mwake, sauti nzito yenye kutisha, akaangalia huku na kule na kumwona binti mmoja amelala kando yake, taratibu akamrukia na kumkamata shingoni kwa nguvu nyingi ambazo hakuwahi kuamini kama alikuwa nazo. Binti huyo alijaribu kujitingisha lakini haikuwezekana, wala hakuna aliyesikia, wengine waliendelea kukoroma mpaka binti huyo akatulia kabisa bila kutoa sauti.
“Kazi nzuri, nimefurahi, nimekunywa damu, haaa! Haaa!” sauti ilisikika tena akilini mwake ikifuatiwa na kicheko, ilikuwa ni sauti ileile ambayo kwa miaka mingi alikuwa ameisikia.
Mawazo yake yakarejea tena kwenye fuvu, hakuelewa mahali lilipokuwa, lilikuwa ni la muhimu mno kwake ili aweze kulisaga na kunywa unga wake, akiamini lilikuwa ni fuvu la mwanamke Mjerumani mwenye akili nyingi kuliko mwingine yeyote, hivyo kunywa unga wa fuvu la kichwa chake kungefanya akili yake ibadilike, awe na akili nyingi badala ya alivyoambiwa na watu siku zote, kwamba alikuwa mjinga na hakuwa na maana, katika maisha yake angeishia tu kuwa kahaba kama mama yake.
Usiku mzima aliendelea kufikiria fuvu lake na kujiuliza pale alipokuwa ni wapi na alifikaje lakini hakupata majibu, hivyo ndivyo ilivyokuwa mpaka ilipogonga saa tatu kamili za asubuhi, fahamu zikamrejea na kukumbuka mahojiano yake na Inspekta Mary Nchimbi na baadaye alivyochukuliwa na kupelekwa Gereza la Segerea kuwekwa mahabusu, akituhumiwa kufanya mauaji kisha kufukua kaburi na kuiba mabaki ya mwanadamu.
“Sijaua mimi! Mnanionea, mimi ni mtawa, nani kati yenu asiyejua?” alianza kupiga kelele kiasi cha kuwafanya wanawake wenzake aliokuwa nao mahabusu wamshangae.
“Wee! Punguza kelele zako, mtawa gani muuaji?”
“Afande!” ilikuwa ni sauti ya mahabusu mwingine.
“Vipi?”
“Rose hajaamka.”
“Kuna nini?”
“Nahisi siyo mzima.”
“Nini?” askari aliuliza kwa mshangao.
Akawaita wenzake wawili ambao walimsogelea na kumsikiliza mahabusu huyo akieleza, uamuzi ukafikiwa kwamba mahabusu ifunguliwe ili wakague, hilo likafanyika na wote wakazama ndani na kumkuta msichana mdogo mwenye umri wa kama miaka kumi na tisa akiwa amelala sakafuni, mwili wake umekwishakauka!
“Mungu wangu!” Sista Karen aliyekuwa ameketi kando kabisa na msichana huyo alishangaa, hakuwa na taarifa kama alikuwa amekufa, yeye alidhani labda amelala! Machozi yakaanza kumtoka, uchungu mwingi ukamwingia.
“Alikuwa anaumwa?” mmoja wa askari magereza aliuliza.
“Hapana, jana tumepiga naye stori kama kawaida mpaka saa mbili ndipo akalala.”
“Masikini, msichana mdogo kabisa!” Sista Karen alisema akimwangalia msichana huyo akinyanyuliwa kupelekwa nje.
“Shingo yake imevimba sana, lazima kuna mtu kati yenu amemnyonga mpaka akafa!”
“Mimi nilikuwa naye hapa karibu lakini sikuona jambo hilo, labda alikuwa anaumwa tu!” Sista Karen alijibu.
“Alama za vidole zitathibitisha!”
“Hilo ndilo jibu pekee, maana ninyi kwa kusingizia watu kesi! Mimi mwenyewe hapa mnataka kunipa kesi ya mauaji ya mlinzi na kufukua kaburi, jambo ambalo silijui hata kidogo!” aliongeza Sista Karen wakati lango la mahabusu likifungwa.
Ilikuwa ni siku ya Sikukuu ya Krismasi lakini kwa Sista Karen, wala haikuwa hivyo, hakika ilikuwa ni siku ya huzuni kuliko nyingine zote ambazo amewahi kukutana nazo. Vilio vya mahabusu wenzake wakimlilia Rose ndiyo vilizidi kumchanganya kabisa na kujikuta akikata tamaa, hakuelewa ni kwa nini polisi walitaka kumuunganisha kwenye kesi ya mauaji ambayo hakuielewa, hakuwa na kumbukumbu hata kidogo kama aliwahi kuua wala kufukua kaburi la mtu.
Mchana wa siku hiyo aliitwa na kutolewa mahabusu akapelekwa kwenye chumba maalum ambako alikutana na mwanamke mmoja maji ya kunde,  mfupi, ambaye kwa kumwangalia alikuwa ni mchanganyiko wa Mzungu na  Mwafrika,  akajitambulisha kwake kama mwanasheria wa serikali aliyeteuliwa kumsimamia katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili.
“Nashukuru sana, kwa kweli wanataka kunionea, sijafanya hilo tendo hata kidogo, naomba unitetee dada yangu,  nahisi kuna mtu nilishamfanyia ubaya anataka kuniondoa duniani.”
“Tutaujua ukweli, huwezi kuonewa, nitakutetea kwa nguvu zote.”
“Ahsante.”
“Napenda nichukue maelezo yako na ninakusihi usinifiche chochote, hata kama uliua kweli niambie tu ili nitafute jinsi ya kukusaidia, watu wengi huwa wanashindwa kesi zao kwa sababu wanashindwa kuwaeleza ukweli wanasheria wao, ningependa kufahamu ukweli, uko tayari?”
“Niko tayari ndiyo maana nimesema unitetee ili ninusurike na kifo, maisha yangu yako mikononi mwako.”
“Jina lako ni nani?”
“Sista Karen Francis Otikin!”
“Hebu nieleze ukweli kuhusu maisha yako.”
Sista Karen hakujibu kwa haraka, alinyanyua macho yake kuangalia juu kama mtu aliyekuwa akijaribu kupanga majibu, dakika mbili zikapita bila kusema chochote, mwanasheria akamwomba kwa mara nyingine amweleze kuhusu maisha yake.
“Duh! Sijui nianzie wapi?”
“Anzia popote.”
“Ina umuhimu?”
“Sana.”
“Sidhani kama maisha yangu ya nyuma ni ya muhimu sana kukueleza, kikubwa ni kwamba sijaua, hawa watu wamekuja kunikamata nyumbani kwangu wakati najiandaa kwenda kwenye darasa kufundisha wanafunzi wangu masomo ya ziada, kama unataka kunijua mimi majina yangu ni kama nilivyokutajia na ni mwalimu pale Shule ya Sekondari ya St. Magdalena.”
“Haitoshi,  hiyo haitoshi, kama kweli unataka nikutetee, ni vyema unieleze historia yako yote,  kesi hii ni ngumu sana siyo kama unavyofikiria, nimeziona kamera za kwenye makaburi ya  Wajerumani, zimeonesha wazi kabisa jinsi ulivyoingia pale, kuua na kufukua kaburi.
“Zaidi ya yote ulisahau kisu pale, hicho kisu ndicho kimekumaliza kabisa maana kina alama za vidole vya mikono yako, isitoshe kuna mtu tena amekufa mahabusu usiku, naye wamempima alama za vidole shingoni zimeonekana ni za kwako, kwa hiyo una kesi ya mauaji ya watu wawili, hiyo siyo kesi ndogo Sista Karen,  ni kazi ngumu sana, ili tushinde ni lazima unieleze ukweli!”
“Nimemuua nani tena?”
“Mahabusu mwenzako usiku.”
“Mimi? Mimi? Mimi? Kweli mmeamua kuninyonga.”
“Sista naomba unieleze ukweli.”
“Niahidi kitu kimoja, dada nani kweli?”
“Agripina Rwechungura, wakili wa serikali niliyepanga kukutetea kwenye kesi hii. Sema unataka nikuahidi kitu gani?”
“Kwamba majadiliano yatakayofanyika hapa kati yangu na wewe ni kati yangu na wewe tu, maana ni siri, tusije tukafukua na mambo mengine yaliyojificha, wewe shughulikia hilihili ambalo nasingiziwa mauaji.”
“Hakuna shida.”
“Usiniuze.”
“Siwezi kufanya hivyo, mazungumzo yangu na mteja wangu ni yetu wawili.”
Sista Karen akainamisha kichwa chake na kuanza kulia kwa uchungu, kwikwi ilikuwa imemshika kabisa, alionekana ni mtu mwenye uchungu mwingi moyoni mwake  sababu ya historia yake ya nyuma ambayo alitakiwa kuisimulia.
“Jikaze, jikaze sista, unieleze.”
“Sawa.”
Je, nini kitafuata? Sista Karen atasimulia nini mbele ya mwanasheria wake?
Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post