A Saint and a Ghost (Mtakatifu na Mzimu) - 3

KWA mwonekano, ni mwanamke mrembo kupindukia aliyejaaliwa shani na uzuri wa kipekee. Upande wake wa kwanza wa maisha anafanya matendo mema yanayoweza kukufanya ukamfananisha na mtakatifu. Ni Sista Karen, mtawa anayefanya kazi ya ualimu katika chuo cha watawa.

Upande wa pili wa maisha yake, ana sifa za tofauti ambazo ni kinyume kabisa na zile za awali. Wema na utakatifu wake hudumu kwa saa kumi na mbili lakini baada ya hapo, hubadilika na kuwa muuaji asiye na huruma, akifahamika kwa jina la Milembe.
Mwanamke huyu mwenye maisha ya ajabu, anayebadilika kutoka utakatifu hadi mzimu, amekamatwa na polisi akijiandaa kwenda darasani kufundisha wanafunzi wake somo la Biashara. Ingawa ni siku ya Sikukuu ya Krismasi, wanafunzi wake walimpenda kwa moyo wa kujitolea bila kujua upande wake wa pili alikuwa ni mtu wa namna gani.
Anafungua mlango na kukutana na midomo mitano ya bunduki ikiwa imemwelekea, mwili wake unatetemeka, anaamriwa kwamba yupo chini ya ulinzi, akiitwa muuaji mkubwa aliyejificha kwenye vazi la Kitawa. Anajaribu kujitetea lakini hakuna anayemuelewa, chumba chake kinapopekuliwa, anakutwa na fuvu la binadamu. Anachukuliwa msobemsobe mpaka kituo cha kati cha polisi.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Wataalamu wa kitengo muhimu cha Jeshi la Polisi cha Forensic and Biometric Department (FBD) walikuwa wakihangaika kuhakikisha wanapata vithibitisho vyote muhimu ambavyo vingetumika kumpandishia kizimbani Sista Karen, aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma nzito.
Uzito wa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili, ulimlazimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Bwana Nzungu Baliza kuwasimamia vijana wake kwa umakini wa hali ya juu, huku akisisitiza kuwa lazima wahakikishe hakuna kosa hata moja linaloweza kutokea na kusababisha mtuhumiwa kuonewa au kupendelewa.
Uthibitisho wa kamera za ulinzi, CCTV zilizokuwa kwenye makaburi ya Wajerumani, ulitosha kumuweka hatiani Karen kwani picha za video zilimuonesha akifanya mauaji kisha kufukua kwenye kaburi la Wajerumani na kuondoka na fuvu lakini kwa kuwa kamera hizo zilikuwa zikichukua picha kutoka mbali, ilibidi uthibitisho mwingine utafutwe.
Kwa kuwa kisu alichokitumia kufanyia mauaji alikiacha eneo hilohilo la makaburi, kiliokotwa na wanausalama kisha kikaenda kuchunguzwa alama za vidole. Baada ya kukamilika kwa zoezi la kuchukua picha za alama za vidole (fingerprints) kwenye kisu kilichotumika kufanyia mauaji, picha hizo zilihifadhiwa kusubiri kufananishwa na mikono ya Sista Karen.
Baada ya takribani dakika arobaini na tano, tayari majibu yalikuwa yametoka. Picha za alama za vidole zilizokutwa kwenye kisu kilichotumika kufanyia mauaji, zilikuwa zikifanana kwa kila kitu na alama za vidole zilizochukuliwa kutoka kwa Sista Karen.
***
“Kwa nini unasema uongo Sista Karen?”
“Sisemi uongo afande, ninachoeleza ni kweli kabisa.”
“Unamuamini Mungu?”
“Ndiyo, tena kwa moyo wangu wote.”
“Unaamini kwamba kusema uongo ni dhambi?”
“Natambua afande lakini hata kukubali kuwa nimefanya kosa ambalo sikulifanya huo pia ni uongo,” alisema Karen huku akijiamini kupita kiasi. Katika kumbukumbu zake, hakuna hata sehemu moja iliyomuonesha kuwa ni kweli yeye ndiyo alikuwa mhusika kwa mashtaka mazito yaliyokuwa yanamkabili.
Inspekta wa Polisi, Mary Nchimbi, mwanamke mpole, makini na Mchamungu aliyekuwa akisifika kwa kufanya kazi katika misingi ya haki, alikuwa akiendelea kumhoji Karen lakini hakupewa ushirikiano alioutegemea. Licha ya kujaribu kutumia mbinu zake zote za kiintelijensia kumhoji Karen, bado majibu aliyokuwa anayatoa yalikuwa yanaonesha kwamba hafahamu chochote kuhusu fuvu alilokutwa nalo.
“Hebu nisubiri, nakuja sasa hivi,” alisema Inspekta Nchimbi na kutoka nje ya chumba cha mahojiano, muda mfupi baadaye alirejea tena akiwa amevaa gloves, mkononi akiwa na kisu kilichookotwa makaburini.
“Sista Karen, unakifahamu hiki kisu?” alisema Inspekta Nchimbi huku akimuoneshea Sista Karen. Alikodoa macho kukitazama kisu hicho ambacho kilikuwa na alama za damu ambayo sasa ilishakauka, akatingisha kisu kuonesha kwamba hakifahamu.
“Hujawahi kukishika au kukitumia mahali popote?”
“Mimi? Wala sijawahi.”
“Sasa kwa nini alama zako za vidole zimeonekana kwenye hiki kisu?”
“Alama za vidole? Afande mbona mi sielewi chochote?”
“Sikia Sista Karen, huo ujanjaujanja unaotaka kuuonesha hauwezi kukusaidia chochote. Kwa nini hutaki kusema ukweli ili tujue wapi pa kuanzia kukusaidia?”
“Afande huo ninaosema ndiyo ukweli wangu, siwezi kukubali kitu nisichokijua, hata Mungu wangu ni shahidi na katika hili atanilinda,” alisema Sista Karen huku akionesha alama fulani kwa kujigusa kwenye paji la uso, kifuani kisha kwenye ubavu wake wa kushoto na kumalizia ubavu wa kulia.
Japokuwa Inspekta Nchimbi hakuwa mtu wa jazba, majibu aliyokuwa anapewa na Sista Karen yalimkasirisha na kujikuta amepandwa na jazba, akainuka kwa kasi na kutoka, akaubamiza mlango wa chumba alichokuwa amefungiwa mtawa huyo kisha akawa anatembea kwa hatua ndefundefu.
Askari waliokuwa nje ya chumba cha mahojiano, walipoona inspekta ametoka, waliingia haraka na kumfunga pingu Sista Karen, wakamtoa na kuanza kumkokota kuelekea mahabusu. Mtawa huyo hakuwa na hata chembe ya wasiwasi, aliendelea kusali na kuamini kuwa ataachiwa huru baada ya muda mfupi.
Inspekta Nchimbi alipotoka kwenye chumba cha mahojiano, alikwenda moja kwa moja mpaka kwenye Forensic and Biometric Department (FBD) alikorudisha kisu kilichookotwa makaburini, eneo la tukio. Pia alitaka aoneshwe mwenyewe ushahidi wa picha za alama za vidole na zile za CCTV ambazo tayari zilishaingizwa kwenye ‘database’ ya Jeshi la Polisi.
Alipochunguza kwa makini, Inspekta Nchimbi alijiridhisha kwamba mtu aliyekuwa akionekana kwenye kamera za CCTV alikuwa ni Sista Karen na hata alama za vidole zilizokutwa kwenye kisu, zilikuwa zikifanana kwa kila kitu na zile za vidole vya Karen.
“Huyu mtawa mbona anataka kuleta usumbufu usio wa lazima? Kila kitu kipo wazi lakini anajifanya haelewi chochote! Jeuri yake itaishia mahakamani,” alisema Inspekta Nchimbi, akatoka kwenye idara hiyo na kwenda mpaka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Ebenezer Mlyuka.
Mipango ya kumfungulia mashtaka Sista Karen ikaanza kufanywa ambapo DPP Mlyuka baada ya kupokea vielelezo vyote vya mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Sista Karen, alimfungulia mashtaka kisha jalada likarudishwa tena kwenye ofisi ya waendesha mashtaka wa serikali.
Kila kitu kilifanyika haraka kwani shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali lilikuwa kubwa, wengine wakiamini mtawa huyo alikuwa anaonewa huku wengine, hasa Wajerumani wakishinikiza mshtakiwa huyo apelekwe mahakamani.
Wakati pilikapilika hizo zikiendelea, umati wa watu ulikuwa ukizidi kuongezeka nje ya Kituo cha Kati cha Polisi ambacho mtawa huyo alikuwa akishikiliwa. Kila aliyesikia juu ya habari hizo, hakutaka kuishia kusimuliwa, kila mtu alitaka akajionee mwenyewe maajabu hayo.
Kwa sababu za kiusalama, Mkuu wa Jeshi la Polisi alitoa maagizo kuwa mtuhumiwa huyo atolewe mahabusu chini ya uangalizi mkali na kupelekwa kwenye Gereza la Segerea ambako angekaa kwa siku zote wakati mchakato wa kuanza kumpandisha kizimbani ukifanywa.
Askari wengi wakamwagwa nje ya kituo hicho cha polisi huku kikosi maalum cha askari waliokuwa na silaha nzito wakimtoa mtuhumiwa kutoka mahabusu na kumuingiza kwenye karandinga, safari ya kuelekea Gereza la Segerea chini ya ulinzi mkali ikaanza.
***
Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka.
Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo. Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo  jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi.
Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu. Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Ijumaa kwenye Gazeti la
Ijumaa.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post