HII ni historia ya kweli ya maisha yangu, kuna baadhi ya watu nakutana nao wananiuliza kama hii ni hadithi kama ambazo nimekuwa nikiandika magazetini. Nataka nisisitize kwamba hii ni historia ya kweli kabisa ya maisha yangu, najaribu kuyapitia maisha yangu ya nyuma na kuwaandikia watu kule nilikopitia.
Lengo langu ni nini? Kumtia moyo mtu aliyevunjika moyo na kumfanya aamini inawezekana kufanikiwa hata kama unatoka familia masikini. Nayasema haya kwa sababu wako watu leo hii wamekata tamaa kabisa na kuamini kwamba watu fulani wanaweza kufanya vizuri maishani na si wao, uongo mkubwa na mbinu ya shetani kuwafanya watu waendelee kuteseka.
Yeyote anayesoma historia yangu ni lazima hata kama yuko katika hali ngumu kiasi gani, aamini kwamba inawezekana, kama iliwezekana kwangu inashindikanaje kwa mtu mwingine? Inuka hapo ulipo, amini akili yako, fanya jambo jema hata kama ni dogo kiasi gani, ukilifanya kwa muda mrefu hatimaye jambo kubwa litakutokea, huu kwangu ni ukweli uliothibitishwa na mimi mwenyewe.
Lengo si kujitapa bali kuwaonesha watu jinsi Mungu anavyoweza kumbariki mtu na ninajua kutoka ndani ya moyo wangu ya kwamba Mungu alininyanyua kwa kusudi moja tu; yeyote aliyekata tamaa atakaponiangalia mimi apate tumaini na kuamini kwamba kumbe inawezekana.
Nimeishia kueleza jinsi baadhi ya wafanyakazi wangu walivyoamua kuniacha kwenye mataa.
ENDELEA...
ENDELEA...
AHAA! Kumbeee!” Nilijisemea moyoni mwangu baada ya kuona majina ya vijana wangu waliocha kazi kwenye Gazeti la Kiu ambalo hapo awali tulikuwa tukiliendesha.
Nilipoona hivyo tu nikajua tayari mpambano umewadia, wakati wa kupima uwezo wa akili (IQ) kati ya kundi lililobaki na lililoondoka ulikuwa umefika. Niliwaza hivyo kwa sababu vijana hawa walijua kila kitu kuhusu kazi tuliyokuwa tukiifanya, ni kama mtu alikuwa akifanya kazi ya kutengeneza juisi na vijana fulani, baadaye wakaondoka kundini na kwenda kando kuanza kutengeneza juisi ileile wakiwa wanajua kanuni zote na siri zote za utengenezaji, hakika nilitegemea ushindani mkubwa kutoka kwa waliokuwa vijana wangu.
Nilipoingia ofisini siku hiyo nilikuta kila mtu akiniangalia kwa jicho la “Sijui tutawaweza?” jambo lililonionesha kwamba watu wangu walikuwa wamepoteza matumaini, nilichokifanya ni kutumia muda wa kama dakika ishirini hivi kuzungumza nao juu ya uwezo mkubwa wa akili tuliokuwa nao, nikawahamasisha na kuwafanya wajisikie washindi, kila mmoja akasisimka na kwa pamoja tukasema USHINDI NI LAZIMA.
Katika mazungumzo yangu niliwapa mfano wa wapiganaji waliokuwa wamekwenda kupigana vita kwenye kisiwa kimoja, walipofika tu ufukweni, wote walishuka na kuichoma moto manowari waliyokwenda nayo, kisha kamanda wao akawaeleza: “Twendeni vitani, hakuna kurudi, huko tunakokwenda ni aidha kushinda au kufa.” USHINDI ULIPATIKANA.
Ushindi ulipatikana kwa sababu hawakuwa na namna ya kurudi nyumbani, manowari yao walishaichoma, hivyo ilikuwa ni lazima kama walitaka kuendelea kuwa hai washinde vita na kuichukua kisiwa hicho. Mfano huo uliwatia vijana wangu hamasa, tukaingia katika mapambano ya kibiashara na Gazeti la Kiu, kila mmoja wetu akiwaza ushindi.
Magazeti yetu yalitoka siku moja, siku ya Ijumaa, yalifanana kila kitu isipokuwa majina na kilichoandikwa kwenye gazeti lakini kama ungekuta Gazeti la Kiu limekunjwa kuficha jina lake, ungesema ni Ijumaa na vivyo hivyo kama ungekuta Ijumaa limekunjwa kuficha jina ungesema ni Kiu, wasomaji wengi walichanganyikiwa.
Tulianzia nakala elfu ishirini ingawa wenzetu walichapa nakala zilezile tulizokuwa tumefika na Gazeti la Kiu; elfu hamsini. Tukaingia sokoni, siku tano baadaye wauza magazeti waliporejesha mabaki, yalikuwa lundo! Ilikuwa ni picha ya kukatisha tamaa kabisa, ikabidi nizungumze na ofisi na kuwaeleza kwamba kilichotokea ni kwa sababu watu walikuwa bado hawajajua kwamba gazeti letu lilikuwa linatoka siku hiyo.
“Lakini jamaa wameuza la kwao,” Peter Mihayo alisema.
“Usijali Peter, kache, kache, imbeba ikamalu msomole!” nilisema msemo wa kabila la Wazinza kutoka kisiwani Kome huko Sengerema unaomaanisha “Taratibu, taratibu, panya alimaliza kula ngozi!” Wote wakacheka.
“Usijali Peter, kache, kache, imbeba ikamalu msomole!” nilisema msemo wa kabila la Wazinza kutoka kisiwani Kome huko Sengerema unaomaanisha “Taratibu, taratibu, panya alimaliza kula ngozi!” Wote wakacheka.
Niliyasema maneno hayo kama kiongozi, ingawa ndani ya moyo wangu kuna wasiwasi mkubwa uliokuwa umeniingia ambao sikutaka kabisa kuwaonesha watu ninaowaongoza, maana kufanya hivyo kungemaanisha kuwavunja moyo. Tukaendelea kuchapa kazi kwa nguvu kila wiki, mabaki yakiendelea kupungua na mpambano wa Kiu vs Ijumaa ukizidi kuwa mkali.
Wasomaji tayari walishagundua tulikuwa tukishindana, wakalazimika kuwa wananunua magazeti yote mawili kufuatilia kilichoandikwa na kambi zote mbili. Huwezi kuamini ndani ya muda wa miezi miwili, tulikuwa tukichapa nakala elfu hamsini na tano, Kiu wakichapa elfu hamsini!
Tukaendelea kupanda nao wakitufukuza kwa nyuma, kitu ambacho nilijifunza baadaye ni kwamba Watanzania wanapenda sana mahali kwenye ushindani, basi nakala za magazeti ziliongezeka mpaka laki moja na elfu hamsini, Kiu wakichapa laki moja na thelathini! Kila mmoja wetu alikuwa na furaha sababu sote tulikuwa tukifanya biashara.
Hapo ndipo nikaanza kuelewa namna ambavyo Mungu hufanya kazi zake, ili ukue au uondoke hapo ulipo kwenda kwenye mafanikio makubwa zaidi, lazima jambo fulani liharibike! Lisipoharibika utaendelea kubaki hapohapo siku zote. Kama Amri Salim asingelichukua gazeti lake, Ijumaa lisingezaliwa na kama Ijumaa lisingezaliwa tungeendelea kuchapa Kiu nakala elfu hamsini.
Ushindani uliotokea ulitusaidia sana kutumia akili za ziada na kugundua uwezo mwingine ambao Mungu ametupa, hatimaye tukawezesha magazeti mawili kukua kwa kasi kubwa na kufikia kiwango cha nakala ambacho hakuna gazeti nchini Tanzania liliwahi kuchapa.
Pamoja na mafanikio hayo, bado hatukuwa na uhusiano mzuri sana na jamaa wa Kiu, kifupi walikuwa si washindani tu bali maadui! Kila mmoja alimwogopa mwenzake. Nikasoma kitabu cha mchungaji mmoja wa Kimarekani aitwaye Robert Schuller, ambaye katika kitabu chake kiitwacho Success is Never Ending, Failure is Never Final, alisema: To be successful you need friends, to be more successful you need enemies (Kama unataka kufanikiwa unahitaji marafiki, lakini kama unataka kufanikiwa zaidi, unahitaji maadui).
Maadui ni wa muhimu katika mafanikio, isitoshe hata kama huwataki watakuja tu, hujawakosea kitu, wewe ni mwema kwa kila mtu na unajitahidi kuishi maisha yako bila kukosana na watu, bado utakuwa na maadui! Maadui alikuwa nao Yesu na Mtume Muhamad, wewe binadamu wa kawaida uwakose? Nani kasema?
Utajitahidi sana kuwafurahisha watu, ndugu, jamaa na marafiki lakini bado mwisho wa siku utakuwa adui wa mtu fulani! Hivyo ndivyo maisha yalivyo, tayari Shigongo nikawa nimeshaanza kuwa na maadui maishani mwangu, jambo ambalo sikuwahi kulitarajia kabisa na huwa silipendi.
Maadui hawakuwa Kiu tu, watu wote wenye majina walioandikwa na magazeti yetu na maovu yao kufichuliwa waligeuka maadui, sikuwa na uhakika nani angekuwa adui siku iliyofuata gazeti likitoka. Jina langu likakua ghafla, nikawa midomoni mwa watu, wapo walioniona mwema na kunipenda lakini wapo walioniona mbaya niliyestahili hata kufa na watu wakafanya sherehe kwamba nimekufa.
Siku moja nikiwa ofisini, akaja mama mmoja, kwa jina simfahamu sababu imekuwa siku nyingi mno, akaomba kuongea na mimi na akaruhusiwa kuingia ofisini kwangu.
Huku akilia alinisimulia juu ya ndoa yake, kwamba ilikuwa imeingiliwa na mtangazaji mmoja wa redio aitwaye Amina Chifupa! Mume wa mwanamke huyo aitwaye Kinemene Mangosongo, alikuwa hasikii wala haambiwi kwa mtangazaji huyo.
Moyo ulinilipuka, sababu Amina Chifupa alikuwa rafiki yangu mkubwa!
“Amina? Anatembea na mume wako?” nilimuuliza mama huyo maswali mengi akanipa vielelezo vyote na nikaridhika. Nilichokifanya ni kuwaita wenzangu na kuwaeleza juu ya simulizi ambayo mama huyo alikuwa akinipa, hawakushangaa.
“Amina? Anatembea na mume wako?” nilimuuliza mama huyo maswali mengi akanipa vielelezo vyote na nikaridhika. Nilichokifanya ni kuwaita wenzangu na kuwaeleza juu ya simulizi ambayo mama huyo alikuwa akinipa, hawakushangaa.
Nilimwomba mama huyo arudi nyumbani siku hiyo ili habari yake ifanyiwe kazi, baada ya kuondoka juhudi za kumtafuta Amina Chifupa ili aongelee suala hilo zilianza, vijana wakampigia simu, alichowajibu Amina kilikuwa ni kitu cha kuwadharau na kuwaona hawana maana sababu eti yeye alikuwa anafahamiana na bosi wao.
Waliponieleza sikufurahia kauli ya Amina, hakutakiwa kuwadharau maana hao walikuwa ni kila kitu kwangu, ni heri angewaomba tu wamsaidie badala ya kuwapuuza. Tukajadiliana na wenzangu juu ya kuiandika habari hiyo, kiukweli nilitamani habari hiyo isitoke kwa kumwonea huruma Amina lakini kwa jinsi wenzangu walivyokuwa na msimamo wakinihakikishia kwamba, tusipoiandika sisi, washindani wetu (KIU) wangeiandika ilibidi nilainike, habari ikatoka.
Kutoka kwa habari hiyo kuliongeza idadi ya maadui, Clouds Media Group yote, ingawa sina uhakika sana na Mkurugenzi wao Joseph Kusaga, ikageuka na kuwa adui mkubwa wa Global Publishers na mimi mwenyewe binafsi! Magazeti yetu na wakati mwingine mimi mwenyewe nikawa nachambuliwa ipasavyo kwenye baadhi ya vipindi vyao, kisa? Amina Chifupa ameandikwa.
Amina akageuka kuwa adui mkubwa wa Shigongo, baadaye mama huyo alikwenda shuleni Tambaza ambako Amina alikuwa akisoma na kufanya vurugu, ikabidi afukuzwe shule na kuhamia Makongo Sekondari, jambo ambalo kwa kweli lilinisikitisha sana! Lazima nikiri kuwa wakati habari hiyo inatoka sikutegemea madhara yake yangekuwa makubwa kiasi hicho.
“Bosi, kuna wageni wanataka kukuona!” Mary Raphael aliniambia.
“Akina nani?”
“Akina nani?”
“Mzee Chifupa na bwana mmoja amejitambulisha kama Gotham!”
“Waambie waingie.”
“Waambie waingie.”
Akaingia mzee Chifupa akifuatiwa nyuma na kijana mmoja mtanashati mweupe, ambaye kwa kumwangalia tu umri wake alionekana ni mtu wa Kung Fu, mapigo ya moyo yakaanza kwenda mbio lakini sikutaka kuonesha udhaifu, nikajikakamua na kuwakaribisha vizuri.
“Shikamoo mzee,” nilimwamkia mzee Chifupa lakini hakuitikia, nikajua leo hapa kuna mtiti.
“Salama kaka?” Gotham alinisalimia na baadaye kujitambulisha kuwa yeye na mzee Chifupa walikuwa pale kujadiliana juu ya habari za binti yake zilizokuwa zikiandikwa na magazeti yetu.
“Salama kaka?” Gotham alinisalimia na baadaye kujitambulisha kuwa yeye na mzee Chifupa walikuwa pale kujadiliana juu ya habari za binti yake zilizokuwa zikiandikwa na magazeti yetu.
“Hivi kwa nini unamwandika mwanangu?” mzee Chifupa aling’aka na kunyanyuka kuanza kuizunguka meza akinifuata.
Gotham ambaye mpaka leo ni rafiki yangu alijaribu kumshika lakini alishachelewa, tayari mzee Chifupa alishanikaba na hapo ndipo nilielewa kwamba mzee huyo aliwahi kuwa mwanajeshi, mikono yake ilikuwa na nguvu na alikuwa akinipeleka ukutani akijiandaa kunirukia kichwa.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia Jumatatu ijayo kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.
Tags
Hadithi & Simulizi