HIVI UNAPOMTESA ‘HAUSIGELI’ WAKO UNATARAJIA NINI?


NDUGU zangu, leo ngoja niwazungumzie watu ambao kwa uelewa wangu ni muhimu sana kwenye jamii yetu. Nawazungumzia wasaidizi wa kike wa kazi za ndani ambao tumezoea kuwaita mahausigeli huku wengine wakiwapachika jina la mabeki tatu.
Hawa ni watu muhimu sana. Msaada unaotolewa na wasichana hawa hasa kwa watu wenye familia ni mkubwa lakini kinachoniuma ni kwamba baadhi yao wamekuwa wakinyanyasika sana.
Juzi nilisoma habari moja iliyokuwa inamhusu hausigeli mmoja ambaye ana mwaka sasa hawajawahi kulipwa mshahara wake lakini pia amekuwa akipigwa, kunyimwa chakula au kupewa makombo.
Aliniambia: “Kaka yangu, nafanya kazi kwenye mazingira magumu sana, huu ni mwaka sasa sijapewa mshahara wangu licha ya kujituma kufanya kazi. Nateswa bila sababu, nafanyishwa kazi kiasi kwamba sipati muda hata wa kupumzika.
“Sijui kwa nini yule mama ananifanyia hivi, hapa nilipo natamani kurudi kwetu licha ya kwamba najua huko nitakutana na maisha magumu sana kwani wazazi wangu wamefariki.
“Lakini sina jinsi, nimekuja kufanya kazi huku mjini ili niwasaidie wadogo zangu ambao wanaishi na bibi yangu kijijini lakini matokeo yake nateswa.”
Binti huyo aliniambia maneno hayo huku akibubujikwa na machozi. Ni binti mzuri ambaye amekosa tu malezi bora. Anaonekana ni mwenye busara lakini katika maelezo yake nikagundua pia kwamba, bosi wake wa kiume amekuwa akimtaka kimapenzi ndipo mkewe akagundua na kuhisi huenda alishawahi kumkubalia.
Hapo ndipo baadhi ya wanawake wenye mahausigeli wanapokosea. Hivi inakuwaje ufikie hatua ya kumtesa hausigeli wako ambaye huwa unamuacha na watoto wako, anakusaidia kuwalea na kufanya kazi mbalimbali?
Kwa nini ufikie hatua ya kumtesa eti kwa kuhisi anatembea na mume wako? Huo ni ulimbukeni jamani. Iweje umtese binti wa mwenzako kwa hisia tu?
Na kama anakosea, unadhani njia sahihi ya kumuadhibu ni kumfanyia vitendo vya kinyama? Kwa nini usizungumze naye na kujaribu kumrekebisha au kumrudisha kwao kama unaona harekebishiki?
Kiukweli matukio ya mahausigeli kuteswa na mabosi wao hasa wale wa kike yananiuma sana. Ndiyo maana tunasikia na kuona baadhi ya mahausigeli wakichukua maamuzi ambayo si mazuri kutokana na mateso wanayopata.
Hujawahi kusikia hausigeli kamchoma moto mtoto wa bosi wake? Hujawahi kusikia mtoto kafungiwa kwenye friji na hausigeli hadi kufa? Hujasikia matukio ya hausigeli kujiua au kuwawekea sumu mabosi wake?
Unadhani kwa nini wanafanya hivyo? Hivi ungekuwa unamchukulia hausigeli kama mdogo wako ambaye amekuja kukusaidia kazi za ndani kisha ukawa unamuonesha upendo angeweza kufanya vitendo vya kinyama kama hivyo?
Tufahamu kwamba, baadhi ya mabosi wanawalazimisha mahasugeli kuwaibia na kuwakimbia, kuwanyanyasa watoto wao na wengine kujiua. Hii inatokana na yale wanayofanyiwa na mabosi wao ambapo mwishowe wanaona bora kulipiza kisasi.
Unapoamua kumchukua msichana wa kazi, kwanza jitahidi sana kumuonesha upendo. Ni lazima ufanye hivyo kwa kuwa, anakusaidia sana kwenye maisha yako. Anakufanya uwe na amani unapokuwa mbali na watoto wako ukijua atawalea vizuri na kukupunguzia kazi ambazo ungezifanya wewe. Mtu huyu ni wa kumpenda sana.
La pili, jitahidi kumpa haki zake kwa wakati. Kama mmekubaliana umtunzie mshahara wake atauhitaji mpatie bila ya kumzungusha. Kumbuka kila anayefanya kazi ana malengo. Wengine wanafanya kazi ili kuwasaidia wazazi na wadogo zao, sasa kama utakuwa mgumu katika kumlipa utamvunja moyo wa kufanya kazi.
Lingine la msingi sana ni kila mwenye hausigeli kujitahidi kumchukulia kama mwanaye. Mpatie haki zote za msingi kama unavyowapa wanao.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post