humphrey the GREAT
Tuzo za Muziki za Kili 2015, Jumamosi ya wiki iliyopita zilitimua vumbi kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo maelfu ya Watanzania wanaopenda burudani walikuwa wakifuatilia mwenendo mzima wa tuzo hizo, ambapo msanii Ali Kiba aling’ara baada ya kunyakua tuzo tano na kumuacha mbali hasimu wake mkubwa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ aliyeambulia tuzo mbili tu.
Tuzo za Muziki za Kili 2015, Jumamosi ya wiki iliyopita zilitimua vumbi kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo maelfu ya Watanzania wanaopenda burudani walikuwa wakifuatilia mwenendo mzima wa tuzo hizo, ambapo msanii Ali Kiba aling’ara baada ya kunyakua tuzo tano na kumuacha mbali hasimu wake mkubwa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ aliyeambulia tuzo mbili tu.
Mpango mzima ulianza, mishale ya saa
tatu za usiku ambapo wasanii pamoja na wadau mbalimbali walijumuika
kwenye zulia jekundu na kupiga ‘mapichapicha’ ya ukumbusho kabla ya
mchakato wa kutoa tuzo haujaanza.
Baada ya hapo, pazia la burudani
lilifunguliwa na msanii chipukizi, Ruby anayetamba na ngoma yake ya Na
Yule, akafuatiwa na Ommy Dimpoz, baadaye akapanda jukwaani Barnaba Elias
sambamba na Vanessa Mdee, akapanda Christian Bella kisha Weusi
wakiongozwa na Joh Makini na Nikki II wakafunga pazia la burudani kwa
kukamua ile mbaya.
ALI KIBA ANG’ARA
Baadaye ulifuatia mchakato wa kutoa tuzo
ambapo msanii Ali Kiba, alizoa tuzo tano; Mtumbuizaji Bora wa Mwaka,
Wimbo Bora wa Mwaka (Mwana), Mtunzi Bora wa Mwaka (Bongo Fleva), Wimbo
Bora wa Afro (Mwana) na Mwimbaji Bora wa Kiume (Bongo Fleva) huku hasimu
wake Diamond Platinumz akiambulia tuzo mbili tu; Wimbo Bora wa Zouk/
Rhumba (Nitampata Wapi) na Video Bora ya Muziki ya Mwaka (MdogoMdogo).
KILICHOMPONZA DIAMOND NI HIKI
Kutokana na matokeo hayo, inaelezwa kuwa
kilichomponza msanii Diamond Platinumz ni ujumbe wake aliowahi kuutuma
kwenye mitandao ya kijamii, akiziponda Tuzo za Kili kwamba hazizingatii
vigezo, kwa kuwaacha wasanii wanaofanya vyema kwenye tasnia ya muziki na
badala yake, ‘kuwapendelea’ baadhi ya wasanii kutokana na sababu
binafsi za waandaaji.
“Unajua Diamond alikosea sana kuziponda
Tuzo za Kili kwa sababu ndizo zilizompaisha mwaka jana, matokeo yake
amempa nafasi mpinzani wake, Ali Kiba kung’ara kwa kunyakua tuzo kibao,
nafikiri atakuwa amejifunza jambo,” alisema Bruno Sanga, mmoja kati ya
wadau waliohudhuria utoaji wa tuzo hizo.
WASHINDI WENGINE
Ukiachilia mbali Ali Kiba na Diamond,
wengine walioziteka tuzo hizo ni mwanadada Vanesssa Mdee aliyenyakua
tuzo mbili; Mtumbuizaji Bora wa Mwaka (Kike) na Mwimbaji Bora wa Kike
(Bongo Fleva), Mzee Yusuph; Mwimbaji Bora wa Kiume Taarab, Mtunzi Bora
wa Mwaka (Taarab) na Kundi Bora la Taarab (Jahazi).
Wengine ni Jose Mara aliyenyakua tuzo
mbili, Isha Mashauzi, Joh Makini, Baraka Da Prince (Msanii Bora
Chipukizi), Nahreel (Mtayarishaji Bora wa Mwaka) na Mrisho Mpoto
aliyeondoka na Tuzo ya Wimbo Bora Wenye Vionjo vya Asili (Waite).
Sauti Sol walinyakua Tuzo ya Wimbo Bora
wa Afrika Mashariki (Sura Yako), Profesa Jay (Wimbo Bora wa Hip Hop -
Kipi Sijasikia), Jux (Wimbo Bora wa R&B- Sisikii) na Wimbo Bora wa
Bendi wa Kiswahili iliyokwenda kwa FM Academia (Vijana wa Ngwasuma) na
Bendi Bora ya Mwaka (FM Academia) huku Yamoto Band wakinyakua tuzo ya
Kikundi Bora cha Mwaka (Bongo Fleva).
0 Comments