humphrey the GREAT
NAMSHUKURU Mungu aliyenivusha salama
Julai na sasa nimeanza safari ya kuipunguza Agosti! Jambo la kuvutia
ndiyo mwezi ambao ligi za England, Hispania na nyingine huanza.
Juma hili nimekuwa nikifuatilia Kombe la
Kagame linaloendelea jijini Dar es Salaam, sitazungumzia matokeo ya
timu zote kwa sababu makala hii inawatazama zaidi Azam FC.
Nimebahatika kuzitazama mechi zote za
Azam za Kundi C ikishinda 1-0 dhidi ya KCC ya Uganda, 3-0 dhidi ya
Malakia FC ya Sudan Kusini na mechi ya mwisho ikiichapa 5-0 Adama City
ya Ethiopia.
Pia niliwatazama katika mechi ya robo
fainali ambayo walishinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Yanga baada ya suluhu
ndani ya dakika 90.
Lengo la kuwafuatilia Azam kwa ukaribu,
ingawa sitazungumzia matokeo yao ya nusu fainali iliyopigwa jana dhidi
ya KCC, ni kuona kama mabadiliko makubwa ya mfumo wa uendeshaji wa timu
yameanza kuleta matunda.
Mara nyingi nimekuwa nikiwapigia kelele
Azam hasa wanapoleta mambo ya ‘Kiswahili’, huku wadau wengi wa soka
wakiamini ndiyo klabu pekee inayoweza kulibadili soka la Tanzania.
Mapema Juni, mwaka huu, Azam walitangaza
mfumo mpya wa utawala wa klabu na kuunda vitengo vyenye watu wenye
taaluma husika, ambao tunaamini hawaingiliwi.
Kwa faida yako msomaji, muundo wa uongozi wa Azam FC uko hivi:
Bodi ya wakurugenzi: Hiki ni
kikao cha juu kabisa cha maamuzi ya klabu, wajumbe wake wamebaki kuwa
wanafamilia wa familia ya Bakhresa. Viongozi na baadhi ya watendaji
hualikwa kwenye vikao ili kutoa ripoti za utendaji na sera.
Uongozi: Mwenyekiti wa klabu
amebaki kuwa mzee Said Mohammed, huku aliyekuwa katibu mkuu wa muda
mrefu tangia klabu ianzishwe, Nassor Idrissa ‘Father’ akiwa makamu
mwenyekiti. Nafasi ya katibu mkuu ilifutwa. Nafasi ya Ukurugenzi wa
Sheria na Haki za Wachezaji imeendelea kushikiliwa na mwanasheria Shani
Christoms.
Watendaji: Saad Kawemba
anaendelea kuwa mtendaji mkuu wa klabu, huku Azam ikimuajiri Muingereza
mwenye asili ya Uganda, Eli Eribankya kuwa meneja utawala na fedha.
Eribankya anasaidiwa na mchezaji wa zamani wa Azam, Mtanzania, Lackson
Kakolaki.
Benchi la ufundi: Stewart John
Hall kutoka Uingereza amerejea kwa mara ya tatu kuongoza benchi la
ufundi la Azam. Hall anasaidiwa na Mganda George ‘Best’ Nsimbe, huku
Mark Philips kutoka Uingereza akiwa kocha wa magolikipa. Kocha wa
magolikipa aliyedumu kwa muda mrefu Iddi Abubakar anaendelea kuwepo kama
msaidizi wa Philips.
Mtaalam wa tiba ya viungo na lishe ‘Team
Physiotherapist and Nutritionist’ ni George Adrian Dobre kutoka Romania
na Yusuf Nzawila ameendelea kuwa mtunza vifaa.
Benchi la ufundi la academy:
Mario Marian Anton Marinica kutoka Romania anaongoza benchi la ufundi
la timu ya vijana akisaidiwa na Mtanzania, Dennis Kitambi na Idd Nassor
Cheche. Twalib Mhidin anaendelea kuwa msaidizi wa ‘Team Dr’ kwa vijana
na mtunza vifaa msaidizi wa vijana ni Saleh Sale.
Ukiangalia mfumo huu wa uongozi, Azam
wanastahili pongezi kwa sababu Stewart Hall na benchi lake la ufundi
wanafanya wanavyotaka na hata ukiwatazama wachezaji wanavyocheza kwa
sasa, unaona kabisa hawachezi kwa ajili ya mtu fulani, wanacheza kwa
ajili ya benchi la ufundi.
Stewart siyo kocha tu bali ni meneja wa timu, hakika anatupa maana halisi ya Wazungu ya meneja wa timu.
Meneja anawajibika kuwaongoza wachezaji
kama kundi, pia anawajibika ‘kum-meneji’ mchezaji mmoja mmoja, anatakiwa
kujua anahitaji nini, ana upungufu gani na amsaidieje ili kupata
kilicho bora kutoka kwake.
Mfano mzuri ni wakati Arsene Wenger
anajiunga na Arsenal mwaka 1996. Alikuta wachezaji wengi ni wazee
wakiwemo Tony Adams, David Seaman, Martin Keown, Mathew Upson, Ray
Parlour, Ian Wright na wengineo.
Ili kupata kilicho bora kutoka kwao,
Wenger kwa kushirikiana na mtaalam wake wa vyakula ambaye Azam pia
wanaye, aliwatengenezea wachezaji ‘Menu’ ya kula ili waendelee kuwa na
nguvu uwanjani.
Wenger alikaa na wake wa wachezaji na
kuwapa semina na ratiba ya chakula kwa mcheza mpira, huwezi amini wale,
‘wazee wa Arsenal’ walichukua ubingwa wa England msimu wa 1997/1998.
Baada ya pale, Wenger akatengeneza
falsafa yake, bodi ya wakurugenzi ikamwambia inataka nini na yeye akajua
nini cha kufanya ili malengo yaweze kutimia nje na ndani ya uwanjani.
Azam imekuwa mfano wa kweli katika hili,
bila kugusia matokeo ya Kagame, timu inaonekana kuwa na viongozi
sahihi, wasioingiliana kimajukumu, ndiyo maana wachezaji wanaonekana
kuwa huru na kucheza kwa maelekezo ya benchi la ufundi.
Nawaasa Azam waendelee kubaki katika
msingi huo na wamwamini Stewart ambaye naamini hajawahi kuwa kocha mbaya
zaidi ya wapambe kumharibia kwa wenye timu.
Tukutane Jumamosi ijayo panapo majaaliwa!
Tags
Michezo na burudani