Yanga inapiga tu

humphrey the GREAT


16
Sweetbert Lukonge,
Dar es Salaam
BAO pekee lililofungwa na Amissi Tambwe, jana Jumapili limeiwezesha Yanga kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Khartoum ya Sudan katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga tangu ipoteze mchezo wa kwanza dhidi ya Gor Mahia, imekuwa ikijipigia tu, kwani imeshinda mechi tatu zilizofuata baada ya Gor Mahia.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi tisa katika kundi lake na kushika nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia yenye pointi 10, Khartoum imeshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba.
Keshokutwa Jumatano Yanga itacheza mechi ya robo fainali dhidi ya Azam FC ambayo imeongoza Kundi C ikiwa na pointi tisa. Kesho katika robo fainali, Gor Mahia ambayo jana iliifunga Telecom mabao 3-1, itacheza robo fainali dhidi ya Malakia ya Sudan Kusini.
Katika mchezo wa Yanga na Khartoum ambao ulikuwa wa kukamilisha ratiba na kujitafutia unafuu wa kucheza robo fainali, timu hizo zilicheza soka la kasi na la kushambuliana kwa zamu.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alionekana kuwapumzisha nyota wake kadhaa akiwemo Donald Ngoma, Deus Kaseke huku akiwaingiza dakika za mwisho Geoffrey Mwashiuya na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
26
Tambwe, raia wa Burundi, aliifungia Yanga kwa kichwa dakika ya 30 akiunganisha kona iliyopigwa na kiungo Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda na kuamsha shamrashamra kwa mashabiki wa timu hiyo.
Baada ya bao hilo, Khartoum walijitahidi kutaka kusawazisha lakini ukuta wa Yanga ulioongozwa na Kelvin Yondani na chipukizi Pato Ngonyani ulikuwa imara kuondosha hatari zote zilizoelekezwa kwao.
Yanga mara kadhaa ilifika katika lango la wapinzani wake, lakini bado iliendelea kuandamwa na tatizo la umaliziaji. Kipindi cha kwanza, Khartoum ilionekana ikimiliki mpira vizuri tofauti na kipindi cha pili.
Dakika ya 83 kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ aliyetangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, aliokoa shuti kali lililoelekezwa langoni kwake.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Yanga, Pluijm alisema: “Nimefurahishwa na ushindi tulioupata japokuwa tumekosa nafasi nyingi za wazi, naijua Azam, hivyo najipanga kwa mechi dhidi yao.”
Naye Kocha wa Khartoum, Kwesi Appiah, alisema: “Tumeyapokea matokeo haya bila tatizo kwani wenzetu wametumia kosa letu kupata bao, sasa tunajipanga kwa mechi ya robo fainali.”
Kesho Jumanne katika robo fainali kwenye Uwanja wa Taifa, Gor Mahia itacheza na Malakia halafu itafuata mechi kati ya Al Shandy ya Sudan na KCC ya Uganda. Keshokuwa Jumatano, APR itacheza na Khartoum na mechi ya pili itazikutanisha Yanga na Azam.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post