humphrey the GREAT
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama
msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa
Muziki wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole kufanya
shughuli za sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe
24/07/2015 hadi tarehe 24/07/2016.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015
akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya
kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania na hivyo
akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili. Pia
itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri
kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza bila kuzingatia utu na
maadili awapo jukwaani.
BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo
yake kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo chake cha
kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa
maelezo. Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili ya
kazi ya sanaa kwenye onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na
amekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.
Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa
sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la
Sanaa la Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005
limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka
Mmoja tokea tarehe 24/07/2015.
Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki
kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya
nchi. Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi
ikiwa ni pamoja na yeyote yule utakaye shirikiana naye.
Ni matumaini ya Baraza la Sanaa la Taifa
kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea kutambua
umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
WASANII WATAKIWA KUFUATA TARATIBU WANAPOENDA NJE YA NCHI ILI KUEPUKA MATATIZO NA MIKANGANYIKO INAYOWEZA KUJITOKEZA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo
ni msimamizi wa sekta ya Sanaa nchini linawakumbusha wasanii wote
nchini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo
wanapokwenda nje ya nchi kufanya maonesho au kushiriki shughuli yoyote
ya Sanaa ili kuepuka matatizo na mikanganyiko mbalimbali inayoweza
kujitokeza.
Kwa mujibu wa taratibu zilizopo, msanii
yeyote anapokwenda nje ya nchi anapaswa kujaza fomu maalumu inayotolewa
na BASATA na baadaye kupewa kibali bure (bila gharama yoyote) ambacho
mbali na kueleza wapi msanii anaelekea kinaeleza kwa kina tarehe ya
kuondoka kwa msanii na ile ya kurudi nchini.
Kutokana na kukua kwa sekta ya Sanaa
nchini hususan muziki na filamu wasanii wengi wamekuwa wakipata fursa ya
kwenda nje ya nchi kufanya maonesho na shughuli zingine za Sanaa hivyo
suala la kufuata sheria, kanuni na taratizu za kupata vibali vya kwenda
nje ya nchi ni muhimu sana ili kuhakikisha kwanza; safari zao zinakuwa
na baraka ya moja kwa moja kutoka Serikalini, pili kusaidia upatikanaji
wa takwimu sahihi za wasaniii wanaokwenda nje ya nchi, tatu usalama wa
wasanii wetu na mwisho, kuwakabidhi bendera ya taifa kama ishara ya
uwakilishi na ubalozi wa nchi yetu katika mataifa wanayoyatembelea.
BASATA limekuwa likiwaelekeza wasanii
wote kuomba vibali vya kwenda nje ya nchi na kuripoti katika balozi zetu
zilizoko kwenye mataifa mbalimbali ili kuhakikisha wanakuwa na wenyeji
katika nchi husika kwa lengo la kujitambulisha pia kupata msaada pale
kunapotokea tatizo lolote linalohitaji utatuzi wa Serikali.
Dunia imekuwa na matukio mengi ya
kiusalama ni vema kuchukua tahadhari hasa ikizingatiwa kazi za Sanaa
huambatana na mikusanyiko mikubwa ya watu hali ambayo inaweza kuzaa
matatizo kwa wasanii wetu wakiwa nje ya nchi bila kuwa na nyaraka
stahiki.
Baraza la Sanaa la Taifa linatambua
kwamba wasanii wanapokwenda nje ya Tanzania kwa lengo la kufanya kazi ya
Sanaa wanakwenda kuipeperusha bendera ya Taifa letu, kwa mantiki hii ni
mabalozi wa nchi. Hivyo basi, lazima wawe wazalendo, wajivunie
utanzania na kuiwakilisha vyema nchi yetu.
Ieleweke kwamba Serikali inafarijika na
kupata heshima kubwa inapoona wasanii wetu wakivuka nje ya mipaka na
kwenda kupata mafanikio kwenye majukwaa ya kimataifa suala ambalo ni
kuitangaza Tanzania kupitia Sanaa na Utamaduni baada ya kuzingatia
taratibu zote. Ndiyo maana kupitia mitandao yake ya kijamii na hata
katika programu ya Jukwaa la Sanaa BASATA limekuwa
likihamasisha wadau wa Sanaa kuwaunga mkono wasanii na kuwapigia kura
kunapokuwa na shindano lolote linalohitaji ushindi wa kura (popular
vote). Aidha, BASATA limekuwa likiandika taarifa kwenye vyombo vya
habari kumpongeza msanii yeyote anapofanya vizuri nje ya mipaka ya nchi
yetu.
Ni sababu hii ndiyo imelifanya BASATA
muda wote kuwasisitiza wasanii na menejimenti zao kutambua wajibu wao
kwa serikali hasa katika kuhakikisha wanafuata taratibu zote zilizopo na
kutoa taarifa hitajika serikalini ili kuepuka mikanganyiko na
sintofahamu inayoweza kujitokeza.
Lengo ni kuhakikisha kupitia taarifa
sahihi zinazokuwa zimetolewa na menejimenti za wasanii au wasanii
wenyewe pia kupitia taarifa zilizopo kwenye vibali vya kwenda nje kwa
wasanii husika, Serikali nayo inajipanga ipasavyo katika kuhakikisha
wasanii wetu wanaagwa na baadaye kupokelewa kwa heshima wanaporejea
nchini.
BASATA linaamini kwamba haileti picha
nzuri na kwa kweli inashusha morali wasanii wetu wanaporudi nyumbani na
mafanikio makubwa pasi na mapokezi ya Kiserikali kwa sababu tu
menejimenti za wasanii zinashindwa kujipanga kwa maana ya kuzingatia
taratibu zilizopo na kutoa taarifa stahiki za lini msanii atarejea na
wakati gani ili mamlaka husika ifanye utaratibu wa mapokezi.
Serikali kupitia BASATA imefanya
mapokezi stahiki kwa wasanii Peter Msechu aliposhinda shindano la Tusker
Project Fame, Mtunzi wa filamu Timoth Konrad wakati filamu yake ya ‘Dogo Maasai’
iliposhinda tuzo nchini Marekani na hivi karibuni imefanyika kwa Msanii
Mayunga aliyeshinda shindano la Airtel Tracing Star. Aidha, washiriki
wote wa mashindano ya urembo wamekuwa wakifanyiwa hivyo kama ilivyo
kwenye sekta ya michezo.
BASATA linatoa wito kwa wasanii
kudumisha upendo baina yao na kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano pia
mawasiliano ya karibu na Serikali muda wote kwani zipo mamlaka ambazo
zipo kwa ajili ya kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika tasnia ya
Sanaa.
Ni wazi kwamba kama wadau wote wa sanaa
wakielewa utaratibu huu basi sekta ya Sanaa ambayo kiasili ni ya upendo,
mshikamano na amani itaendelea kukua katika mwenendo mwema na kuwa
yenye tija zaidi kwa wasanii wenyewe pamoja na jamii kwa ujumla. Wasanii
tudumishe upendo, amani na mshikamano.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Tags
Burudani