humph the GREAT
WAZO ni hatua ya kwanza katika
mafanikio, vitendo ni hatua inayofuata. Haijalishi wazo la kufanikiwa
unalipata ukiwa na umri gani, ilimradi tu ukiwa ‘active’ katika
kulitendea kazi.
chanzo: grobal publisher
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa mwanadada
wa Kitanzania, Hellen Dausen ambaye ametajwa hivi karibuni na Jarida la
Forbes katika orodha ya mabilionea wa miaka michache ijayo wenye umri
chini ya miaka 30.
Katika mahojiano ‘Exclusive’ na Over Ze Weekend kutoka
nchini Marekani ambako yuko kimasomo, Hellen amefunguka mambo mengi
ikiwemo siri ya yeye kufanikiwa hata kufika mahali alipo sasa.
OVER ZE WEEKEND: Watanzania wangependa kujua elimu yako, ulikozaliwa na hata kukulia.
HELLEN: Nimezaliwa na
kukulia Mitaa ya Makumbusho, Kijitonyama, Dar. Elimu ya Msingi nilipatia
Shule ya Msingi Muhimbili huku sekondari nikisoma Shule za St. Mary’s
kwa elimu ya awali na baadaye Shaabani Robert zote za jijini Dar.
Nilipomaliza masomo ya sekondari nilijiunga na chuo cha United
International University kilichopo Kenya kwa masomo ya biashara ambapo
nilichukua digrii.
OVER ZE WEKEEND: Elimu yako inaonesha wazi ungeitumia kuajiriwa na kufanya mambo makubwa, nini hasa kilikuvutia kwenye ujasiriamali?
HELLEN: Ndoto yangu
kubwa siku moja niwe bosi. Niwe na kampuni yangu, niweze kuajiri watu na
kuishi maisha mazuri. Baada ya kumaliza tu masomo niliamua kujiingiza
kwenye mitindo nikiamini siku moja nitamiliki kampuni ya masuala hayo.
Nilienda Marekani kusomea mitindo na
uigizaji pia nikiwa huko nilitafuta fursa kwenye tasnia ya u-miss na
mitindo lakini sehemu kubwa niliambiwa mfupi na pia walihitaji wasichana
wenye umri mdogo zaidi yangu miaka 17 hadi 18 na mimi nilikuwa na miaka
25. Sababu hizo zilinikatisha tamaa ambapo baada ya kurudi nyumbani
mwaka 2012 na kukosa kazi ya kufanya ndipo nilipoamua kujiingiza rasmi
kwenye ujasiriamali.
OVER ZE WEEKEND: Lakini
umewahi kuwa mshindi wa u-miss nchini, kwa nini hukuhamishia nguvu
uliyokuwanayo Marekani na kuendeleza masuala ya mitindo nyumbani?
HELLEN: Yah! ni kweli
nimewahi kushinda Shindano la Miss Universe mwaka 2010. Lakini nilisomea
biashara na sikutaka kung’ang’ania kitu ambacho hakiniletei faida hasa
kwenye suala zima la kifedha.
OVER ZE WEKEEND: Wazo la kuwa na ‘products’ zako mwenyewe lilitoka wapi?
HELLEN: Kwa kweli wazo
lilikuja tu bila kutegemea. Ilikuwa ni siku moja nimetoka kuoga nikawa
napaka mafuta ya ubuyu nikajikuta tu najiuliza kwani siwezi kuwa na
sabuni za mafuta haya? Baadaye nikaingia mtandaoni na kuanza kusoma
kuhusu vipodozi vya asili baadaye nikaomba wazazi wangu kuniwezesha na
kwenda kusomea masomo yanayohusu vitu hivyo nchini Malaysia na baada ya
hapo ndiyo kama hivi nina bidhaa zangu ambazo ziko tano. Sabuni za
kuogea, mafuta mepesi ya kupaka, Mafuta halisi ya nazi, body scrub na
zingine pia.
OVER ZE WEKEEND: Changamoto gani ambazo umekutana nazo wakati unaanza?
HELLEN DAUSEN: Sana
ilikuwa ni kukatishwa tamaa, wengi walikuwa wananiambia kwa nini
nisifanye mambo mengine, wengine wakinisema kuwa nachomeka juani na
nisingefika popote lakini Mungu mkubwa nilipambana na wazazi wangu
walinisapoti mpaka nimefika hapa.
OVER ZE WEEKEND: Forbes Afrika walipataje taarifa kuhusu wewe?
HELLEN: Mimi ndiye
niliona tangazo la fomu yao kwenye Ukurasa wa Instagram zikihitaji
kuwafahamu wajasiriamali ambao wanahisi biashara zao ndani ya miaka
michache zinaweza kuwafanya kuwa mabilionea. Kwa hiyo baada ya kuiona
nikaijaza na kawaida ya Forbes huwafanyia uchunguzi wahusika wanaojaza
fomu hizo zaidi ya miezi mitano. Hilo lilifanyika na nikaibuka kuwa
mmoja wa watu waliokuwa wanawahitaji.
OVER ZE WEKEEND: Baada ya Forbes kukutaja katika orodha yao hiyo imekusaidia vipi kibiashara?
HELLEN: Watu wameongeza
imani zaidi kwenye bidhaa zangu. Nakumbuka kabla kuna makampuni
niliyafuata ili kunisapoti kwenye suala zima la mtaji lakini
hayakuonesha ushirikiano, baada tu ya kutangaza yamenitafuta na
tunafanya kazi tena pamoja.
OVER ZE WEKEEND: Shughuli zako hasa unazifanyia wapi kwa sasa? Umeajiri watu wangapi na vipi kuhusu tetesi kuwa una mpango wa kujenga kiwanda?
HELLEN DAUSEN: Makao
makuu yangu kibiashara kwa sasa ni Zanzibar, watu niliowaajiri si zaidi
ya 10. Lakini ni wengi kidogo maana kuna ambao wananisaidia hapo
Zanzibar na wengine Dar ila kuna uwezekano wa kuajiri wengine zaidi
kutokana na ukomavu wa biashara. Kuhusu kujenga kiwanda nina mpango huo
na malengo nikufikia mwaka ujao niwe nimekijenga.
OVER ZE WEKEEND: Kuna namna yoyote serikali inakusapoti tangu Forbes wakutangaze?
HELLEN: Hapana bado haijaanza kunisapoti.
OVER ZE WEKEEND: Vipi kuhusu familia, umeolewa au una watoto?
HELLEN DAUSEN: Hapana sijaolewa, sina mtoto na wala siko katika uhusiano wowote ule.
Tags
Burudani