humph the GREAT
ILIPOISHIA
Waliosema kwamba ukiona giza
linaongezeka ujue mapambazuko yamekaribia hawakukosea. Msemo huo wa
wahenga unaonekana kuanza kutimia kwa Jafet Lubongeja na msichana
aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote, Anna.
Baada ya kupitia kwenye
misukosuko mingi, penzi lao likitawaliwa na machozi, maumivu ndani ya
moyo, usaliti na kukataliwa, hatimaye mapambazuko yameanza kuonekana.
Wawili hao walikutana wakiwa
bado wadogo, Jafet akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana
ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kwimba, Mwanza huku Anna akiwa ni mwanafunzi
wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru.
Penzi zito likachanua kati yao
kiasi cha kumfanya Jafet afikie hatua ya kutoa figo yake moja na kumpa
Anna aliyekuwa anasumbuliwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya
kazi.
Hata hivyo, licha ya wema mkubwa
alioufanya Jafet, baadaye wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet baada
ya Anna kupona kabisa. Sababu kubwa ya kumchukia ni baada ya kugundua
ukweli kwamba kijana huyo alikuwa akitokea kwenye familia maskini sana,
wakaona hana hadhi ya kuwa mkwe wao.
Wakafanya kila kilichowezekana
na hatimaye wakafanikiwa kuwatenganisha wawili hao. Hata hivyo, baadaye
mambo yanaanza kumwendea kombo Anna, anapewa ujauzito na mwanaume
mwingine na wazazi wake wanapoamua kuutoa, maradhi yake ya figo yanarudi
upya.
Mtu pekee anayekuja kusaidia
kumrudishia Anna furaha, akiwa hoi kitandani ni Jafet. Uwepo wake
unasababisha msichana huyo apone maradhi yote yaliyokuwa yanamsumbua,
jambo linalomshangaza kila mmoja. Mwisho wanatafutiwa chuo nchini
Marekani wanakoendelea na masomo kwa bidii.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
ENDELEA
Maandalizi ya mitihani ya kuhitimu chuo
yalienda sambamba na maandalizi ya mahafali, wazazi wa pande zote mbili
nao kwa upande wao wakaanza kujipanga kwa ajili ya kufanikisha mahafali
ya watoto wao. Mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana na Jafet na Anna na
kupeana utaratibu wa jinsi mahafali hayo yatakavyokuwa.
Hatimaye siku ya mahafali iliwadia,
kutoka nyumbani Tanzania, baba na mama yake Anna walisafiri sambamba na
mama yake Jafet ambaye walimlipia kila kitu, kuanzia gharama za kupata
hati ya kusafiria, visa mpaka nauli ya ndege ya kwenda na kurudi.
Jafet hakuamini siku hiyo alipopigiwa
simu na kuambiwa wajiandae kuwapokea wageni kutoka Tanzania. Awali
alihisi lazima watakuwa ni baba na mama yake Anna tu lakini hakuyaamini
macho yake alipomuona mama yake akiwa miongoni mwao, akiwa amependeza
mno.
“Mama! Siamini macho yangu!”
“Ni mimi mwanangu, Mungu kweli mkubwa,
na mimi nimepanda ndege,” alisema mama yake Jafet kwa Kiswahili chenye
lafudhi ya Kisukuma, wote wakacheka na kukumbatiana kwa furaha. Jafet na
Anna waliwaongoza wageni wao mpaka kwenye ukumbi yalipokuwa
yakifanyikia mahafali hayo.
Ilikuwa siku ya furaha sana kwa Anna,
Jafet na wazazi wao kwa sababu hatimaye ndoto yao ya miaka mingi ilikuwa
ikielekea kutimia.
“Siku ulipokataa kwenda kusomea upadri
ulinikasirisha sana moyo wangu, wala sikuwa najua Mungu amekuandalia
nini maishani mwako, wabheja gete bhabha! (hongera sana baba!) alisema
mama yake Jafet na kumkumbatia tena mwanaye aliyekuwa amevalia joho
lililompendeza sana.
Shamrashamra ziliendelea mpaka jioni,
ikabidi wazazi wao waende kutafuta hoteli ya kupumzika, tayari kwa
maandalizi ya kurudi Tanzania siku iliyokuwa inafuatia, Jafet na Anna
wakawasindikiza na kukubaliana kuonana tena asubuhi, wakarudi chuoni
kuendelea na sherehe kwani usiku huo kulikuwa na disko maalum kwa ajili
ya wanachuo wote.
“Niambie kama kweli utanioa!”
“Lazima nikuoe Anna, tena tukirudi
nyumbani tu jambo la kwanza itakuwa ni kukuvalisha pete ya ndoa, hata
mama yangu nimeshamwambia na amesema atazungumza na wazazi wako,”
alisema Jafet, akamkumbatia Anna na kumbusu, kisha wakagusanisha ndimi
zao wakati muziki laini ukiendelea kupigwa ndani ya ukumbi huo, wanachuo
wengi wakiendelea kufurahia mahafali.
“Nitafurahi sana Jafet, nimeshasubiri
kiasi cha kutosha, nataka kuwa mkeo wa ndoa, nataka nikuzalie watoto
wazuri kama baba yao,” alisema Anna kwa hisia za hali ya juu,
wakaendelea kukumbatiana huku wakicheza muziki mpaka baadaye kila mmoja
alipoanza kuonesha dalili za kuchoka.
Wakaondoka na kwenda kulala, kila mmoja
kwenye hosteli yake ambapo asubuhi waliamshana na kwenda mpaka kwenye
hoteli waliyofikia wazazi wao. Maandalizi ya safari yakaendelea ambapo
baadaye, waliagana na wazazi wao waliofunga safari kuelekea uwanja wa
ndege wakati wao wakirudi chuoni.
Siku zilizidi kusonga mbele, hatimaye
wakafanya mitihani yao ya mwisho na kusafiri kurejea nchini Tanzania
ambapo walipokelewa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na wazazi wa pande zote
mbili.
Breki ya kwanza ilikuwa nyumbani kwa
akina Anna ambapo kwa kuwa tayari Jafet alishawaambia wazazi wake,
iliandaliwa sherehe ndogo ya kuwapongeza wawili hao, Jafet akaitumia
nafasi hiyo kumvalisha pete ya uchumba Anna, wawili hao wakaanza ukurasa
mpya wakiwa wachumba rasmi.
Walikaa jijini Mwanza kwa siku kadhaa,
baadaye wakaondoka pamoja kuelekea kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa akina
Jafet. Kutokana na kukaa Marekani kwa kipindi kirefu, mfumo wao wa
maisha ulibadilika kabisa, wakawa wanaishi kama Wamarekani weusi.
Baada ya kukaa kijijini kwa siku kadhaa,
walirejea jijini Mwanza ambako tayari baba yake Anna alishawafanyia
mipango ya kupata kazi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Wakaanza
kazi katika hospitali hiyo, Anna akiwa daktari wa figo, Nephrologist,
wakati Jafet yeye akiwa ni mtaalamu wa mishipa ya fahamu.
Japokuwa walikuwa wakifanya kazi, bado
walikuwa wakiishi nyumbani kwa akina Anna walikotengewa vyumba vyao,
huku mipango ya ndoa yao ikizidi kupamba moto.
MIEZI 7 BAADAYE
Jafet alikuwa amevalia suti maridadi ya
rangi ya maziwa, huku Anna akiwa amevalia shela kubwa jeupe lililomfanya
apendeze kuliko kawaida. Nyuma yao, kulikuwa na wapambe wao ambao nao
walivaa nguo zinazofanana na za kwao, muziki wa taratibu ukawa unapigwa
huku wakitembea taratibu kuingia ukumbini, shangwe na vifijo vikisikika
kila upande.
“Wanameremetaaa! Wanameremetaaa!
Wanameremetaaa!” watu wote ukumbini walikuwa wakiimba huku wakipiga
vigelegele na shamrashamra za kila aina. Jafet na Anna walikuwa
wakiingia ukumbini, baada ya mchana wa siku hiyo kufunga ndoa takatifu
katika Kanisa la Kristo Mfalme jijini Mwanza, harusi iliyohudhuriwa na
watu wengi na kuweka rekodi ya kipekee jijini humo.
Baada ya kuingia ukumbini, maharusi
walienda kukaa sehemu waliyoandaliwa, watu wote wakakaa kwenye siti zao
na ratiba zikaendelea kama kawaida. Muda wote mama yake Jafet alikuwa
akitokwa na machozi kwani hakuamini kwamba mwanaye huyo, aliyekulia
katika mazingira magumu kiasi kile, alikuwa akifunga ndoa ya kifahari
kama hiyo, tena akiwa anamuoa msichana mrembo kutoka familia ya
kitajiri, Anna. Muda wote akawa anainua mikono juu kama ishara ya
kumshukuru Mungu wake.
Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Anna,
alikuwa haamini kwamba hatimaye amekuwa mke halali wa Jafet. Muda wote
alikuwa akitazama kidole chake kilichokuwa na pete mbili, ya uchumba na
ya ndoa, akawa anajihisi kama yupo ndotoni. Taratibu za ukumbini
ziliendelea mpaka saa sita za usiku ambapo maharusi walitoka na kwenda
hotelini.
Kesho yake asubuhi wakasafiri kwenda kwenye Visiwa vya Shelisheli kwa ajili ya kula fungate lao.
“Siamini Jafet! Siamini kama kweli leo
nimekuwa mke wako, nakupenda sana mume wangu,” alisema Anna, wakiwa
wamejilaza kwenye vitanda maalum vya kamba, wakipunga upepo wa baharini,
kwenye hoteli ya kitalii ya Coconut Empire kwenye Visiwa vya
Shelisheli.
“Nilikuahidi Anna kwamba lazima
nitakuoa, namshukuru Mungu kwamba hatimaye umekuwa mke wangu,” alisema
Jafet, akamkumbatia Anna na kugusanisha ndimi zao. Muda mfupi baadaye,
walibebana msobemsobe mpaka chumbani, wakapeana haki yao ya ndoa.
Siku tatu baadaye, Jafet alipokea simu
iliyoonesha kwamba ilikuwa inapigwa kutoka nje ya nchi hiyo,
harakaharaka akapokea ambapo sauti ya mwanamke ilimtaarifu kwamba
anatakiwa kusoma barua pepe aliyotumiwa kwani ilikuwa muhimu sana.
Harakaharaka Jafet alichukua laptop yake na kuiwasha, Anna akiwa pembeni yake wakafungua upande wa barua pepe.
“Whaaat?” (Niniii?) alisema Jafet akiwa
ni kama haamini. Ilikuwa ni barua iliyomtaarifu kwamba alikuwa
amechaguliwa kuwa miongoni mwa madaktari watakaoenda kufanya kazi makao
makuu ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) jijini Geneva,
Uswisi. Barua pepe hiyo ilimueleza kwamba atagharamiwa kila kitu yeye na
mkewe, kuanzia nauli, makazi, malazi na atakuwa analipwa mshahara
mzuri.
Jafet alibaki amepigwa na butwaa akiwa
ni kama haamini, akakaa na mkewe na kujadiliana ambapo walikubaliana
kwamba wakubali wito huo. Badala ya kukaa siku thelathini kwenye fungate
lao, walikaa siku kumi tu, wakarejea Tanzania ambapo walizungumza na
wazazi wa pande zote mbili ambao nao walifurahi sana kusikia taarifa
hizo na kuwapongeza wanandoa hao.
Wiki moja baadaye, mipango yote ya
safari ilishakamilika, wakasafiri mpaka jijini Geneva, Uswisi na
kuyaanza maisha mapya huku Anna akiwa na dalili za ujauzito. Miezi tisa
baadaye, alijifungua watoto wawili mapacha, wa kiume na wa kike ambao
walizidisha furaha kwenye ndoa yao.
Maisha yakaendelea kwa raha mustarehe
huku kila likizo wakifunga safari mpaka nchini Tanzania kuwasalimu
wazazi wao. Jafet aliyabadilisha kabisa maisha ya nyumbani kwao. Ile
familia ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa ikidharaulika kwa sababu ya
umaskini, ikageuka na kuwa gumzo kutokana na utajiri na mafanikio
yaliyopatikana.
Mwisho.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/
Tags
Hadithi & Simulizi