Tozo za kutuma, kutoa fedha kwa njia ya simu ziangaliwe upya!

humph the GREAT
 Money-Mobile-Phone   
Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutupa afya njema mimi na wewe leo na kama kuna mtu anaumwa, basi kwa pamoja tumuombee  apone haraka. Baada ya kusema hayo nizungumzie tozo za huduma ya kutuma au kupokea fedha kwa njia ya simu.
Nasema hivyo kwa sababu tangu Julai Mosi mwaka huu watu wamekuwa wakilalamika kwamba wanatozwa fedha nyingi kwa kuwatumia fedha ndugu zao kwa njia ya simu.
Niliposikia malalamiko hayo nami nikajitosa kwa wakala mmoja ili nione kama walalamikaji wanasema kweli au ni porojo zao tu.
Nilikwenda kwa wakala mmoja nikiwa na orodha ya ndugu zangu niliotaka niwatumie fedha kidogo kwa ajili ya matumizi yao. Orodha hiyo ilikuwa na watu watano.
Nilipompa wakala wa kutuma fedha kwa njia ya mtandao alisema kila fedha nitakayotuma pale sina budi kuongeza shilingi 500 kama gharama ya kutuma fedha kwa ndugu zangu hao. “Ama sivyo nikuingizie fedha hizo katika akaunti yako kisha utume mwenyewe,” alinieleza wakala huyo wa mitandao ya kutuma fedha.
Nilifikiri kidogo nikaamua ni bora nifanye hivyo ili nijue ni kiasi gani nitatumia kwa kuwatumia fedha watu hao. Nilimpa fedha akaziingiza katika akaunti ya simu yangu.
Nilituma fedha kwa watu wale na nikagundua kuwa kila niliyemtumia, nilikatwa shilingi 300, sikuwauliza wapokeaji kama nao walitozwa fedha wakati wanachukua fedha nilizowatumia.
Kwa watu wale watano niliowatumia fedha, nilijikuta nikikatwa shilingi 1,500 jumla, si fedha ndogo ni nyingi hivyo wahusika wanapaswa kuliangalia hili.
Nasema wanapaswa kuliangalia kwa sababu ningeruhusu wakala anitumie kwa gharama alizonitajia ya shilingi 500 kwa kila mtu, kwa watu watano, ningelipa shilingi 2,500.
Hiyo ni kwa mimi ambaye nipo jijini Dar es Salaam, naamini huko mikoani wananchi watakamuliwa zaidi hasa kwa kuwa baadhi yao hasa wale wa vijijini hawajui lolote, wanaweza kujikuta wakitozwa gharama kubwa zaidi.
Niliwahi kumsikia mtu akisema ‘Ukitumiwa shilingi 100,000 unakatwa shilingi 20,000.’ Nilimsogelea mtu yule na kumwambia asipotoshe watu, si kweli hilo analolisema, yeye akajitetea kuwa naye aliambiwa na mtu mwingine.
Mikanganyiko hiyo ndiyo iliyonifanya nitumie muda wangu kutuma mwenyewe fedha lakini pia kuingia katika utafiti mdogo kama mlivyoona hapo juu.
Ni jukumu sasa la vyombo husika kuchukua muda wao kuelimisha jamii kuhusu makato anayokatwa mtumaji na mtumiwa fedha ili kuepusha watu kuibiwa na mawakala wenye uroho wa kujitajirisha haraka kwa kuwanyonya watu wasiojua.
Ni kawaida sana katika nchi yetu kungoja kitu kilalamikiwe na watu na kelele zikiwa nyingi ndipo wahusika hukuguta na kuanza kuelimisha umma kwa gharama kubwa, huku wananchi wakiwa wameumia kama tulivyoona zoezi la kufungia simu feki, wakaguzi na wadhibiti wa ubora wa simu hawakujali na sasa walalahoi ndiyo wanaoadhibiwa kwa kuzimwa simu zao.
Ili watu wasiibiwe, haya mambo yawekwe hadharani mapema. Kinga ni bora kuliko tiba.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post