Hussein Jumbe: Nimechungulia kaburi, asante Mungu

humph the GREAT
Hussein Jumbe 
                                    MKONGWE wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe ni mgonjwa. Katika mitandao mbalimbali ya jamii wiki iliyopita, zikaenezwa taarifa kuwa staa huyo wa miaka mingi yu mahututi, jambo lililosababisha Risasi Vibes kumtembelea mmiliki huyo wa Talent Band nyumbani kwake, Temeke jijini Dar es Salaam.
Nyumbani kwake, safu hii ilimkuta Jumbe, ambaye mwaka 1999 aliwahi kuzushiwa kifo, akiwa bado kitandani huku mkewe akisema hivi sasa ni nafuu kuliko wiki tatu zilizopita, ambapo alipoteza kabisa fahamu.
Zakia Hussein, mke wa mwimbaji huyo wa zamani wa Mlimani Park Orchestra, alisema mumewe alianza kuugua Julai 27, mwaka huu baada ya kutoka katika ziara mikoani, akilalamika kifua chake kuwa kizito na maumivu makali.
“Hali ilizidi kuwa mbaya kila siku zilivyokuwa zinazidi kwenda, nikampeleka Hospitali ya Kwa Massawe hapahapa Temeke, akafanyiwa kipimo cha X-RAY na kuonekana kifua chake hakina matatizo, pia damu iko safi ila wakasema ana nimonia.
“Akalazwa siku mbili huku akiwa ametundikiwa dripu sita, tukarudi nyumbani, lakini hali ilizidi kuwa mbaya, huku akiwa hajui kinachoendelea kwani alikuwa haongei wala hamtambui mtu yeyote.
“Baada ya kuona hivyo kuna ndugu yetu mmoja akaja, akatushauri tumpeleke kwenye hospitali ya Wakorea iliyopo Sinza, tukaenda ndipo akaanzishiwa matibabu upya, huku akiambiwa asitishe matumizi ya dawa za nimonia kwani hana na zimeingiza sumu nyingi mwilini.
“Alivyofanyiwa vipimo hospitalini hapo, aligundulika kuwa ana ugonjwa wa kisukari ambao ulikuwa umepanda mpaka kufikia 40, ndipo akaanzishiwa matibabu ya haraka.
“Kwa sasa tunamshukuru Mungu hali inaendelea vizuri na kila siku asubuhi lazima turipoti hospitali ambako anaendelea na matibabu,” alisema Zakia.
Kwa upande wake, mkali huyo wa kibao cha Nachechemea, Jumbe aliwashukuru Watanzania wote kwa dua zao na kuwatoa wasiwasi kwamba kwa sasa anaendelea vizuri tofauti na mwanzo.
“Kwa imani ya dini yangu, inasema kuugua ni ibada na usipougua ndani ya miaka mitano unapaswa kujiuliza ni kwa nini hujapitia hatua hiyo, maana ndiyo njia mojawapo ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
“Nakumbuka mwaka 1999 ndiyo niliugua sana kama hivi mpaka watu wakatangaza kuwa nimekufa, nimejifunza kitu kikubwa sana katika kuugua kwangu, kwamba tunatakiwa tuishi na binadamu wenzetu vizuri na jamii inayotuzunguka kwani ukipata shida wao ndiyo wanaokusaidia.
“Ninawashukuru sana waandishi wa habari kwani kama siyo wao Watanzania wasingejua kama mimi nina matatizo, niwaambie tu mashabiki wangu kwamba Talent Band inaendelea kama kawaida aliyekosekana ni Jumbe tu, lakini nawaahidi hivi karibuni hali yangu ikitengemaa nitarudi tena jukwaani muda wowote,” alisema Jumbe.
Hata hivyo, aliwaasa watu wanaovumisha vitu ambavyo havina ukweli waache mara moja kwa sababu vinaumiza sana familia yake na mashabiki kwa jumla.
“Jamani mnaonizushia habari za uongo nawaomba muache, maana hivi ninavyoumwa kuna watu walisema nimekatwa miguu yote, kitu ambacho siyo kweli na kimeumiza sana familia yangu ni kama ilivyokuwa mwaka 1999 walivyozusha kwamba nimekufa, watu wakajaa hapa nyumbani kwa ajili ya kuja kunizika,” alisema Jumbe.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post