MWANAMUME mmoja mburudishaji amewashangaza wengi kwa uwezo wake wa
kugongelea misumari kwenye mbao akitumia kichwa chake mithiri ya nyundo.
Video na picha zilizowekwa kwenye tovuti ya asasi ya rekodi za dunia cha
Guinness, zilionyesha umati ukishangazwa na jamaa huyo mkazi wa Boston
nchini Marekani, John Ferraro.
Maelezo ya wataalamu wa afya yanasema fuvu lake la kichwa ni karibu mara tatu kwa uzito ikilinganishwa na binadamu wa kawaida.
Katika moja ya matukio alishuhudiwa akigongelea misumari 38 ya inchi
tisa katika mbao kwa dakika mbili tu, akilenga kuvunja rekodi ya dunia
kuhusu misumari mingi zaidi iliyogongelewa kwa kutumia kichwa kwa dakika
chache zaidi.
Inasemekana mbali na kipaji hicho kisicho cha kawaida, jamaa huyu ni mwanamieleka.
Ferraro si tu ana uwezo wa kupigilia misumari kwa kichwa bali pia
anaweza kustahimili tofali zito kuvunjwa kichwani mwake kwa kutumia
mipira mizito ya mchezo wa kuviringisha tufe (bowling).
Kana kwamba hiyo haitoshi, Ferraro huruhusu watu kuvunja matofali katika kichwa chake.
Ferraro ambaye ni mkazi wa Boston mara ya kwanza alijigundua kuwa na
kipaji akiwa mvulana wakati alipojigonga kichwa kwa kishindo kikubwa
katika mlango wao mzito uliotokana na mwaloni wakati akimkimbiza kaka
yake.
Mwenyewe anasema: “Nikiwa bado mdogo wakati namkimbiza kaka yangu
ulipotokea ugomvi, alifunga mlango kwa nyuma ili kunikwepa. Kwa bahati
mbaya sikuwa na hili wala lile nilijikuta nikiugonga kwa kishindo kwa
kichwa kwa bahati mbaya na kusababisha ulegee bawaba zake na fremu zake.
“Wakati nilipokuwa mkubwa nilitumia kila aina ya mbinu kukuza kipaji
changu kupitia usomaji wa vitabu vya zamani na makala kisha kufanyia
mazoezi niliyojifunza pamoja na mbinu za mafunzo.
“Maandalizi, mafunzo na dhamira ya kufikia lengo viliniwezesha kujiamini
juu ya uwezo wangu. Wakati muda wa kufanya onesho huwa nafanya kweli na
kutoa burudani itakiwayo.
“Wakati wa maonesho haya ya kugongelea misumari, kupasua tofali kichwani
kwa kutumia mpira mzito, 'maumivu huwa si kitu hata kidogo, nguvu ya
akili na moyo ndivyo vinavyoniongoza. Inapobidi kutoka damu kwa ajili ya
sanaa niioneshayo, hutoka damu. Ni kitu cha kukufanya uweze kujiamini
mwenyewe,” anasema.
Anasema kuwa unachotakiwa ni kujiamini kwamba una nguvu na kitu kitapinda, kuharibika au kuvunjika.
Kitabibu, fuu la mburudishaji huyo ni karibu mara tatu ya wastani wa
kawaida wa binadamu, likipimika kwa unene wa milimita 16 kulinganisha na
wastani wa milimita 6.5 wa kawaida.
Ferraro alifanyiwa vipimo vya scan ya MRI katika shule ya Utabibu
Harvard mjini Boston na wataalamu wa nyolojia na maradhi ya ubongo.
Ilifichua kwamba hana tatizo lolote la kiafya katika fuu lake na kumfanya Ferraro aamini ni zawadi toka kwa Muumba.
Kupitia uchunguzi wa kina wa x-ray, wataalamu wa afya walibainisha kuwa
ubongo wa mburudishaji huyo uko vizuri licha ya kukumbana na vipondo
karibu kila siku wakati akifanya maonesho.
Anasema: “Kamwe sijawahi kuumia au kupata athari kichwani au ubongoni
kutokana na nguvu kubwa ya vipondo kichwani. Madaktari wanashangazwa
kwamba niko vile vile kiafya bila kuumia kutokana na shughuli pevu ya
gongagonga inayokabili kichwa.
Farraro kwa sasa ameshaweka rekodi mbili katika Kitabu cha Rekodi za
Dunia, Guinness World Records moja ikihusu kuvunjwa kwa tofali kwa
kutumia mpira mzito wa bowling wenye uzito wa lb 16 sawa na kilo saba
kutokea umbali wa futi 10 juu ya kichwa chake. Nyingine ya kupigilia
msumari katika mbao kwa kutumia kichwa.
0 Comments