humph the GREAT
MAMA shujaa! Ikiwa imebaki miezi minne na siku kadhaa itimie miaka
miwili kutokea kwa kifo cha aliyekuwa kada muaminifu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, marehemu Deo
Haule Filikunjombe, mkewe Sarah Filikunjombe (Pichani) amethibitisha
ushujaa kwa kuendelea kupambana na changamoto za kimaisha na kufikia
vilele mbalimbali vya mafanikio, Ijumaa limemfungia kazi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita na mwanzoni mwa wiki hii, kwa siku tatu
tofauti, waandishi wetu walijipa kazi ya ziada ya kumtafuta Sarah ili
kujua nini kimeendelea katika maisha yake baada ya kuondoka kwa mumewe
ambapo walibaini mambo mengi mazuri yenye kutia moyo, ambayo mama huyu
licha ya kuonekana sistaduu, ameyafanya kwa ujasiri wa kipekee.
IJUMAA NYUMBANI KWAKE
Hatimaye Jumanne mchana, gazeti hili lilifika nyumbani kwake, Kijichi
Mbagala jijini Dar na kufanya naye mahojiano ambapo alitoa ushirikiano
wa kutosha na kufunguka mengi juu maisha yake tangu kuondokewa na
mumewe.
BAADA YA KIFO CHA MUMEWE
“Kufiwa ni kovu la milele maishani, kifo cha mume wangu kiliniumiza sana
na hata sasa sijapona jereha hilo, nililia, nilihuzunika na bado
nahuzunika lakini ilikuwa lazima maisha yaendelee. Aliniacha na watoto
ambao bado ni wadogo hivyo wanahitaji uangalizi wa hali ya juu, kwa hiyo
ilinibidi nijipange upya namna ya kuwatunza,” alisema Sarah na
kuongeza; “Ukiondoa nyumba na miradi mingine, mume wangu aliacha Kampuni
ya Jumbo Camera House inayojishughulisha na uuzaji wa kamera za kisasa,
iliyopo Posta Mpya, kwenye Jengo la Benjamin Mkapa, lakini sikutaka
kabisa kutegemea kitu hicho pekee, niliamua kuangalia njia nyingine za
kuingiza kipato ili nikikusanya huku na huku, maisha yanasonga kwa
wepesi.
“Hivyo, nilianza kujishughulisha na kilimo na ufugaji ambapo nafuga kuku
wa kisasa na pia nina mabwawa ya kufuga samaki aina ya kambale, vyote
hivyo viko wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani, pia nimewekeza kwenye
vinywaji ambapo nimefungua baa iliyopo Vianzi hukohuko Mkuranga na
vilevile niko kwenye hatua ya mwisho kukamilisha mradi wa kuuza unga wa
sembe ambao nitakuwa naufunga kwenye viroba, yote hayo yako chini ya
Kampuni ya Tripple L, ambayo inawakilisha majina ya wanangu wapendwa
watatu, Lee, Levis na Larry ambapo hata nembo ya viroba vya unga itakuwa
na picha yetu wote wanne,” alisema Sarah.
MARAFIKI WAPO PAMOJA NAYE?
“Idadi imepungua kwa kweli, hata wale marafiki waliokuwa karibu na mume
wangu hawana tena ule ukaribu kama ilivyokuwa zamani, lakini huwezi
kulaumu maana majukumu yanabana na kila mtu anapambana kukimbiza ndoto
zake maishani.
“Hata marafiki zangu wamebaki wachache sana, wengi walidhani ningekuwa
tegemezi na niseme bila kuficha walikuwa karibu na mimi kipindi mume
wangu akiwa hai, wakitarajia msaada wa haraka . Sasa mambo yamebadilika,
ingawa mimi nipo na ninapigana na maisha, simtegemei mtu zaidi ya Mungu
na wale wanaokuwa karibu yangu maana sasa nina marafiki wapya kabisa,”
alisema Sarah.
KUNA HILI LA MADENI “Katika mzunguko wa kutafuta mafanikio maishani,
hususan kwa wafanyabiashara jambo la madeni halikwepeki, iwe kudai au
kudaiwa. Sisi tunadaiwa na duka moja kule Dubai, wakati mume wangu akiwa
hai, alikopa mzigo na alifariki tukiwa bado hatujakamilisha lakini
Mungu yu mwema ulipaji utakamilika na pia tuna pesa tunadai, siwezi
kusema ni wapi lakini ieleweke tu kwamba kuna mahali tunadai na vilevile
matarajio ya kulipwa ni makubwa,” alisema.
SUALA LA MIRATHI LIKOJE?
“Kuna watu wanashughulikia jambo hilo, hivyo siwezi kulisemea chochote.”
ANASAIDIA NYUMBANI KWAO?
“Japo si kwa haraka kama ilivyokuwa zamani, sasa hivi wakihitaji msaada
kutoka kwangu, lazima niwaambie wasubiri kwanza nijikusanye au kuangalia
kilichopo kwa wakati huo, unajua kwenye familia yetu ni mimi na dada
yangu ndiyo tumejaaliwa kuwa na unafuu wa kimaisha hivyo familia yetu ni
ya kawaida sana kwa maana ya kipato,” alisema Sarah.
MSAADA KWA WANAWAKE WENZAKE
“Sitaki kujisifia juu ya hilo, lakini kwa kidogo nilichojaaliwa kwa
maana ya mawazo ya kimaisha, huwa nashirikiana sana na wanawake
wenzangu, hususan wajane kama nilivyo, kuna kipindi nilikuwa naendesha
mafunzo ya namna ya kufuga samaki bure na elimu ya kufungua miradi
mbalimbali, sikutaka malipo yoyote na hata sasa huwa nawafundisha,
nikitarajia malipo kutoka kwa Mungu,” alisema Sarah.
VIPI KUHUSU MRITHI WA DEO?
“Hapana, kwa sasa nimeelekeza nguvu na akili yangu yote kwa wanangu,
nawapenda mno, zaidi ya neno lenyewe na hata wao wanajua kuwa nawapenda,
napambana kuhakikisha wanapata mahitaji yao yote kwa wakati, sitaki
kujiingiza kwenye mambo ya kuwekeana msongo wa mawazo na mwanaume
mwingine, pia hayupo wa kuziba pengo la marehemu mume wangu mpendwa,
ameacha nembo ya milele maishani mwangu, kwa hiyo siwezi kuwaza kuwa na
mtu kwa sasa,” alisema.
NENO LAKE KWA WAJANE NA WANAWAKE KWA UJUMLA
“Kufiwa ni jambo moja, lakini haipaswi kulia tu
bila kutenda jambo. Kama nilivyosema mwanzoni, kovu la kufiwa lina
maumivu ya kuvuka kiwango cha kutamkwa, lakini lazima mwanamke asimame
na kupambana na maisha, wapo wanawake wengi walifiwa na wanaume zao na
kuwaacha mikono mitupu kabisa, wakati mwingine kunyang’anywa kila
kilichokuwepo na baadhi ya ndugu, lakini leo hii wamesimama na
kufanikiwa zaidi ya ilivyokuwa awali. “Nguvu ya mwanamke ni kubwa,
mwanamke ni kiumbe wa pekee mno akiamua kufanya jambo kwa kuielekeza
akili na nguvu yote kwenye jambo husika, lazima lifanikiwe ndiyo maana
kuna ule msemo kwamba nyuma ya mafanikio ya kila mwanaume kuna mwanamke,
hivyo sisi ni Generation point (chanzo cha uzalishaji) ya mafanikio,
Mungu ameweka nguvu kubwa mno maishani mwetu, wanawake tuamke na tuzidi
kupambana huku tukimuweka Mungu kama nguzo muhimu maishani,” alisema
Sarah.
ANAO MPANGO WA KUJITOSA KWENYE SIASA?
“Sifikirii, nina mambo mengi sana kuhusu maisha na siasa inahitaji muda
wa kutosha katika kuwahudumia wananchi, nilikuwa naona wakati wa mume
wangu, jinsi alivyokuwa akijitoa kwenye siasa na wakati mwingine zaidi
ya ilivyokuwa kwa familia, kwa hiyo sina wito wa siasa, mimi napambana
na maisha tu,” alisema Sarah Filikunjombe katika mahojiano hayo maalum.
NI MAUMIVU KUKUMBUKA, LAKINI TURUDI NYUMA KIDOGO
Marehemu Deo Haule Filikunjombe alifariki dunia Oktoba 15, mwaka 2015
wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, katika ajali ya chopa ilikuwa na
usajili namba 5Y-DKK ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Selous, ambapo watu
wengine watatu walifariki, akiwemo rubani William Silaa, aliyekuwa
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Egdi Mkwera na aliyekuwa
mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Vitalis Blanko Haule