humph the GREAT
JESHI la Polisi mkoa wa Pwani limetangaza zawadi ya Sh. milioni tano kwa
mwananchi ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 12 ambao limedai
wanajihusisha na mtandao wa mauaji yanayoendelea katika Wilaya za
Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Onesmo
Lyanga, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Jeshi hilo linaendelea
kuwasaka watuhumiwa hao.
Alisema Polisi imepata picha za baadhi ya watuhumiwa na fununu za mahali wanapopenda kutembelea mara kwa mara.
MAJINA YA WATUHUMIWA
Kamanda Lyanga aliwataja watuhumiwa hao pamoja na mwanzilishi wa mtandao
huo wa mauaji kuwa ni Abdurshakur Ngande Makeo, Faraj Ismail Nangalava,
Anaf Rashid Kapera, Said Ngunde na Omary Abdallah Matimbwa.
Wengine ni Shaban Kinyangulia, Haji Ulatule, Ally Ulatule, Hassan
Uponda, Rashid Salim Mtulula, Sheikh Hassan Nasri Mzuzuri na Hassan
Njame.
“Jeshi letu limewabaini watuhumiwa hao kwa kushirikiana na wasiri wetu
huku tukiendelea na uchunguzi zaidi," alisema Kamishna Lyanga.
Alisema polisi imegundua kuwa watuhumiwa hao hupendelea kutembelea
maeneo ya kisiwa cha Simbaulanga, kisiwa cha Saninga katka kijiji cha
Nchinga na kijiji cha Mfesini kata ya Nyamisati pamoja na maeneo
mbalimbali ya wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.
Kamishna Lyanga aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa
kuwafichua watuhumiwa wote wa mtandao ambao unahatarisha hali ya usalama
mkoani hapa.
LHRC KUANIKA UKWELI
Jijini Dar es Salaam, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC),
kimesema hakijaridhika na hatua ambayo inachukuliwa na serikali chini ya
Wizara yake ya Mambo ya Ndani katika kushughulikia mauaji yanayoendelea
nchini na kuitakata kutafuta njia madhubuti ya kudhibiti mauaji hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu
Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga, alisema kumekuwa na matukio ya mfululizo
katika kipindi kifupi hususani katika Mkoa wa Pwani, lakini mpaka sasa
hawaoni njia mbadala ambayo imefanywa na serikali kuhusu mauaji hayo.
Alisema kupeleka askari wengi Mkoa wa Pwani na maeneo mengine
kunakotokea mauaji hayo hakutasaidia endapo hakutafanyika uchunguzi wa
kina kujua chanzo chake.
“Kinachotakiwa hapa ni kuhakikisha inatafutwa njia madhubuti ambayo
itasaidia kuja na majibu ya kutatua tatizo hili, wafanye uchunguzi wa
kawaida wa kijamii, kukaa na wananchi, tunaamini watapata tu sababu zake
na hapo ndipo itakuwa mahali pazuri pa kuanzia na hii pia itasaidia wao
kujua ni mbinu gani watumie kuwashughulikia,” alisema.
Alisema LHRC ilipeleka timu yake mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya
uchunguzi juu ya matukio hayo ya mauaji na kwamba hivi sasa wako katika
hatua za mwisho za mapitio ya ripoti ya uchunguzi na itasomwa hadharani
ikikamilika.
Mauaji ya raia na hasa viongozi wa kisiasa katika wilaya hizo za mkoa wa
Pwani yalianza kama utani Aprili 30 mwaka jana alipopigwa risasi
mwenyekiti wa kijiji, Said Mbwana kabla ya kushika kasi na kupoteza
maisha ya watu zaidi ya 30 wakiwamo polisi.
Kiongozi wa mwishoni kuuawa ni aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kata ya Bungu wilayani Kibiti na mkoani Pwani, Arife Mtulia wiki
iliyopita.
Mtulia aliuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana ambao hawakuchukua chochote wakati akienda kuoga usiku.
Kifo cha Mtulia kimekuja huku kukiwa na operesheni kabambe ya kusaka
majambazi yaliyoua polisi nane katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa
katikati ya mwezi uliopita.
Polisi inaendesha kimyakimya operesheni hiyo kwa hofu ya kuanika
kinachofanywa na kikosi cha operesheni katika kuchunguza tukio hilo.
Polisi hao waliuawa saa 12:15 jioni wakati wakitoka lindo kuelekea kambini.
Waliouawa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, askari mwenye
namba F.3451, Koplo Francis, F.6990 Konstebo Haruna, G. 3247 Konstebo
Jackson, H.1872 Konstebo Zacharia, H.5503 Konstebo Siwale, H. 7629
Konstebo Maswi na H. 7680 Konstebo Ayoub.
Majambazi hao walipora bunduki saba ambazo ni SMG nne na Long Range tatu zikiwa na risasi zake.
Operesheni hiyo inayoendelea kwenye mapori na maeneo mengine inahusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Imeandikwa na Robert Temalilwa na Magreth Malisa, KIBAHA na Elizabeth Zaya, DAR
Tags
HABARI
