Wachezaji wa Simba wakiwa katika picha ya pamoja.
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kama timu yake itaendelea kuonyesha kiwango kama walichocheza dhidi ya Mtibwa Sugar, wanaweza kufungwa na Yanga.
Hans Poppe alionyesha hasira za wazi baada ya kumalizika mechi ya Simba na Mtibwa Sugar wikiendi iliyopita ambayo walitoka sare ya bao 1-1. Simba ilisawazisha dakika ya 90+4 kupitia kwa mkwaju wa faulo uliopigwa na Emmanuel Okwi.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, mchezo uliojaa upinzani wa hali ya juu kwa kila timu.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Hans Poppe alisema, iwapo Simba itaendelea kucheza kiwango cha chini basi kuna uwezekano mkubwa wa kufungwa na Yanga.
“Wachezaji hawajitumi kutafuta mabao, badala yake timu inacheza kwa kuzuia tu, wachezaji hawafundishwi ipasavyo, wanatakiwa wabadilike ili tuweze kupata matokeo mazuri katika kila mchezo.
“Iwapo wataendelea kucheza katika kiwango hiki, Yanga watatufunga tu Oktoba 28, wachezaji wanatakiwa wajitume,” alisema Hans Poppe.
Kabla ya kukutana na Yanga wiki ijayo, leo Jumamosi Simba inacheza na Njombe Mji kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ukiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara.
Agosti 23, mwaka huu, Simba na Yanga zilikutana katika mechi ya Ngao ya Jamii ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda kwa penalti 5-4 baada ya muda wa kawaida kutoka suluhu.
0 Comments