humph the GREAT
WANAMUZIKI nguli wa muziki wa dansi nchini ambao ni Raia wa DRC, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanae, Papii Kocha wameanza maandalizi ya ujio wao mpya katika muziki, ikiwa ni takribani miaka 14 tangu waachie kibao cha mwisho kabla ya kupelekwa gerezani.
“Miaka 14 si mchezo, mambo kama haya si unayaona mwenyewe, niliyamiss, nimemiss vitu vingi, picha za ukweli, mambo haya kule tulipotoka hamna. Lazima uelewe hii ni dunia nyingine,” alisema Papii Kocha.
Papii amesema kuwa kazi zao mpya zitakuwa nzuri zaidi ya zile za zamani. “Kwasababu tumejipanga vizuri na kazi zinazokuja zitakuwa nzuri zaidi ya zile tulizofanya mwanzo,” amesisitiza Papii.
Wanafamilia hao ambao walipewa msamaha na Rais Dkt. John Magufuli kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 56 ya Uhuru, Desemba 9, mwaka jana, Serikali imeonesha nia ya kuwasaidia waimbaji hao wanaopendwa sana kurejea tena kwenye muziki kwa kishindo.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Bi. Juliana Shonza aliwakutanisha na uongozi wa Wanene Studios waliokubali kuchukua jukumu la kuwarudisha tena kwenye muziki. Tayari wameanza kuingia studio kuandaa kazi mpya katika studio hizo kubwa na bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Wameanza kwa kufanya photoshoot, kitu ambacho wamekiri kuwa ni kigeni mno kwao kutokana na kuwa gerezani kwa miaka 14 na wametoka katika nyakati ambazo muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa ukilinganisha na zamani.
Tags
Burudani
