humph the GREAT
KAMA ilivyo kwa wanawake
wengi, inapofikia wakati wa hedhi, huwa wanapatwa na maumivu makali sana
ya tumbo, likiwa limezoeleka kama tumbo la uzazi na maumivu haya
huwasababishia kukosa amani kabisa, kuachana na shughuli zao za kikazi,
masomo na mambo mengine mbalimbali lakini kwa bahati nzuri maumivu haya
yanaweza kuzuilika. Lakini kabla hatujatibu tatizo, inabidi tuufahamu mzizi wake kwanza.
CHANZO CHA MAUMIVU YA TUMBO
Maumivu ya tumbo la uzazi (Uterus) hutokana na kukaza na kukakamaa
kwa misuli ya tumbo hilo ili kuwezesha uondoaji wa kuta za tishu zenye
damu zilizojishikiza wakati wa hedhi.
Kitendo hiki huchangiwa na kemikali aina ya homoni zinazoitwa
prostaglandins ambazo ndizo zinahusika na maumivu na kujisikia muwako wa
moto na ndizo huanzisha kusinyaa kwa misuli ya Uterus. Kiwango cha
prostaglandins kinapozidi, ndivyo maumivu yanavyoongezeka zaidi.
Sasa, baada ya kuugundua mzizi wa tatizo, tunaweza kutafuta njia za
kuondokana na tatizo. Kwa maana hiyo, tukiweza kudhibiti kiwango cha
prostaglandins, au kuifanya misuli ya tumbo ilegee badala ya kusinyaa na
kujikaza tutakua tumelidhibiti tatizo. Njia za kufanya kuondokana
maumivu ya tumbo wakati wa hedhi.
FANYA MAZOEZI
Unaweza kulichukulia kama mzaha lakini ni jambo la msingi sana kwa
afya yako, kufanya mazoezi hata ya kutembea umbali flani, kukimbia au
kazi yoyote inayohitaji nguvu, moyo wako husukuma damu nyingi kwa kasi
zaidi katika mwili; hii husaidia kutoa kemikali nyingine inayoitwa
‘Endorhins’ ambayo hufanya kazi kinyume na prostaglandins na kuzuia
makali yake, hivyo kuzuia maumivu ya tumbo na kuurudisha mwili katika
hali ya msawazo wa kawaida.
Jaribu kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki, kama ulikua ukisumbuliwa na maumivu haya, matokeo utayaona.
TIA JOTO KULEGEZA MISULI
Joto husaidia kulegeza misuli ya Uterus iliyojikaza ambayo hasa ndio
chanzo cha maumivu. Kuna vifaa mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya kazi
hii, kama vile ThermaCare na Bengay, ambavyo vinatumika zaidi ya mara
moja.
Lakini kama huwezi kuvipata hivi, usijali, tumia njia za kawaida kama
kuweka maji ya moto ndani ya chupa ya plastiki na kuanza kujikanda nayo
sehemu za tumboni zenye maumivu, itakusaidia.
PATA VITAMIN D
Siku zote kinga ni bora kuliko tiba, hivyo, kwa kuhakikisha unakua na
vitamin D3 (cholecalciferol) muda wote, itakukinga na maumivu haya.
Utafiti uliofanyika kule Italia, imeonekana kuwa wanawake waliopewa
dozi ya kutosha ya vitamin D3, maumivu yao yalipungua kwa asilimia 40.
Vitamini hiyo hupatikana kutoka kwenye jua la asubuhi na kula vyakula
kama maini ya ng’ombe, kiini cha yai na samaki wenye mafuta.
0 Comments