humph the GREAT
BAADA ya Janga la Corona kupungua makali, wasanii nao wanaanza kurudi
kwenye reli tena kama zamani.Kwani wasanii wengi walikuwa wakitoa ngoma
kwa kusuasua sana, wakihofia ngoma zao kutokiki kutokana na janga
hilo.Juni hii tayari zimeruka ngoma kali kali ambazo kwa sasa ndizo
habari ya Mji wa YouTube, kuanzia So Hot ya King Kiba ambayo inakimbiza
na kuwa trending namba moja.
Mwanadada anayetikisa kwenye anga la Bongo Fleva kwa sasa, Faustina
Charles ‘Nandy’, ametisha vibaya mno baada ya kupiga pasi ndefu
alipotoka na ngoma ya Na Nusu, basi ameachia mkwaju mwingine mkali wa
Acha Lizame.
Nandy ameachia ngoma hiyo Juni 12, mwaka huu akiwa na mkali na
Mkurugenzi wa Lebo ya Konde Music WolrdWide, Rajab Abdul ‘Harmonize’.
Ndani ya saa chache tu imetazamwa mara laki nne kuelekea tano na
kukamata trending namba mbili pale mjini YouTube.Mwanzo mashabiki
walianza kuhisi kuna kolabo inakuja kati ya Nandy na Harmonize au Harmo
baada ya kuonekana wakiwa wanachati.
OVER ZE WEEKEND
inakuletea usichokikua juu ya ngoma hii ya Acha Lizame;Kabla ya kutoa
video ya ngoma hiyo, mwanzo Nandy aliipigia promo kwa kuweka cover,
akiwa anawaandaa mashabiki wake wakae mkao wa kula.Nandy amekuwa akitoa
ngoma baada ya ngoma na zote zikiwa kali, hajawahi kushuka kwenye chati
kutokana na bidii na uzuri wa kazi zake.
KOLABO
Tukizungumzia kolabo ya ngoma hii, Nandy na Harmonize ni wasanii
ambao wana fun-base (wafuasi) kubwa na vipaji vikali sana.Kemistri hii
imeweza kutengeneza kitu kikali sana, kwani wote ni wasanii wakali
katika kuimba, kutumbuiza na wana mtandao mkubwa wa mashabiki kila pande
ya Afrika.
Hii ni miongoni mwa kolabo ambazo zitakuwa kubwa sana na zinaweza
kuweka historia kutokana na ukubwa wa majina ya wakali hawa wawili,
kwani wote wana nyota ya kupendwa na mashabiki wa muziki mzuri.Katika
ngoma hii, Harmonize ‘Konde Boy’, amefanya kazi kali sana, kwani
amefanya hata mwenye ngoma hiyo ambaye ni Nandy, kumwachia uwanja jamaa
ili afanye yake.
UTUNZI
Acha Lizame, ni ngoma ambayo imepita katika kalamu za watunzi wakali
ambao wamekuwa wakishiriki katika utunzi wa ngoma za Nandy.Ngoma hii
imeandikwa na J Melody, Logic na Harmonize mwenyewe.Watunzi wawili; J
Melody na Logic, wamekuwa wakihusika sana kwenye uandishi wa ngoma
nyingi za Nandy ambazo zimekuwa zikifanya poa kunako soko la muziki wa
Bongo Fleva.
Mbali na kuandikwa na waandishi hao wakali, pia imepita kwenye mikono
ya producer anayefanya poa sana, Kimambo kutoka Studio za SOV. Mbali na
ngoma hii, pia amehusika katika kutengeneza Ngoma ya Aibu ambayo
ilifanya poa kwa wakati wake.
MAUDHUI
Ngoma hii kila mtu anaitafsiri kiaina yake, kutokana na jina la ngoma
hiyo.Acha Lizame, imezungumzia mapenzi, katika mashairi yake
yamezungumziwa mapenzi.Mwanadada anayemsifia mpenzi wake kwa sifa
kedekede kutokana na mapenzi anayopewa.Hata ukiisikiliza kwenye vesi ya
pili jinsi Harmonize alivyoimba, aisee ni mashairi makali sana na ya
kiufundi zaidi.
UBUNIFU
Video hii imepita kwenye mikono ya Director Elvis kutoka Studio za
Rockshottz ambaye ametengeneza pia So Hot ya King Kiba na Bedroom Remix
ya Harmonize.Nandy amejiachia ile mbaya kwani ameonekana kuwa
comfortable kwa kila kitu, kikubwa ambacho amefanya ni yale mauno ya
hatari ndani ya video hii.
Lokesheni iliyotumika humo ni mazingira ambayo ni sahihi ingawa ni
studio video, lakini kwa namna ambavyo yametengenezwa, imefanya hata
rangi zisimchoshe mtazamaji.Hata ukiangalia kwa upande wa mavazi, Nandy
ameuza mno kwenye mavazi, ila kwa Konde Boy kama kawaida yake lazima
avue shati, hiyo nayo imetosha kunogesha utamu wa video.Miongoni mwa
video kali za mwezi huu, video hii imetisha kwani director wake amefanya
kazi kali. Ubunifu uliotumika ni balaa.
UCHANGAMFU
Ngoma hii imechangamka mno, kiasi kwamba unaweza kuitazama zaidi ya
mara mia moja, ina vibe la kutosha.Wasanii wenyewe wameonesha
kuchangamka katika video jinsi inavyoonekana.Harmonize ameonesha utundu
wake kwenye kuimba, kwani ameimba kwa uhuru sana na kufanya ngoma inoge
japo ameimba viitikio sana.
NANDY AFUNGUKA
Nandy amefunguka sababu ya kufanya kolabo na Harmonize katika ngoma
hiyo, kwa kusema kuwa mapokezi ya ngoma hiyo ni makubwa.“Mapokezi ya
ngoma ni mazuri na makubwa mno, kwani ndani ya muda mfupi imetazamwa na
watu zaidi ya laki nne kuelekea tano. Sababu kubwa ya kufanya kazi na
Harmonize, ni msanii mzuri, haikuwa ngumu kukutana na kufanya naye kazi,
mimi nina desturi ya kufanya kolabo na wasanii tofauti tofauti,”
amesema Nandy.
HITIMISHO
Pongezi nyingi ziende kwa Nandy, kutokana na uzuri wa ngoma hii,
kwani ameweza kuliteka tena soko kama ilivyo kawaida yake.Hakika
hajawahi kukosea, ni msanii wa kike wa Bongo Fleva ambaye anaipeperusha
vilivyo bendera ya Tanzania.
0 Comments