Taifa Stars yaibamiza Zimbabwe


Stars wakishangilia ushindi dhidi ya Zimbabwe.

TIMU ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), imeanza vizuri kampeni za kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), mwakani kwa kuipa kipigo Zimbabwe (Mighty Warriors) bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, jana.
Stars ambayo ipo chini ya kocha mpya, Mart Nooij, raia wa Uholanzi, ilicheza mchezo huo kwa nguvu huku ikifanya mashambulizi mengi licha ya kuwa Zimbabwe ilitoa upinzani mkali.
Akizungumzia mchezo huo mara baada ya kipenga cha mwisho, Nooij alisema ni jambo zuri kushinda nyumbani na kusisitiza kuwa hiyo ni faida kwa Stars. “Tutaenda Zimbabwe kwa lengo moja tu la kusonga mbele,” alisema.
Upande wa Kocha wa Zimbabwe, Ian Gorowa, alisema: “Tumepoteza kwa timu ambayo siyo mbaya lakini kukosekana kwa wachezaji wetu watatu muhimu kumechangia kufungwa.”
Mshambuliaji John Bocco ndiye aliyeanza kuwaamsha Watanzania dakika ya 13 kwa kufunga bao zuri lililotokana na krosi ya chini iliyopigwa na Thomas Ulimwengu kutoka winga ya kulia.
Baada ya hapo mashambulizi yaliendelea kwa kasi, hasa upande wa kulia aliokuwa akicheza Ulimwengu.
Zimbabwe ilirejesha majibu kwa kushambulia mara kadhaa lakini washambuliaji wake walikosa umakini wa kumalizia mipira ya mwisho.
Stars nayo haikuwa nyuma kwani dakika ya 28, Mwinyi Kazimoto alipiga shuti kali ambalo lilipita pembeni kidogo ya lango, lakini dakika ya 31 almanusura Stars wajifunge kutokana na kukosa maelewano mazuri wakati beki Oscar Joshua alipomrudishia mpira kipa wake, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Katika mchezo huo, Stars ilifanya mabadiliko kipindi cha pili muda tofauti kwa kuwatoa Frank Domayo, Mrisho Ngassa na John Bocco kisha nafasi zao zikachukuliwa na Amri Kiemba, Haruna Chanongo, Ngassa na Hamis Mcha.
Katika mchezo huo, Milton Nkube na Steven Almenda wa Zimbabwe walizawadiwa kadi za njano kwa kucheza vibaya.
Baada ya mchezo huo, mbunge Zitto Kabwe alimsifia Shomari Kapombe kwa kuonyesha kiwango kizuri. “Kwangu Kapombe ndiye nyota wa mchezo, amecheza vizuri licha ya kuwa hana timu lakini wachezaji wote kwa jumla wamecheza vizuri,” alisema Zitto.
Kikosi cha Stars kilichoanza: Dida, Kapombe, Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Domayo, Ngassa, Kazimoto, Bocco, Mbwana Samatta na Ulimwengu.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post