Kumbe! Siri imefichuka sababu ya malori ya mizigo na mafuta kuungua moto baada ya jeshi la polisi mkoani hapa kuwashikilia watu sita akiwemo dereva na utingo wa lori aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Dandu wakidaiwa kuchoma moto lori hilo. Ilidaiwa kwamba jamaa hao wakazi wa Mbeya walifanya hivyo baada ya kutaifisha mzigo wa mitumba na viatu wenye thamani ya shilingi milioni 100 waliokuwa wakiusafirisha kwenye lori hilo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ilidaiwa kuwa wawili hao walifanya njama ya kulichoma moto lori hilo baada ya kushusha mzigo huo na kuuhifadhi kwenye Kijiji cha Maguhani Mufindi ili kuuuza kutokana na dereva wa lori hilo kudaiwa kodi ya shilingi laki 4 na baba mwenye nyumba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Ramadhan Mungi alisema watu sita wanashikiliwa na jeshi hilo wakihusishwa na tukio hilo na kuwa lori hilo lilikuwa na mzigo wenye thamani ya shilingi milioni 100.
Mungi alisema kuwa, polisi wakiwa doria katika maeneo ya Mafinga wilayani Mufindi walikuta lori likiungua bila kuwepo kwa dereva wala utingo.
Baada ya uchunguzi walimbaini dereva wa lori hilo alijulikana kwa jina moja la Elia (26) na utingo wake, Deusi (20).
Alisema kuwa watuhumiwa hao waliwasha moto lori hilo baada ya kushusha kwa magendo mzigo huo wa mitumba kwa mtu aliyetajwa kwa jina moja la Agrey.
0 Comments