humph the GREAT
MAELFU ya
mashabiki wa Muziki wa Kizazi Kipya nchini walikuwa wameelekeza macho na
masikio yao katika Ukumbi wa Barcklays Center pale New York, Marekani
kwenye utoaji wa tuzo za BET, ambako Mtanzania Diamond Platnumz alikuwa
mmoja wa wasanii saba kutoka Afrika waliokuwa wakishindana kuwania
kipengele cha Best Internatinal Act 2016 (Africa).
Wakitaraji kuwa mwakilishi wao huyo
angeibuka kinara, ghafla ikatangazwa kuwa DJ Black Coffee kutoka Afrika
Kusini, ndiye mshindi na hivyo kufuta ndoto za Diamond kutwaa tuzo
katika ardhi ya Marekani. Mshindi huyu ni nani?
Jina lake linaweza kuwa geni kwa baadhi,
lakini kwa wafuatiliaji wa burudani watakuwa wanamfahamu vyema mkali
huyu wa miondoko ya House ambaye pia ni prodyuza hasa kupitia ngoma yake
iitwayo Juju, iliyofanya vizuri sana barani Afrika miaka ya hivi
karibuni.
Ni mzaliwa wa jijini Durban akiitwa
Nkosinathi Innocent Maphumulo, lakini alipogusa tu ulimwengu wa
‘entertainment’ mwanzoni mwa miaka ya 1990, akajiita DJ Black Coffee.
Ameanzia wapi muziki?
Dj Black Coffee kabla ya kuufanya muziki
kuwa biashara ya kumuingizia mkwanja, alikuwa ni mwanakwaya katika
shule yake ya sekondari, baadaye alikwenda kusomea muziki katika chuo
kiitwacho Natal Technikon na kabla ya kumaliza masomo, alianzisha bendi
iitwayo Shana (Simply Hot And Naturally African).
Akiwa ameanza kuvuna mashabiki kutokana
na kazi yake ya muziki, mwaka 2003 mkali huyo alikuwa mmoja kati ya
wanamuziki wawili wa Afrika Kusini waliochaguliwa na kituo cha
kujifunzia muziki kiitwacho The Red Bull Music Academy kuwa Dj wake,
ambapo huo ndiyo ukawa mwanzo wa kujipatia umaarufu kupitia muziki na
u-dj.
Mpaka sasa amefanikiwa kutoa albamu sita
ambazo ni Black Coffee (2005), Have Another One (2007), Home Brewed
(2009), Africa Rising DVD (2012), Africa Rising CD (2012) pamoja na
Pieces Af Me ya mwaka 2015 na albamu zote hizo zimefanya vizuri kimauzo.
Tofauti yake na wasanii wengine
Moja ya vitu vilivyompa umaarufu mkali
huyu na kumtofautisha na wasanii wengi ni uwezo wake wa kucheza na
vyombo vya muziki kwa kutumia mkono wake mmoja tu wa kushoto kwani akiwa
na miaka 13 alipoteza matumizi ya mkono wake wa kulia baada ya kupata
ajali ya kugongwa na gari katika sherehe za kuachiwa huru kwa hayati
Nelson Mandela.
Mwaka 2010 alivunja rekodi ya dunia kwa
kuwa Dj mwenye uwezo wa kuburudisha kwa muda mrefu akitumia mkono mmoja
tu. Anatajwa pia kuwa ni mmoja kati ya wasanii wanaopendwa mno Afrika
Kusini, hasa kwa msaada wake kwa jamii ikikumbukwa mwaka 2009, aligawa
asilimia tano ya mauzo ya albamu zake zote kwa makundi maalumu yenye
uhitaji.
Ukongwe umempiga tafu!
Katika orodha ya wasanii waliokuwa
wanachuana kuwania tuzo ya BET katika kipengele cha Best International
Act 2106 (Africa) ambao ni Wizkid, AKA, Diamond Platnumz, Cassper
Nyovest, Yemi Alade na Serge Beynaud, ni DJ Black Coffee pekee ambaye ni
mkongwe kuliko wote na mwenye mafanikio kwenye tasnia ya muziki.
Tuzo ya mwaka huu kwake ni ya 16 ikiwemo ile ya Channel O aliyobeba mwaka 2011 ya msanii mwenye kipaji zaidi kuliko wote Afrika.
Kuhusu familia
Mwaka 2011 alifunga ndoa na muigizaji
mwenye jina kubwa Afrika Kusini, Mbali Mlotswa na wamefanikiwa kupata
watoto wawili, Anesu na Asante lakini kabla ya hapo, DJ Black Coffee
alikuwa na watoto wengine wawili aliowapa katika uhusiano wake wa nje
ambao ni Esona na Lilitha.
Tags
Burudani