humph the GREAT
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KOCHA mpya wa Simba ni Sellas Tetteh Teivi, raia wa Ghana, pia ni mmoja wa makocha maarufu barani Afrika.
Kwa sasa kocha huyo gwiji barani Afrika,
ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya Sierra Leone na Simba imefanya
mazungumzo naye kwa takriban wiki nzima, imefahamika.
Tayari Simba imetenga dau, tayari
imefanya mazungumzo naye na yenyewe imeshakubali kila kitu, kilichokuwa
kinasubiriwa ni kitu kimoja tu, neno “Yes” kutoka kwa Tetteh.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa timu ya
taifa ya Ghana, ni maarufu kutokana na mambo kadhaa likiwemo lile la
kuiongoza timu ya vijana wa Ghana chini ya miaka 23 kucheza Kombe la
Dunia mwaka 2013.
Pia aliwahi kuwa kocha wa muda wa timu
kubwa ya taifa ya Ghana na wakati akiwa mwanasoka, alicheza kwa
mafanikio katika klabu za Great Mao Mao, Zebi na Hearts of Oak kwao
Ghana, pia nchini Nigeria alipozitumikia ACB, Julius Bereger na
Iwuanyanwu.
Habari za uhakika kutoka nchini Ghana kwa rafiki wa karibu wa kocha huyo, zimethibitisha Simba kufanya naye mazungumzo.
“Mazungumzo yao yamefikia pazuri sana,
kocha alichelewa kutoka Sierra Leone ndiyo ikawa shida. Lakini leo
(jana) atawapa Simba jibu rasmi, mwanzo alitaka kuona ‘profile’ ya
Simba.
“Simba wenyewe wamemwambia wanasubiri na leo (jana) ni mwisho, la sivyo wataendelea na plani nyingine,” kilieleza chanzo.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe kuhusiana na hilo, alionekana kuwa mkali hiyo jana.
“Nafikiri si sahihi kusema vitu
nusunusu, tuacheni tumalize kama kweli ni huyo au mwingine mtajua.
Sipendi kuzungumzia vitu nusunusu,” alisema Hans Poppe ambaye amekuwa
akipambana kuhakikisha Simba inarejea kwenye fomu. Iwapo Tetteh
atachelewa, uhakika kabisa Simba itaenda kwenye mpango C kumyakua kocha
wa zamani wa Azam FC, Joseph Omog raia wa Cameroon. Mpango A ulikuwa ni
Kocha Kallisto Pasuwa wa Zimbabwe ambaye amesitisha kuja baada ya timu
yake kufuzu Caf.
Tags
Michezo na burudani