humph the GREAT
MUZIKI ni lugha inayowaunganisha
watu wengi, wala haujalishi tofauti za kidini, kikabila, wala kitaifa,
muziki huwaweka watu pamoja na kuwafanya kuwa kitu kimoja.
Ndiyo maana leo Afrika Mashariki
tunaweza kuzungumza muziki wa sehemu zingine ikiwemo Afrika Magharibi
ambako miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri huko ukiachana na kina
Wizkid, Patoranking, P Square na wengine wengi ni Deborah Oluwaseyi
Joshua ‘Seyi Shay’.
Huyu ni mwanadada aliyezaliwa nchini
Uingereza kwa wazazi wa Kinigeria, baba yake akitokea kwenye Kabila la
Ife huku mama yake akitokea kasikazini mwa nchi hiyo. Katika ‘exclusive’
interview’ na
RisasiJumamosi, Seyi Shay amefunguka mengi kuhusu kazi yake ya muziki!
Risasi Jumamosi: Stori
inayo-trend kwa sasa ni juu ya bifu lako na Tiwa Savage, unaweza kueleza
nini sababu ya tofauti zenu na uhusiano wenu kwa sasa?
Seyi Shay: Siwezi kuzungumza lolote lile juu ya hilo suala.
Risasi Jumamosi: Sawa,
umefanya kazi na kupafomu na wasanii wengi wa kimataifa, miongoni mwao
ni Kelly Rowland na Wale, kuna mipango yoyote ya kolabo na wasanii hao?
Seyi Shay: Ndiyo,
mipango ya kufanya kolabo za kimataifa ipo, lebo yangu iliyopo Uingereza
iitwayo Island Records inalifanyia kazi hilo. Lakini mimi mwenyewe
ninafanya kazi na wasanii wa kimataifa Afrika kwa sasa wakiwemo kutoka
Tanzania.
christian bella, mzee wa masauti kutoka tanzania
Risasi Jumamosi: Kuwa na uraia Uingereza kunakusaidia vipi kimuziki?
Seyi Shay: Hakuna
msaada zaidi ya kuingia Ulaya bure na labda kusaini kwenye lebo kubwa
Uingereza. Mafanikio mengine Afrika ni kukomaa kwangu mwenyewe.
Risasi Jumamosi: Ni wimbo gani ambao umekupa mafanikio makubwa kimuziki na kivipi?
Seyi Shay: Wimbo wa Right Now, ulikuwa mkubwa sana, umefika mbali na umenitambulisha vyema kwenye Tasnia ya Muziki Duniani.
Risasi Jumamosi: Mpaka sasa umefanikiwa kupata tuzo ngapi?
Seyi Shay: Kumi na moja.
Risasi Jumamosi: Nani msanii wako bora Nigeria na kwa nini yeye?
Seyi Shay: Wapo wengi
na siwezi kutaja mmoja. Kuna Sultan. Ana kipaji sana tofauti na wasanii
wengi ninaowafahamu. Nampenda pia Wizkid kutokana na kufanya kazi kwake
kwa juhudi pia tunapigana tafu, 2 Face naye ana muziki mzuri.
Risasi Jumamosi: Unaweza kuzungumza lolote lile kuhusu Tasnia ya Muziki Afrika Mashariki? Ni msanii gani unayemkubali?
Seyi Shay: Tasnia ya
Muziki Afrika Mashariki inakua, napenda wanachokifanya. Nilipotembelea
Tanzania miaka michache iliyopita nilijifunza mengi na kufahamu nini
kinaendelea huko, niko katika mipango ya kufanya kazi na wasanii wa huko
pia nafagilia sana swaga za Christian Bella.
Risasi Jumamosi: Kuna kampuni yoyote ambayo imekupa shavu kwa sasa la ubalozi?
Seyi Shay: Ndiyo, mimi ni Balozi wa Etisalat, Pepsi na mtandao wa simu uitwao Telecoms.
Risasi Jumamosi: Tofauti na muziki kuna biashara nyingine ambazo unajishughulisha nazo?
Seyi Shay: Yap, pia
jambo kubwa ninatarajia kutambulisha kwenye tasnia ya urembo hivi
karibuni ni nywele za bandia (wig), ninafikiri itakuwa mwishoni mwa
mwaka huu.
Risasi Jumamosi: Kuna kazi yoyote ambayo iko mbioni kutoka kwa sasa?
Seyi Shay: Ndiyo, ninamalizia kushughulikia video ya wimbo wangu uitwao Seyi Or Shay, unaobeba jina la albamu yangu mpya.
Risasi Jumamosi: Jambo lingine ambalo mashabiki wa muziki watafurahi kufahamu ni kuhusu maisha yako ya uhusiano, wafahamishe lolote.
Seyi Shay: Oke, niko katika uhusiano wenye furaha na mpenzi wangu hayuko kwenye tasnia kabisa. Namaanisha ya muziki.
Risasi Jumamosi: Pamoja sana Seyi Shay, labda kama una lolote kwa mashabiki wa kazi zako.
Seyi Shay: Ninawashukuru kwa kuniunga mkono, niwasiliane nao kupitia Snap Chat, Ig na Twitter @iamseyishay.