humph the GREAT
Rais Dk. John Magufuli.
NCHI ilimaliza uchaguzi miezi saba
iliyopita na sasa ipo katika mwendo wa kawaida kuhakikisha maisha ya
Watanzania yanabadilika. Malumbano ya kisiasa ambayo yalikuwa ya kiwango
cha juu kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya taifa hili,
yalimalizika mara tu baada ya kuapishwa kwa Rais Dk. John Magufuli pale
Novemba 5, 2015.
Siku chache tu baada ya Magufuli kuanza
kazi, wazalendo wa kweli wa nchi hii walisahau tofauti zao kisiasa,
wakaungana pamoja baada ya kiongozi huyo kuonesha kuwa ni mtu
aliyejitolea kwa dhati ili kuwatumikia watu wote, hasa wanyonge.
Vitu alivyovifanya, vilisababisha aungwe
mkono hata na watu ambao miezi michache nyuma walimuona adui na ambaye
asingebadili lolote, hasa kwa kuwa wengi wanaamini chama tawala, CCM,
kimekosa mbinu za kuinua hali ya maisha ya Watanzania ambao licha ya
nchi yao kuwa na maliasili nyingi, lakini wanaishi maisha mabovu.
Uzalendo wake, chuki zake za wazi dhidi
ya wabadhirifu, kudhibiti matumizi yasiyo na tija, mafisadi na
uwajibikaji katika utumishi wa umma, ni vitu ambavyo vimemfanya kuwa
nuru katikati ya giza nene ambalo lilikuwa limewagubika Watanzania ambao
walifikia kipindi cha kuamini kuwa kama ataendelea na moto huo,
uchaguzi ujao utakuwa rahisi mno kwa CCM kuliko wakati mwingine wowote
tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi.
Lakini katikati ya mazuri haya, kuna
mambo machache yanayofanyika, yanayoonesha kuwa mbele ya safari,
kutatokea matatizo kama yasipodhibitiwa mapema.
Kuna kauli za viongozi zinazoonesha kuwa
siasa zimekwisha, kilichobakia hivi sasa ni kazi tu. Ni jambo jema,
kwamba tuache blahblah, tupige kazi. Kama ni hivyo, tunapozuia mikutano
au mikusanyiko, tufanye hivyo kwa haki.
Haileti picha nzuri, mikutano na
mikusanyiko inayolengwa ni ile ya wapinzani pekee, wakati hata wale wa
chama tawala nao wanafanya. Maisha ni siasa, hauwezi kuvitenganisha hivi
vitu.
Unapomzuia mwanasiasa kukutana na watu,
maana yake hana sababu ya kuwepo. Inanikumbusha wakati f’lani Augustine
Mrema alipokuwa akibebwa na wananchi kila alipoonekana, kutokana na wao
kuwa na ‘mahaba’ naye.
Jambo lile lilionekana kuwakera wakubwa,
wakampiga marufuku kubebwa, kana kwamba yeye alikuwa anaandaa watu ili
wambebe. Lakini busara za Mwalimu Nyerere ndizo zilizomnusuru akaendelea
kubebwa hadi wabebaji walipokuja kumshtukia, baada ya kuwataka polisi
wamuache abebwe kama maiti.
Tunapozuia mikusanyiko ya wapinzani,
tunatengeneza tatizo. Ni sawa na kujaribu kuyazuia maji katika mkondo
wake, mwishowe yatasababisha mafuriko yanayoweza kuwa na hasara kubwa
zaidi kuliko kuyaacha yapite katika njia yake ya kawaida.
Tusiwape wapinzani sababu ya kutafuta
njia mbadala ya kukutana na watu wao, ambayo kwa vyovyote itakuwa haina
afya kwa taifa. Tuwaache wakusanyike, waongee ilimradi wasivunje sheria
tulizokubaliana. Ni wananchi ndiyo wataamua, kama wanachoambiwa kiko
sawa au la, vinginevyo mikusanyiko hiyo itakufa yenyewe kifo cha
kawaida.
Tags
HABARI