Alliance yaangusha kipigo kwa Warundi

humph the GREAT
TIMU ya soka ya Alliance Fc ya mkoani hapa juzi imetoa kipigo kikali cha mabao 5-1 kwa timu ya Aigle Noir kutoka Burundi katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye viwanja vya shule ya Alliance.
Mabao ya Alliance Fc yalifungwa na Juhudi Philemon katika dakika ya 19 aliyefunga bao la kwanza na bao la pili likifungwa na Ismail Zuma katika dakika ya 55 na mabao mengine yalifungwa na Athnas Mdamu katika dakika ya 67,77 na 89 huku bao la kufuta machozi la Aigle Noir likifungwa na Biziman Kuban katika dakika ya 19.
Kocha mkuu wa Aigle Noir, Ndikumana John alisema baada ya hiyo kuwa timu yake imepoteza mchezo huo kutoka na uchovu wa safari ndefu kutoka Burundi mpaka Mwanza, Tanzania. “Uchovu wa safari umepelekea sana kupoteza mchezo huu wa leo (juzi) ambapo na mpaka kufika kucheza na Alliance tulicheza na Mwadui fc ambapo pia tulipoteza,” alisema.
Ndikumana ameipongeza timu ya Alliance Fc kwa ushindi na kusema inaonekana ni timu iliyokaa muda mrefu na wachezaji wake ni wadogo na wanacheza kwa kujituma.
Ndikumana alisema lengo lao kubwa kuja Tanzania ni kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki dhidi ya Alliance fc,Mwadui fc na Mbao fc ikiwa ni moja ya mikakati yao ya kujiandaa na Ligi Kuu ya Burundi inayotarajiwa kuanza Septemba mwaka huu.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha msaidizi wa Alliance Mathias Wandiba alisema vijana wake wamecheza kwa kujituma sana ndio kilichopelekea kushinda mchezo wao dhidi ya Aigle Noir.
“Vijana wamecheza vizuri sana na wameweza kufuata maelekezo yangu na kiukweli tuliweza kutawala dakika zote za mchezo kiukweli timu inacheza vizuri sana kadiri siku inavyozidi kwenda,” alisemaWandiba.
Alisema, timu hiyo Agosti 20 mwaka huu itaelekea Kenya kwa ajili ya kucheza mashindano ya umoja wa shule za sekondari za Afrika mashariki na kati (FEASSA).

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post