humph the GREAT
Rais John Magufuli angalau amefanya jambo la ujasiri,haya yalimshinda
Rais wa awamu ya nne Mh Jakaya Kikwete ambaye pamoja na kuunda kamati
mbili,ile ya Jaji Mark Bomani na ile ya Laurence Masha, baada ya
kumaliza kazi ziliwekwa kabatini!.
Kuiweka wazi Ripoti ya Prof Mruma ili watanzania wajue angalau
kinachoendelea kwenye mgodi wa Kahama,kumeibua angalau hasira kidogo kwa
watanzania,moja ya madhaifu ya watanzania wengi huwa hawakasiriki hata
pale wanaponyonywa,wanapoibiwa tena waziwazi!.
Madhaifu makubwa ya watanzania ni upole na unyonge hata pale
wanapotendewa mambo ya hovyo,wanaoonyanyaswa,miaka yote wakazi wa
Geita,Kahama,Nzega,Tarime,Biharamulo wameishia kitazama tu mali zao
zikipanda ndege na kwenda Ulaya,Asia na Marekani!.
Angalau Mrehemu Chacha Wangwe aliyekuwa mbunge wa Tarime alivishinda kwa
kiasi chake vita hivi,Wangwe alihakikisha wana wa Tarime wanapata
angalau kiasi kidogo,alisimama kidete kuhakikisha kila mkazi wa vijiji
vinavyozunguka mgodi wa North Mara wanapata karo ya shule/Chuo kama
sehemu ya kufaidi utajiri wao!.
Angalau Tundu Lissu wakati hata akiwa hajawa mbunge alizunguka kuanzia
Kahama mpaka Nyamongo akitoa msaada wa kisheria kwa walioitwa wavamizi
wa mgodini,nakumbuka akiwa na shirika la wanasheria watetezi wa masuala
ya mazingira walitoa masaada wa bure kwa waliokamatwa kwa kudaiwa
kuvamia mgodi!.
Nakumbuka jinsi Lissu alivyokumbana na kesi ya uchochezi pale alipopaza
sauti baada ya kuwepo kwa taarifa za watu kufukiwa huko kwenye mgozi wa
dhahabu wa Bulyanhulu!.
Angalau wewe Lissu uliuweka uwoga pembeni ukaandika kitabu kwa
kushirikiana na Mark Curtus mlichokipa jina la "The golden
opportunity"kitabu mlichokiandika kwa lugha ya kiswahili na
kingereza,kitabu hiki kimeleza kinagaubaga jinsi tunavyoibiwa!.Kama
serikali ingeamua kukifanyia kazi kitabu hiki,tusingefika hapa leo!.
Angalau Comrade/wakunyumba Hamis Kigwangala wakati fulani alisimama
kidete kupinga wana wa Nzega kuishi maisha ya ufukara wakati Mungu
kawajalia dhahabu,ndugu yangu huyu nakumbuka alivyojikuta mikononi mwa
polisi!.
Niliwahi msikia Augustino Mrema akizunguka nchi nzima akiwatuhumu
Ashanti Gold mine kuwa walimhonga kiongozi wa juu wa serikali ya awamu
ya tatu,angalau ulipaza sauti kulikemea hili!.
Angalau Zitto Kabwe ulisimama kidete kuusaka ukweli ndani ya bunge mwaka
2007,juu ya waziri wa kipindi hicho Nazir Karamagi kwenda Uingereza na
kusaini mkataba kati ya Tanzania na Barrick ili wachimbe madini Buzwagi!
Angalau Marehemu Dr Sengondo Mvungi ulipinga bila woga kwenye maandiko
na hata ulipoalikwa kwenye vyombo vya habari kiongozi mkuu wa nchi
kujiuzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwila tena kwa bei ya kaptula!
Angalau aliyepata kuwa mbunge Mh Kimaro yeye alipambana bungenu na Mzee
Sitta kupaza sauti kupinga kiongozi wa juu kabisa kujiuzia mgodi,kelele
hizi zilioazwa sana na Dr Wilbroad Slaa kila akisimama bungeni alikuwa
mwiba kuhusu mgodi wa Kiwila,nakumbuka sauti zenu zilizaa matunda mpaka
serikali ikatangaza kuurejesha mgodi ule serikalini!.
Angalau kamati ya viongozi wa dini ya haki na amani,mlitimiza wajibu
wenu,amlizunguka nchi nzima mkiongozwa na akina Askofu Mkuu Paul
Ruzoka,Shehe Fereji na maaskofu wengine na mashehe,nakumbuka jinsi
mlivyozuiliwa kuingia kwenye mgodi wa Geita bila kujali nafasi zenu
kwenye jamii,jinsi mlivyotafuta ukweli wa kilichoitwa sumu za mto
Tigithe huko Mkoani Mara.
Ripoti yenu ambayo hata mimi mlinioatia imethibitisha kuwa majinya mto
tigite yalikuwa na sumu kutoka mgodini,watu waliyatumia
wakafa,wakababuka,lakini mgodi ukaishia kuwaita wavamizi,watumishi wa
Mungu mmeacha alama kwenye utetezi wenu dhidi ya wizi huu!.
Mh Rais Magufuli akiongea kwa uchungu mara baada ya kukabidhiwa ripoti na Prof Mruma,na alichukua hatua pale pale!.
Mh Rais geukia sasa upande wa sheria zako,hawa wakezaji muda wote huo
wamekuwa wanafanya biashara halali ya kinyonyaji,serikali ya awamu ya
tatu iliasisi huu ukwapuaji wa madini yetu!.
Tarehe 26.3.1997,serikali ilipeleka mapendekezo ya miswada miwili ya
sheria,ile ya kodi na ile ya uwekezaji,ikiwa ni kipindi kifupi toka sera
ya madini itungwe mwaka 1997.
Serikali ya Mkapa ilikuja na sera za kuwakaribisha wawekezaji na kuvutia
mitaji kutoka nje(FDI),ikatunga sheria laini kwa wawekezaji,ikiwapa
kipindi kirefu cha kuchota bila kulipa kodi,na hata walipoanza kulipa
kodi walilipa kiduchu!.
Haya unayoyalilia Mhe Rais Magufuli ni matokeo ya watanzania kuwa na
tabia za kutokasirika hata wanaponyonywa,haya ni matokeo ya wataalamu wa
serikali ya awamu ya tatu ya mzee mkala,wabunge wa bunge ya Mzee
Msekwa,baraza ka mawaziri la Mzee Mkapa kutuletea na kupitisha kwa hati
ya dharua sheria mbili za kodi na ile ya uwekezaji!.
Mh Rais sasa badili sheria,waandae wataalamu wako wa sheria,zungumza nao
ujue katika hili taifa litanasuka vipi na unyonyaji huu uliotengenezwa
na sheria zetu wenyewe!.
Mh Rais bunge ambalo na wewe ulikuwa sehemu yake,miaka kumi iliyopita
liliitaka serikali iipeleke bungeni ripoti ya ukaguzi kwenye sekta ya
madini kutoka kutoka kampuni kutoka Marekani ya Alex Stewart
Assayers(ASA report).
Nakumbuka ASA baada ya kukamilisha ukaguzi wao,walizungukza na waandishi
wa habari,mbaya zaidi hawakusema jambo,walipoambiwa waseme wamebaini
nini?jibu likawa,"Kazi tukiyotumwa na serikali imekamilika,hatuwezi sema
chochote kwa sababu tunafungwa na sheria za ukaguzi za
kimataifa",alisema Alex mbele ya waandishi wa habari jijiji Dsm!
Mh Rais mwaka 2007,Kuliibuka sakata la mkataba wa serikali na kampuni ya
madini ya Barrick kutoka Canada juu ya uchimbaji wa madini huko
Buzwagi,nakumbuka wewe ulikuwa naibu waziri,waziri wa nishati na madini
Ndugu Nazir Karamagi alituhumiwa kusaini mkataba mbovu tena
hotelini,bunge lilipoudai mkataba huo,liliambiwa mkataba ni siri,si
media wala wabunge wamewahi uona mkataba huo,ni mkataba wa Buzwagi pekee
ndiyo baadhi nasikia waliwahi uona baada ya kuvuja!.
Mh Rais badili sheria,ondoa kipengere cha usiri kwenye mikataba hii ya
madini na maeneo mengine,ruhusi wananchi kupitia bunge wajadili mikataba
hii inayowahusu!.
Na ndiyo maana ya utawala bora wenye dhana kama,uwajibikaji,utawala wa sheria,uwazi,haki za binadamu,n.k.
Ripoti ya Prof Mruma imetupa picha kiduchu cha tatizo kwenye sekta ya
madini,hatujajua tunachopoteza Geita,kwenye mgodi mkubwa barabj
Afrika,ripoti ya Prof Mruma haijagusa Geita,ripoti hii imepapasa tu
kuhusu uhalisia kwenye sekta ya madini!.
Rais badili sheria ili unasuke katika mapambano haya,tunapambana na wizi
,kilio cha muda mrefu,ni sisi hawa hawa tuliojigunga kupitia sheria ya
kodi na na ile ya uwekezaji zilizopitishwa kwa mbwembwe kwa hati ya
dharura na kutusababishia umasikini,badili sheria Mh Rais tuwabane
wawekezaji,ruhusu uwazi,hii ni biashara halali ya kinyama,iliyoruhusiwa
na serikali na bunge letu huko nyuma!.
Katika vita hii dhidi ya mali zetu wenyewe,tujilaumu wenyewe,tulitunga
sheria mbovu wenyewe,tukazipigia debe wenyewe,zimetifanya masikini,ni
wakati wa wanasheria wetu kutuonesha tunapita wapi ili tutoke salama!.
Kumbuka hii ni vita na mabeberu,ukitaka kujua nguvu ya hawa
mabwana,fanya utafiti juunya akina nani wanaunda Geopolitics department
ya kampuni la GGM!.
Tuwaruhusu wanasheria waoneshe njia,wataalam wa miamba wameshaonesha
udhaifu,wasikilizeni sasa magwiji wa sheria,tupo katika kipindi kigumu!.
Tags
HABARI