humph the GREAT
MGAWO waliopata wabunge, maofisa wa serikali na viongozi wa dini kutoka
kwa watuhumiwa wakuu wa kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya akaunti ya
Tegeta Escrow unatosha bajeti ya mwaka mzima ya miradi ya maendeleo ya
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nipashe imegundua.
Katika miaka mitatu iliyopita ya bajeti (2014/15, 2015/16 na 2016/17),
wizara hiyo ambayo kwa sasa iko chini ya Waziri Dk. Harrison Mwakyembe,
ilitengewa bajeti ya Sh. bilioni tatu kila mwaka, ikiongoza wizara zote
18 kwa kuwa na bajeti ndogo zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Wakati wizara hiyo ikiambulia Sh. bilioni moja (theluthi ya bajeti yake
ya maendeleo) hadi inapofika robo tatu ya mwaka wa bajeti katika miaka
hiyo mitatu, imebainika Sh. bilioni 4.77 zinazodaiwa zao la kashfa ya
uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow walizopatiwa wabunge,
maofisa wa serikali viongozi hao wa dini zingelitosha kugharamia
kikamilifu miradi ya maendeleo ya wizara hiyo kwa mwaka mzima na
'chenji' ya Sh. bilioni 1.7 ikabaki.
Katika mwaka uliopita wa fedha, kwa mfano, kati ya Sh. bilioni tatu
zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara
hiyo, ni Sh. bilioni 1.19 tu (asilimia 40) ndizo zilizokuwa zimetolewa
hadi Aprili 30, mwaka huu kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe.
Kiasi hicho cha fedha hakifikii hata mgawo waliopata Mwanasheria Mkuu wa
Serikali wa zamani, Andrew Chenge na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi wa zamani, Prof. Anna Tibaijuka kwenye mgawo huo
unatokana na uchotwaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow mwaka 2014.
Wawili hao waliripotiwa kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kila mmoja.
Miradi ya maendeleo ambayo Wizara ya Habari ilipanga kutekeleza mwaka
uliopita wa fedha ni Programu ya Urithi na Ukombozi wa Bara la Afrika
ambayo hadi Aprili 30, mwaka huu, ulikuwa umepokea Sh. milioni 30.324
badala ya Sh. milioni 700 na mradi wa Ujenzi wa Ukumbi wa Wazi wa
Maonyesho ya Sanaa ambao ulikuwa haujapokea hata senti licha ya
kuidhinishiwa na Bunge Sh. milioni 800.
Miradi mingine ni Ukarabati wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo uliokuwa
umeidhinishiwa Sh. milioni 300, lakini hadi Aprili 30, mwaka huu,
ulikuwa umepokea Sh. milioni 100 na Ujenzi wa eneo la Changamani la
Michezo uliopokea Sh. milioni 60 kati ya milioni 100 zilizoidhinishwa na
Bunge.
Miradi mingine ya maendeleo ya wizara hiyo iliyopaswa kutekelezwa mwaka
jana ni Habari kwa Umma ulioidhinishiwa Sh. milioni 100, lakini
haukupatiwa hata senti na mradi wa Upanuzi wa Usikivu TBC ambao
ulipatiwa fedha zote, Sh. bilioni moja zilizoidhinishwa.
ILIANIKA MAJINA
Mgawo wa fedha za akaunti hiyo pia ni karibu nusu ya fedha ambazo
serikali imetumia kufanya ukarabati wa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es
Salaam. Uwanja huo umekarabatiwa na Kampuni ya Beijing Construction ya
China kwa gharama ya Sh. bilioni 10.
Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwenye kikao cha 18 cha Bunge la 10,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilianika majina ya
maofisa wa serikali, wabunge na viongozi wa dini waliopata mgawo wa
fedha zinazohusishwa na kashfa hiyo.
Watu hao walipewa fedha hizo na Mkurugenzi wa VIP Engineering na mmiliki mwenza kwa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.
Mkurugenzi huyo na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Power African Power
(T) Limited (PAP), Seth Sigh wako mahabusu kwenye Gereza la Keko jijini
baada ya kukosa dhamana walipofikishwa mahakamani na Takukuru mwanzoni
mwa mwezi wakikabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo ya kugushi, utakatishaji
fedha na kusababisha hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 na Sh
bilioni 309.4 kwa serikali.
Mbali na Chenge na Prof. Tibaijuka, wengine waliopata mgawo huo ni ofisa
katika Ofisi ya Rais wakati huo, Shabani Ngurumo aliyepewa Sh. milioni
80, Jaji wa Mahakama Kuu aliyejiuzulu, Eudes Ruhangisa Sh. milioni
404.25, aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco),
Dk. Enos Bukuku Sh. milioni 161.7 na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja (CCM), ambaye Jumatatu iliyopita alirejesha serikalini Sh.
milioni 40.4 alizopewa.
Katika ripoti hiyo Waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, Mbunge wa zamani wa Sumbawanga
Mjini, Paul Kimiti, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC),
Emmanuel Ole Naiko na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Aloisius Mujulizi
walitajwa kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.
Wengine ni ofisa wa TRA, Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa
Mkurugenzi wa Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita),
Philip Saliboko Sh. milioni 40.2, maaskofu Methodius Kilaini Sh. milioni
80.9 na Eusebius Nzingirwa Sh. milioni 40.4, Padri Alphonce Twimannye
Sh. milioni 40.4, maofisa wa Rita Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na
Theophil Rugozobwa Sh. milioni 323.4.
Tags
Je wajua ?