humph the GREAT
MSHAMBULIAJI tegemeo wa Yanga, Ibrahim Ajibu ametoa kauli ambayo
inaweza kutafsiriwa kuwa ni kama ‘anamzuga’ mpachika mabao wa Simba,
Emmanuel Okwi.
Ajibu amedai kuwa yeye hana mpango wa kuwemo katika orodha ya
wachezaji wanaowania Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kauli hiyo, imetolewa na Ajibu muda mfupi baada ya kuifungia timu
yake bao kisha kumpa asisti Mzambia, Obrey Chirwa katika mchezo wa ligi
hiyo dhidi ya Kagera Sugar, Jumamosi iliyopita.
Mshambuliaji huyo alitua kuichezea Yanga kwenye msimu huu wa ligi
kuu akitokea Simba kwa dau la shilingi milioni 50 mara baada ya mkataba
wake wa miaka mitatu kumalizika.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ajibu alisema yeye
anachokiangalia hivi sasa ni kuifungia timu yake mabao ili wapate pointi
tatu kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya ubingwa.
Ajibu alisema, pointi tatu ndiyo muhimu ambazo ameahidi kuendelea
kufunga na kutengeneza nafasi za mabao kwa wachezaji wenzake ili
wafanikishe malengo yao kama timu waliyojiwekea.
Aliongeza kuwa, yeye ataendelea kufunga mabao kama kawaida lakini
kama ikitokea mwishoni mwa msimu ligi kuu ikamalizika na yeye akawa
mfungaji bora, basi atashukuru kwani haikuwa mipango.
“Niseme kuwa, mimi sifungi mabao ili niwe mfungaji, lakini ninafunga
mabao ili niiwezeshe timu yangu ushindi na mwisho wa mechi tuchukue
pointi tatu.
“Kwani nimesikia tetesi kuwa ninafunga mabao kwa ajili ya kushindana
na mchezaji flani (Okwi), hapana mimi ninafunga kwa ajili ya kuiwezesha
timu yangu kutwaa ubingwa wa ligi kuu.
“Mimi bado nina deni kubwa na Yanga ambalo bado sijalilipa kama
unavyokumbuka wakati ninasajiliwa kuja Yanga nilitoa ahadi kadhaa
ikiwemo hii ya ubingwa wa ligi kuu, hivyo ni lazima niitimize.
“Hivyo, nitaendelea kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao
kama kawaida na kama ikaja kutokea mwishoni mwa msimu ninakuwa mfungaji
bora, basi nitashukuru Mungu kwani haikuwa mipango sana,” alisema
Ajibu.
Okwi, anaongoza kwenye ufungaji akiwa amefunga mabao 7 akifuatiwa na
Mohamed Rashid wa Prisons (4), Habib Haji wa Mbao FC, Shiza Kichuya
(Simba), Eliud Ambokile (Mbeya City) na Ajibu wote (3).
0 Comments