humph the GREAT
JUZI Jumamosi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera
Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa katika Uwanja wa Kaitaba
uliopo mjini Bukoba mkoani Kagera. Katika mchezo huo, Obrey Chirwa na
Ibrahim Ajibu ndiyo walioifungia Yanga mabao mawili, huku lile la Kagera
likifungwa na Jaffar Kibaya.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata ushindi huo ugenini, lakini ngoja
nikwambie kikubwa ambacho kilichoibeba timu hiyo inayonolewa na Mzambia,
George Lwandamina. Yanga imekuwa ikicheza vizuri sana kwenye viwanja
ambacho vina sehemu nzuri ya kuchezea. Miongoni mwa viwanja hivyo ni
Taifa, Uhuru, Azam Complex na Kaitaba. Mbali na hivyo, vilivyobaki vyote
havipo vizuri.
Ukiangalia Uwanja wa Kaitaba, ulikuwa ukiwaruhusu Yanga kucheza
wanavyotaka na kujiona kama walikuwa nyumbani, hiyo ndiyo sababu kubwa
iliyowafanya kuibuka na ushindi huo ujapo si mkubwa sana. Ushindi ni
ushindi tena hasa ukiwa ugenini unatakiwa kujivunia kwani timu nyingi
zimekuwa zikipoteza zikienda ugenini tofauti na zinapokuwa katika
viwanja vyao vya nyumbani.
Hivi sasa Yanga inakwenda Shinyanga kucheza na Stand United ambapo
mchezo wao utapigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani
humo. Uwanja huo ni mmoja kati ya viwanja vinavyolalamikwa kwamba havina
ubora sehemu ya kuchezea. Mchezo huo ujao kwa Yanga ndani ya Uwanja wa
Kambarage, unaweza kuwa mgumu kwao kutokana na hali ya uwanja ilivyo.
Tuliona Simba ilipokwenda kucheza na timu hiyo uwanjani hapo, ilipata
ushindi wa 2-1 lakini kwa tabu sana. Sasa Yanga sijui itakuwaje.
Tukiachana na hilo, wiki iliyopita nilisema kwamba mechi za wikiendi hii
zitakuwa na ushindani mkubwa na zinaweza kubadilisha kabisa sura ya
msimamo wa ligi hiyo na kweli ikawa hivyo.
Waliokuwa juu wameshuka na wale waliokuwa chini wamepanda. Hiyo yote
ni kudhihirisha kwamba hakuna timu ya kuibeza kwenye ligi hiyo
inayoshirikisha timu 16. Tumeona ushindi wa Yanga juzi, uliwafanya kukaa
kileleni wakifikisha pointi 12. Hiyo ni kabla ya jana Simba
haijapambana na Mtibwa Sugar. Mechi zingine za wikiendi tuliona Singida
United ambao walianza vizuri, wamepata sare dhidi ya Ruvu Shooting, huku
Azam nao ambao walikuwa wakipambana na Mwadui, wakitoka sare.
Ndanda na Majimaji zilitoka 1-1, huku Njombe na Lipuli zikishindwa
kufungana. Ugumu huo wa ligi unanifanya niendelee kuamini kwamba msimu
huu bingwa hawezi kutabirika mpaka sasa, tunasubiri kuona huko mbele
itakuwaje. Msimu uliopita tulishuhudia Yanga ikichukua ubingwa kwa
tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba, jambo kama hilo
linaweza kutokea kwa msimu huu pale atakapoamuliwa bingwa, lakini
inaweza kuwa zaidi ya hivyo, yaani zaidi ya timu mbili zikafungana
pointi kutokana na hiki kinachotokea sasa
0 Comments