humph the GREAT

Abdul Juma ‘Baba D’
Erick Evarist na Gladness mallya
DAR ES SALAAM: Maskini wee! Baba
wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Juma
‘Baba D’ anaumwa sana! Ndivyo Risasi Mchanganyiko linavyoweza
kukuhabarisha baada ya mzazi huyo kuzidiwa ghafla na kukimbizwa
hospitalini kutibiwa kwa msaada kutokana na kukosa fedha, twende hatua
kwa hatua.
NI JUMAPILI ILIYOPITA
Tukio hilo la kusikitisha la baba mzazi
wa msanii ambaye anatajwa kuwa na ukwasi wa kutosha Bongo, lilijiri
Jumapili iliyopita ambapo kwa msaada wa Dk. Fadhili Emily wa Kituo cha
Tiba cha Fadhaget Sanitarium kilichopo Mbezi Beach-Africana, Dar, baba
Diamond alifikishwa kutoka nyumbani kwake Magomeni-Kagera hadi
hospitalini hapo na kupatiwa matibabu.
CHANZO CHAVUJISHA
Awali, Risasi Mchanganyiko lilipokea
taarifa za mzee Abdul kuzidiwa nyumbani kwake lakini ikaelezwa kwamba,
hakuwa na msaada wowote hadi majirani walipopata mawasiliano ya daktari
huyo na kumuomba amsaidie.
“Jamani baba D (baba Diamond) yupo hoi
hapa nyumbani kwake Magomeni. Miguu inamuuma, anashindwa kutembea na
ukizingatia hana kipato, anashindwa pia kwenda hospitali. Na bahati
mbaya kwa muda mrefu hata majirani wamekuwa wakimsaidia lakini bado
hajapata tiba sahihi.”
AUNGANISHWA NA DK. FADHILI
“Leo (Jumapili) kuna jirani yake mmoja
hapa ndiyo amepata wazo baada ya kusoma Gazeti la Risasi Jumamosi (ndugu
na hili), amepata namba za Dk. Fadhili katika makala anazoandika
gazetini kuhusu afya. Akampigia na kumuomba msaada na bahati nzuri dokta
huyo ameguswa na tatizo la mzazi huyu, amemtumia nauli ya teksi ili
akimbizwe hospitalini kwake, sasa hivi ndiyo wanaelekea huko,” kilisema
chanzo hicho.
MAKACHERO WAUNGA TELA
Licha ya kuwa muda huo ulikuwa umeyoyoma
(saa 1 usiku), makachero wetu waliingia mzigoni kuelekea moja kwa moja
Mbezi kwenye hospitali hiyo na kumkuta baba D akiwa anaingia mapokezi
katika kliniki hiyo.
Akiwa mapokezi, makachero wetu
walimshuhudia baba Diamond akisaidiwa na vijana wawili ambao ni wahudumu
wa hospitali hiyo, walimkalisha kwenye kochi kisha wakaanza kumpa
huduma ya dharura ambapo walimpima presha na kumuita Dk. Fadhili atazame
miguu yake.
KUHUSU MIGUU
Dk. Fadhili alipofika, alimvua soksi
baba huyo na kuikagua vizuri miguu hiyo kabla ya kuingia naye ndani
katika chumba maalumu cha vipimo na matibabu.
Ilibainika kuwa, miongoni mwa vipimo
alivyopimwa baba D ni pamoja na kile cha Quantum Magnetic Analyzer ‘QMA’
ambacho kazi yake ni kutambua magonjwa mbalimbali ndani ya mwili wa
binadamu. Hata hivyo, Risasi Mchanganyiko halikufanikiwa kujua kipimo hicho kilitambua nini!
BABA DIAMOND AFUNGUKA
Baada ya kupimwa na kupatiwa dawa za
kutumia, baba Diamond aliliambia gazeti hili kuwa, anamshukuru daktari
huyo kwani ameweza kugundua tatizo linalomsumbua na kwamba anaamini dawa
alizopewa zitamsaidia.
“Kwa kweli ni Mungu tu, hali yangu ni
mbaya, miguu inanisumbua kwa zaidi ya miaka nane sasa. Inauma, imevimba
na inabadilika rangi kuwa myeupe. Inakuwa kama inatoka mabakamabaka.
Kiuchumi siko vizuri kabisa.”
“Dk. Fadhili amenipima, amebaini ngozi
yangu imeathirika vibaya. Amenitajia tatizo langu kitaalamu na amenipa
dawa za kutumia, lakini pia amenielekeza mazoezi maalum ambayo natakiwa
kuyafanya,” alisema baba Diamond huku uso wake ukijaa simanzi.
AMWAGA SHUKRANI
Baba Diamond alipoulizwa kama alimueleza
mwanaye Diamond kuhusu suala hilo wakati alipozidiwa, alisema hakuona
na haoni sababu ya kumwambia kwani analijua na hapendi kuendeleza
malumbano na mwanaye lakini anamshukuru Dk. Fadhili kwa kujitolea
kumsaidia bila malipo yoyote.
“Sipendi kuendeleza malumbano,
ninachokiangalia kwa sasa ni miguu yangu. Nitamshukuru Mungu zaidi
nitakapopona kabisa maana nimeshahangaika nayo sana. Kipekee, kutoka
moyoni nimshukuru Dk. Fadhili kwa kusikia kilio changu na kunisaidia
bure.
“Sikutegemea, mtu unaumwa, anakwambia
anakutumia fedha ya teksi uende hospitalini kwake akakutibu bure. Ni
upendo wa hali ya juu na Mungu amzidishie, pale alipotoa apabariki na
apate zaidi,” alisema baba Diamond.
DIAMOND ANASEMAJE?
Gazeti hili lilifanya jitihada za kutaka
kumsikia Diamond anazungumziaje suala hilo la ugonjwa hadi kufikia
mzazi wake kusaidiwa na mtu baki, simu yake haikuwa hewani lakini hata
alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia Mtandao wa WhatsApp
ulioonesha ameusoma, bado hakujibu chochote.
TUMEFIKAJE HAPA?
Baba Diamond amekuwa akisumbuliwa na
ugonjwa huo wa miguu ambapo awali, mzazi huyo alisema anasumbuliwa na
kansa ya ngozi lakini hata hivyo, mwanaye Diamond amekuwa mzito
kumsaidia kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni mwanaume huyo
kumtelekeza mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ yeye akiwa mdogo.
MAJIBU YA DK. FADHILI
Juzi Jumatatu, Risasi Mchanganyiko
lilimpigia simu daktari huyo na kumuuliza kuhusu tatizo la baba Dimaond
na namna alivyolishughulikia, ambapo alijibu:
“Ha! Jamani, ugonjwa wa mtu ni siri kati yake na daktari, labda kama ataona sawa aseme yeye mwenyewe.”
Tags
Udaku