humph the GREAT
Hassani Athumani akiugulia.
MARA:
Ama kweli kabla hujafa hujaumbwa! Kijana Hassani Athumani (30) mkazi wa
Kiabakari, Kata ya Kukirango, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara anaishi na
risasi mwilini kwa miaka nane sasa huku akiwa anasikia maumuvi makali
na mwili wake ukiwa umejaa vidonda kutokana na kulala muda wote.
Kijana huyo amepata masaibu hayo baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi Machi 6, 2008.
Akisimulia juu ya tukio hilo Ijumaa ya
wiki iliyopita nyumbani kwao akiwa amelala huku akitokwa na machozi
kutokana na kudhoofika mwili wake kuanazia sehemu ya mgongo aliyopigwa
risasi hadi miguuni, Hassani alikuwa na haya ya kusema:
“Hiyo Machi sita mwaka 2008 tulikuwa
tunacheza disko na wenzangu katika ukumbi mmoja uliopo Kiabakari, ghafla
saa 4.30 usiku, majambazi yakiwa yamevalia makoti meusi na kufunika
nyuso zao, yalivamia katika ukumbi huo na kuamuru wote tulale chini
kisha wakaanza kurusha hovyo risasi, ambapo risasi mbili zilinipata moja
ikaingia mgongoni na nyingine ikaniparaza kichwani.
“Baada ya kupigwa risasi hizo,
nilianguka na kupoteza fahamu na nilipopata fahamu nilijikuta nikiwa
katika Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini Musoma ambako nilipelekwa na
wasamaria wema ambako nilitibiwa kwa siku mbili kisha kuhamishiwa katika
Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
“Nilikaa Bugando kwa miezi sita bila
kupona na kushauriwa na madaktari wa hospitali hiyo kuwa hawana uwezo wa
kuondoa risasi mgongoni badala yake niende nchini India, nilishindwa
kwenda huko kwa sababu ya ukosefu wa fedha na nikarudishwa nyumbani
ambako naendelea kuteseka hadi leo nikiwa na risasi hiyo mwilini kwa
miaka nane sasa.
Hassani Athumani kabla hajapigwa risasi.
“Niliambiwa na madaktari kwamba risasi
iliyoingia mgongoni iliingia ndani ya uti wa mgongo na kukata mishipa
yote ya fahamu na tangu siku hiyo ya tukio nimelemaa moja kwa moja
kuanzia eneo ilipoingia risasi hadi miguuni.
“Nimekuwa mlemavu wa miguu bila
kutarajia, sina matumaini yoyote ya kurudia hali yangu ya mwanzo maana
mwili umeingia ganzi na miguu imekuwa myembamba kabisa, sina fedha ya
kwenda India, sasa nimejikabidhi kwa Mungu, sijui nilikosa nini kwa
muumba wangu hadi kupewa adhabu hii!
“Najiuliza kila kukicha nani atanitunzia
mtoto wangu ambaye mama yake alishafariki, kwetu hatuna uwezo, sina
baba nina mama pekee anayeishi kwa kuuza samaki wa kukaanga, najisaidia
haja kubwa na ndogo hapa nilipolala, sina uwezo wa kuamka, mama yangu
kila wakati ananibadilishia matandiko kama mtoto mchanga…,” alishindwa
kujieleza Hassani akawa analia kwa kwikwi!
Mgonjwa huyo ana vidonda sehemu kadhaa
za mwili kutokana na kile alichosema kulala kwa muda mrefu kwa kuwa huwa
anashindwa kujigeuza.
Yeyote atakayeguswa na habari
hii na anahitaji kumsaidia Hassani awasiliane naye kwa namba yake ya
simu 0765 435 782 au ya mama yake mzazi 0754 309 645, kutoa ni
moyo.
Tags
HABARI