Laana ya titi la mama’ke, amuua nduguye kwa mchi

humph the GREAT
 Mauaji (1)  
Mama mzazi wa marehemu na mtuhumiwa,  Mwaija Bakari.
Humphrey, blogger
MAJALIWA Mzaramingo, mkazi wa Chalinze mkoani Pwani, amemuua kaka yake kwa kumpiga kichwani na mchi, ikidaiwa ni laana iliyotokana na kushindwa kutekeleza masharti aliyopewa, baada ya kunyonya titi la mama yake mzazi.
Mauaji (2)Akizungumza na gazeti hili, mama mzazi wa marehemu na mtuhumiwa,  aliyejitambulisha kwa jina la Mwaija Bakari (pichani) alisema awali, Majaliwa alikuwa mlevi wa kupindukia, lakini hivi karibuni alikwenda kwa kiongozi mmoja wa dini, akiomba maelekezo ya namna ya kuacha pombe.
“Ukweli tukio hili linanipa uchungu sana, kwani sasa ni kama nimeshapoteza watoto wawili kwa mpigo, ukweli mtuhumiwa alikuwa na tabia ya ulevi uliopindukia na hivi karibuni alikwenda kwa ustaadhi f’lani akamuelekeza jinsi ya kuacha pombe.
“Ustaadhi huyo alimwambia aje aniambie nilioshe ziwa langu la kushoto, kisha alinyonye huku akinuizia na maji niliyooshea mengine ampelekee.
“Mwanangu alifanya hivyo na mwanzoni aliacha kabisa pombe, lakini siku za hivi karibuni alirudia tena kwa kasi, ingawa ustaadhi huyo alishamuonya kuwa kama angerudia kuonja kilevi basi yatakayomtokea asije kumfuata tena.
“Sasa siku ya tukio wote tukiwa hapa nyumbani marehemu Mwalimu alikuwa akijisikia homa hivyo hakwenda kazini. Mtuhumiwa alimwambia kaka yake wachange ili wanunue kitoweo kwa ajili ya chakula cha jioni.
“Marehemu alimwambia mdogo wake kuwa leo sina pesa, si unajua mimi naumwa sijatoka kwenda kutafuta.
“Baada ya kusikia hivyo mtuhumiwa alianza kumshutumu kaka yake kuwa alikuwa na pesa lakini alijifanya bahili ili amtegee.
“Hivyo Majaliwa alienda kununua nyama na kumpa mkewe apike, lakini akaagiza kaka yake asipewe hata kipande kimoja kwa kuwa hakuchangia chochote.
“Mkewe alikarangiza na ulipofika muda wa kula, kwa kuwa mtuhumiwa hakuwepo, mkewe akamchotea kidogo shemeji yake.
“Wakati marehemu akiendelea kutafuna, mtuhumiwa alitokea ghafla na kumuuliza kwa nini alikuwa akila kitoweo ambacho alimuagiza asikiguse.
“Hali hiyo ilizua malumbano kabla ya Majaliwa kuchukua mchi wa kutwangia na kumpiga nao kaka yake kichwani mara tatu, alianguka na kuanza kugaragara.“Nilipoona hali hiyo nilianza kupiga mayowe kuomba msaada, wasamaria wema walifika lakini mtuhumiwa alishakimbia. Tulimkimbiza zahanati ya serikali hapa jirani lakini walisema hali yake ilikuwa mbaya hivyo tumkimbize Hospitali ya Rufaa ya Tumbi iliyopo Kibaha.
“Tukiwa maeneo ya Kongowe kuelekea Tumbi mwanangu aliaga dunia, jamani sasa nimekosa watoto wawili kwa mpigo, huyu amekufa na mtuhumiwa naye siwezi kuwa naye tena ni lazima atafia jela,” alisema mama huyo huku akilia.
Kufuatia tukio hilo, waandishi wetu walimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Bonaventura Mshongi lakini simu yake haikuwa hewani.
Marehemu alizikwa kijijini hapo Juni 30, mwaka huu.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post