humph the GREAT
WAKATI
vichwa vya habai nyingi za michezo hapa nchini ikiwa ni kuhusu sakata
la Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji kudaiwa kujiuzulu nafasi
yake hiyo, taarifa ambazi zilianza kusambaa jana kwenye mitandao ya
kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, mwanachama mkongwe wa klabu
hiyo, Ibrahim Omary Akilimali maarufu kwa jina la Mzee Akilimali ametoa
kauli tata juu ya sakata hilo.
Ikiwa mpaka sasa Manji hatatoa tamko
lolote juu ya uamuzi wake huo wa kujiuzulu, Mzee Akilimali amenukuliwa
akisema kuwa kuna watu wa Yanga wamemuita ili kuzungumza kuumaliza
mvutano unaoendelea ambapo inaelezwa kuwa mzee huyo amechangia maamuzi
ya Manji kujiondoa Yanga kutokana na kumshutumu kwa maneno mengi.
Akihojiwa na kituo cha Radio cha EFM,
leo asubuhi Mzee Akilimali alinukuliwa akisema: “Msitake kuyakuza haya
mambo, subirini kwanza nataka tuyamalize, mimi wameniita ndiyo maana
nipo huku ili kuyamaliza.”
Alipoulizwa yupo wapi na ameitwa na
nani, Akilimali alisema: “Nimekwambia nimeitwa huku, wewe subiri kwanza
tuyamalize kisha utanipigia, subiri baada ya nusu saa nitakubeep
unipigie.”
Licha ya kuendelea kubanwa kufafanua zaidi juu ya kinachoendelea, mzee huyo alisisitiza kuwa pigiwe baadaye na kukata simu.
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa Mzee Akilimali ameibuka na kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa ikiwemo kuomba radhi kwa kauli zake.
Baadaye alipopigiwa simu mzee huyo
alisikika kama mtu ambaye amepoa na kuwa mpole ambapo alisema anawaomba
radhi Wanayanga kama atakuwa amewakosea kwa kauli zake lakini nia yake
ni kuitaka Yanga iwe moja na Manji aonyeshe heshima kwa wazee wa klabu
hiyo.
“Manji ni kijana wetu, sisi wazee
nikiwemo mimi tulichangia yeye kuingia ndani ya Yanga, hata mimi ndiye
niliyemkabidhi ngao ya uchifu wa Yanga, sasa hapo katikati alikuwa
hatushirikishi sisi wazee kama ilivyokuwa zamani.
“Akawa anafanya maamuzi anayoyajua yeye, nia yetu sisi wazee ni
kuifanya Yanga iwe moja kuwe na mshikamano, unajua Manji ametutoa mbali,
sisi ni Yanga moja, kwa mapenzi yangu yote nataka Yanga iwe kitu
kimoja. Yanga ni moja na hakuna mpasuko.” Alisema Mzee Akilimali.
Mzee Akilimali ni mzaliwa wa Kigoma, ambapo anadai alianza kuipenda Yanga tangu miaka ya 1950.
Tags
Michezo na burudani